NISHATI YA KUPIKIA:Kuni mkaa sikia, tutaacha kuzitumia

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA Mosi, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametaja mikakati mitatu mikubwa itakayotekelezwa haraka na Serikali yake kuhakikisha ndani ya miaka 10 ijayo kuanzia sasa nchi inaweza kufikia asilimia 80 hadi 90 ya uwepo wa nishati safi na endelevu ya kupikia ifikapo 2032.

Picha na SimGas / Courtesy of Global Alliance for Clean Cookstoves.

Ameyabainisha hayo wakati wa ufunguzi wa mjadala wa nishati safi ya kupikia uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Rais Samia amesema, miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuunda kikosi kazi, kutengwa kwa fedha mwaka ujao wa bajeti ya Wizara ya Nishati na kuanzishwa kwa Mfuko wa Nishati Safi na jambo la tatu taasisi zote za serikali zenye kuhudumia watu zaidi ya 300 zianze kutumia nishati mbadala ikiwemo gesi na kuachana na mtumizi ya kuni au mkaa.

Amesema, nishati safi ya kupikia ni mjadala mpana, unaopaswa kuja na mawazo ya pamoja kwa kuwa suala hilo linaibua changamoto nyingi kwa jamii na ni lazima kama Serikali ianze kuchukua hatua za haraka. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,mpango wa nishati safi, siyo kuni na mkaa, endelea;
 
1:Nishati ya kupikia, ndiyo waijadilia,
Ambayo tunatumia, na ile tutatumia,
Lengo tuweze fikia, pazuri Watanzania,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

2:Mjadala meingia, hapahapa Tanzania,
Namna ya kufikia, malengo twayawania,
Tuweze kutupilia, mambo ya kujiwangia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

3:Miaka kumi sikia, kwingine tutahamia,
Kule tutakotumia, nishati ya Tanzania,
Ile safi nakwambia, shidani sijeingia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

4:Rais wetu Samia, ndiyo ametuambia,
Pazuri kupafikia, mipango inaingia,
Sote tuje furahia, mbadala kuingia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

5:Uhamisho wanukia, nishati ya kupikia,
Kuni mkaa sikia, tutaacha zitumia,
Mazingira kuvutia, siyo kujiharibia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

6:Nishati ya kupitia, ikiwa ya kuvutia,
Hapo twawasaidia, wanawake Tanzania,
Moshi unawaishia, kuni wanazopigia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

7:Jinsi tunavyotumia, nishati safi sikia,
Ndivyo twawapunguzia, shida wanazopitia,
Pia tunasaidia, mazingira jitunzia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

8:Hapa tunafurahia, Mungu ametujalia,
Tuna gesi asilia, ambayo twajivunia,
Vema tukiitumia, malengo tutafikia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

9:Hata magari sikia, gesi hiyo yatumia,
Kule kujiagizia, mafuta tajishushia,
Fedha tunazotumia, nchini zitasalia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

10:Mifugo kwa Tanzania, ni mingi twashangilia,
Nayo twaweza tumia, nishati kuzalishia,
Bayogesi nakwambia, kupikia yavutia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

11:Wataalam twasikia, nishati zungumzia,
Kile tunakitakia, suluhisho tupatia,
Nishati ya kupikia, safi ya kufurahia,
Mpango nishati safi, siyo kuni na mkaa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news