Kamati ya Bunge yaguswa na kasi ya NHC, yampa saluti Rais Samia

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lipate fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ambayo ilikwama awali.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa wa Kamati hiyo, Mheshimwa Ally Makoa leo Novemba 15, 2022 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipofanya ziara katika miradi mbalimbali ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa miradi iliyotembelewa na kamati hiyo huku ikitoa pongezi kutokana na kutekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu huku ikitarajiwa kukamilika hivi karibuni ni Mradi wa Morocco Square na Samia Housing Scheme uliopo Kawe Tanganyika Packers.

"Tunatembea miradi ya National Housing, kwanza tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuruhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lipate hizi fedha za kutekeleza miradi hii ambayo ilikwama kwa muda mrefu.
"Kwa kweli kamati imetembelea na kuona mawazo na fikra za Mheshimiwa Rais Samia ni jambo jema sana Shirika la Taifa la Nyumba kupata hizo fedha za kutekeleza hii miradi.

"Miradi inafaida kubwa, haya majengo tulizoea kuyaona nchi za Ulaya, kwa sasa tunayaona Tanzania, tunampongeza Mheshimiwa Rais, tunaipongeza Wizara (Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuiendeleza hii miradi. Miradi ilikwama na hela nyingi za Serikali zilipotea, lakini sasa hivi kwa vile imefufuka tunatarajia kwamba tunakwenda sasa kuonesha juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu.

"Ni matarajio ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuona kwamba miradi hii sasa imeanza na inakwenda mpaka mwisho, maana yake ikienda mpaka mwisho italeta tija, isipoenda mpaka mwisho haitaleta tija,"amefafanua Mheshimiwa Makoa.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa kamati ya kudumu amebainisha kuwa, "Sisi wito wetu kama kamati, tunaitaka sasa Wizara isimamie na tunalitaka Shirika la Nyumba sasa kwa sababu limeshapewa uwezo lifanye haraka sasa kwa viwango vinavyohitajika kuhakikisha hii miradi inakamilika.

"Na tumefuatilia mipango ya Shirika la Nyumba ni mikubwa na mizuri, kama hii mipango itatekelezwa tija itakuwa kubwa sana katika taifa letu.

Mwenyekiti wa wa Kamati hiyo, Mheshimwa Ally Makoa akizungumzia kuhusu uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) itakayofanyika kesho Novemba 16, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, amesema ni jambo la heri sana.

"Ni jambo jema kwa sababu tunatarajia majengo haya na miradi hii ifanyike nchi nzima, kuliachia shirika peke yake ni mzigo mkubwa sana. Faida kubwa ambayo tutaipata kwa ubia ni kwamba miradi mingi inakwenda kufanyika maeneo mengi,majengo na miradi hii inakwenda kufanyika kwa ubia kwa kushirikiana na shirika na wabia mbalimbali.
"Wito wetu kwa wabia kesho tutafanya uzinduzi, matarajio yetu tutakuwa na washiriki wengi watakaoshiriki na kwa kweli sisi tumeona mipango ni mikubwa na mizuri na kama itatekelezeka basi tutakuwa na tija kubwa sana," amesema Mheshimiwa Makoa.

Katika uzinduzi huo, zaidi ya washiriki 1,000 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki.

Washiriki hao wanajumuisha vyama,Bodi za Kitaaluma, Balozi zaidi ya 20, taasisi za kimataifa 10, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Wenyeviti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mawaziri, Mhimili wa Mahakama, taasisi za fedha na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi.

Mikataba

Mheshimwa Ally Makoa akizungumzia kuhusu mikataba amesema, "Na sisi angalizo letu ni hilo tunapoingia kwenye mikataba lazima tuhakikishe kuna uadilifu kwenye mikataba. Haki na uwazi lazima iwepo kwenye mikataba na kuangalia zaidi taifa kunufaika zaidi sio kuleta hasara, unajua mikataba mingine inaweza ikasababisha hasara lazima kuwepo na tahadhari zaidi.

Wajumbe

Kwa upande wake Mjumbe wa kamati hiyo, Timotheo Mzava ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini amesema kuwa, "sisi kama kamati tumetembelea mradi tumeuona, tumeridhika na kazi inayofanyika hapa kwa maana ya viwango na ubora wa kazi tunaipongeza wizara, Shirika na Mheshimiwa Rais kwa kuruhusu fedha hizi zitoke kufanya kazi hii.
"Malengo ni kuhakikisha miradi inakamilika, sisi kama kamati kwa miaka mingi tumekuwa tukishauri moja Shirika la Taifa la Nyumba kuanzisha miradi ambayo wataweza kuianza mpaka kuimaliza.

"Pili tumekuwa tukisisitiza usimamizi wa mikataba na tumefurahi kwa jambo kubwa ambalo limefanyika kwa Sera ya Ubia kutokana na ushauri wa wabunge.Shirika linakuja na Organization Structure ya Shirika la Taifa la Nyumba ambapo tunaamini kwa asilimia kubwa inatoa kipaumbele kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa sababu ndio wasimamizi wa mikataba na pia shirika kuhakikisha halipati hasara na linafanya kazi kwa umakini,"amesema Mheshimiwa Mzava.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo,Mheshimiwa Dkt.Florence George Samizi Mbunge ambaye ni Mbunge wa Muhambwe anampongeza Mheshimiwa Rais Samia Hassan kwa uamuzi wake madhubuti wa kukwamua miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa ambayo ilikuwa imekwama kwa muda mferu ambapo ikimalizika amesema italeta tija.

"Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kukwamua miradi hii ambayo ikikamililika italeta tija na tayari ilikuwa imeshatekelezwa kiasi,lakini ikasimama.

"Pongezi nyingi kwa uamuzi huu wa Mheshimiwa Rais kuamua miradi hii ikwamuliwe basi tunaamini shirika litakwenda kufanya vizuri kuimaliza hii miradi kwa ajili ya kuwanufaisha watanzania.
"Kuhusu sera hii ya ubia tunakwenda kuizindua kesho niseme tu kwamba kwamba miradi hii kuliachia shirika peke yake kuitekeleza basi itatekelezwa kwa muda mrefu kupitia ubia maana yake kwamba miradi hii itatekelezwa kwa haraka zaidi.

"Tunafahamu wananchi wanaohitaji nyumba za bei nafuu ni wengi,kwa hivyo tunaamini miradi hii itakuwa na urahisi na wananchi wenye uhitaji wa nyumba wakae tayari kwa sababu sasa watakwenda kujipatia nyumba na wabia wataenda kuwekeza na watajenga nyumba nyingi kwa wakati mfupi, tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana kwa sababu mtaji wa hizi nyumba ni mkubwa sana.

"Sisi kama wajumbe wa kamati hii tunamuunga mkono kuhakikisha tunasimamia vizuri shirika hili liweze kufanya vizuri kwa ukweli na uwazi,"amesema Mjumbe huyo wa Kamati.

Katibu Mkuu

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amesema,fedha kwa ajili ya kufanikisha mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) uliopo Kawe Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam zipo na mradi huo kwa awamu ya kwanza unatarajiwa kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja.

"Siku ya leo tumepitia hapa katika huu mradi wa nyumba za makazi ambao umepewa jina la Samia au kwa Kiingereza Samia Housing Scheme. Huu ni mradi wa makazi nafuu kwa ajili ya Watanzania, kama mnavyofahamu Watanzania wana vipato tofauti tofauti, kuna ambao wana kipato cha chini, vipato vya kati na vipato vya juu. Kwa hiyo niseme kwamba, mradi huu ambao unaendelea katika eneo hili ni mradi kwa ajili ya Watanzania wenye kipato cha kati.
"Na mradi huu unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa ambao wana miradi mbalimbali na hii ni sehemu ya miradi ambayo inatekelezwa. Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu zipo. Na ndiyo maana unaona kwamba shughuli za kufanya maandalizi ya awali kuanza ujenzi zinaendelea kwa kasi.

"Kwa hiyo niwathibitishe watanzania kwamba, tumejipanga vizuri. Kwa kupitia Shirika letu la Nyumba, kazi imeanza na kwa mpango kazi uliopo tunategemea kazi hii itakamilika ndani ya mwaka mmoja, kwa maana ya awamu ya kwanza. Baada ya hapo tutakwenda awamu ya pili na tatu,"amesema Dkt.Kijazi.

Post a Comment

0 Comments