Kamati ya Dkt.Mwakyembe yafukua yasiyofahamika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST)

NA DIRAMAKINI

NOVEMBA 20, 2022 Mwenyekiti wa Kamati ya Tathimini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST),Mheshimiwa Dkt.Harrison G.Mwakyembe amewasilisha ripoti kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt.Damas D.Ndumbaro.
Wasilisho hilo limefanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention Centre-JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mheshimiwa Dkt. Damas D.Ndumbaro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria wengine walioshiriki katika hafla hiyo ni Bi. Mary Makondo, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, wanakamati, Prof. Lazaro Lukumay, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo,viongozi waandamizi wa Serikali na waandishi wa habari. Ungana na Dkt.Mwakyembe hapa chini, endelea;

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya na kutuwezesha leo hii kukutana hapa kwenye Ofisi za Wizara Dar es Salaam, kukukabidhi rasmi Taarifa ya Kamati uliyoiunda tarehe 13 mwezi uliopita wa Oktoba kufanya Tathmini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania au Law School of Tanzania, ambayo katika mkutano wetu wa leo, nitaiita kwa kifupi Law School, LST au Taasisi

Mheshimiwa Waziri, uliniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati hii, na wanasheria wenzangu 6 kuwa wajumbe wa Kamati:

1. Mhe. Sirilius Matupa, Jaji Mstaafu, Mahakama Kuu ya Tanzania;
2. Mhe. Assaa Ahmad Rashid, Mwenyekiti, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Zanzibar;
3. Bi. Mary Stephen Mniwasa, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Soko la Hisa Dar es Salaam;
4. Bi. Gloria Kashununu Kalabamu, Makamu wa Rais, Chama cha Wanasheria Tanganyika;
5. Bi. Alice Edward Mtulo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali; na
6. Bw. John John Kaombwe, Mhitimu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo LST, Kundi la 33.

Mhe. Waziri, kwa niaba ya wajumbe wenzangu wote wa Kamati, naomba nitumie nafasi hii kukushukuru kwa dhati kwa heshima kubwa uliyotupa kwa kutuamini na kututeua kuwa wajumbe wa Kamati hii adhimu katika mustakabali wa maendeleo ya sekta nzima ya sheria nchini.

Naomba vilevile, kwa niaba ya wajumbe wenzangu, nimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara Bi. Mary Makondo kwa kuiwezesha Kamati kutekeleza majukumu yake bila vikwazo na kutupatia sekreterieti ya vijana wanasheria
watatu wachacharikaji:

1. Bw. Griffin Venance Mwakapeje, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kwa Umma, WKS;
2. Bw. Moses Marko Mkapa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi; na
3. Dkt. Dafina Ndumbaro, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Waziri, uliamua kuunda Kamati hii baada ya mjadala mkubwa kuibuka nchini kufuatia kutangazwa (tarehe 5 mwezi uliopita wa Oktoba) kwa matokeo ya mitihani ya Law School ya Kundi la 33 (au Cohort 33 kwa Kiingereza) la mwaka 2021/2022.

Kati ya Wanafunzi 633 wa Kundi hilo waliofanya mitihani hiyo, ni wanafunzi 26 ndio waliofaulu katika mkao wa kwanza (first sitting).

Wanafunzi 342 walifaulu baadhi ya masomo na wana fursa ya kurudia mitihani ya masomo waliyoshindwa watakapokuwa tayari, na 265 walifeli mtihani mzima lakini wanaweza kuanza upya mafunzo hayo wakati wowote watakapokuwa tayari.

Taarifa hazikupokewa vizuri na watahiniwa, wanafunzi wa sasa na waliopita wa Taasisi, wadau mbalimbali wa sheria na wananchi kwa ujumla na kuibua tuhuma nyingi, madai mengi yaliyoigusa Taasisi na mengine yakivigusa vyuo vikuu vinavyotoa shahada za sheria nk.

Hali hii ya kurushiana tuhuma na madai kupitia vyombo vya habari iliyoendelea kwa siku kadhaa, dhahiri haikukufurahisha wala kukusaidia Waziri mwenye dhamana.

Ndipo tarehe 13 Oktoba, 2022 ukaamua kuunda Kamati ya Tathmini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST).

Lengo la kuundwa kwa Kamati lilikuwa kufanya tathmini na kutoa ushauri kuhusu changamoto zilizopo katika mfumo wa utoaji wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo katika Taasisi (LST).

Katika kutekeleza uamuzi wako Mhe. Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara aliipa Kamati Hadidu za Rejea 16, zote zikilenga kukiainisha chanzo cha tatizo na kushauri njia za kuondokana na tatizo.

Kamati imezifanyia kazi Hadidu za Rejea zote. Baada ya kukamilisha taratibu zote za maandalizi ikiwa ni pamoja na
hadidu za rejea, wajumbe wote kukutana Dar kuanza kazi, sehemu ya kufanyia kazi nk.

Kamati ilianza kazi rasmi tarehe 17 Oktoba, 2022 na kukamilisha ndani ya siku 30 kama ulivyoagiza Mhe. Waziri.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mhe. Waziri kuwa baada ya pilikapilika za Bunge na majukumu mengine ya kusimamia Wizara, umejumuika nasi leo tuweze kukukabidhi rasmi Taarifa uliyotutuma tuiandae.

Mhe. Waziri katika kuzifanyia kazi Hadidu za Rejea na hatimaye kuandaa taarifa hii, Kamati iliweza kuitisha, kupitia na kuchambua taarifa mbalimbali kuhusu mfumo wa elimu ya Sheria kutoka Baraza la Elimu ya Sheria (au Council of Legal Education - CLE),Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Chuo Kikuu Iringa, Chuo Kikuu Tumaini (Ndaki ya Dar es Salaam), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo Kikuu cha Kiislam Morogoro, Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Zanzibar na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania.

Aidha, Mhe. Waziri, Kamati ilipokea maoni kutoka kwa wadau wapatao 141, kati yao 46 ana kwa ana, wadau 10 kupitia simu, na wadau 85 kupitia mitandao ya kijamii na barua pepe.

Wadau hao ni pamoja na: Viongozi wa Serikali wastaafu, Majaji wastaafu, watumishi wa vyuo vikuu vinavyotoa shahada ya kwanza ya sheria, Mawakili wa kujitegemea, Wahandisi, Wasanifu wa Majengo, Wakadiriaji Majenzi, Madaktari wa binadamu, Wakufunzi na Wafanyakazi wa Taasisi za Uanasheria kwa Vitendo pande zote mbili za Muungano, Wanahabari, wanafunzi wa makundi mbalimbali ya LST, Wajumbe wa Baraza la Taaluma ya Sheria LST, Watendaji wa TCU, NACTVET, na wadau wengine waliofika mbele ya Kamati ama kwa kuitwa na Kamati au wao wenyewe kuomba kusikilizwa na Kamati.

Vile vile, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuchambua na kutathmini maoni mbalimbali, Kamati ilitembelea miundombinu yote ya Taasisi, LST:

Maktaba, Mahakama, kumbi za mihadhara na madarasa, ukumbi mkubwa wa mihadhara, ofisi za waalimu na maafisa mbalimbali wa taasisi pamoja na ofisi za Viongozi wa wanafunzi (Rais na Makamu wake) na mazingira ya
Taasisi kwa ujumla.

Kwa nia njema Kamati, katika taarifa nzima imetumia ushahidi mbalimbali bila kutaja majina ya watu ila majina ya vyanzo rasmi vya maandiko na vya kitaasisi.

Aidha, ili kuendana na misingi ya haki asili, Kamati ilihakikisha inampa nafasi ya kujieleza kila aliyeguswa na ushahidi hasi na kuhakikisha kuwa maoni ya Kamati hayaathiriwi na mgongano wowote ule wa kimaslahi kwa upande wa Wajumbe wenyewe na Sekretarieti yake.

Mheshimiwa Waziri,

Baada ya kupitia na kuchambua taarifa na kuwasikiliza wadau mbalimbali,Kamati ilihitimisha taarifa yake tarehe 17 Novemba, 2022.

Taarifa hii imechambua hadidu za rejea zilizotolewa kwa Kamati, imebainisha changamoto zilizopo na kutoa ushauri utakaowezesha kuboresha mfumo wa elimu ya sheria na mafunzo ya uanasheria kwa vitendo nchini.

Mheshimiwa Waziri, taarifa hii ina Taarifa Kuu yenye kurasa 66, viambatisho 17 na majedwali 5. Majedwali hayo yamesheheni taarifa muhimu ambazo tunaamini Mhe. Waziri utazihitaji katika kufikia maamuzi mbalimbali ya kuimarisha elimu ya sheria nchini.

Kwa sababu Mheshimiwa Waziri taarifa hii ni ya kwako, nakuomba kwa niaba ya wajumbe wenzangu uipokee kwanza na kwa ruhusa yako tuuelezee umma wa Watanzania kupitia vyombo hivi vya habari, yale tuliyoyaona na ushauri wetu kwako, kwa muhtasari.

Mheshimiwa Waziri, kama nilivyosema awali, taharuki iliyojitokeza baada ya matokeo kutangazwa ya mitihani ya Law School, iliibua malalamiko mengi na tuhuma nyingi kuhusu Law School au Taasisi - kwamba taasisi yetu ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo imeng'ang'ana mno na mafunzo ya nadharia; kuna dhamira mbaya katika utungaji wa mitihani -lengo likiwa ni kuwakomoa wanafunzi; kuwepo katika taasisi upendeleo, uonevu, rushwa ya ngono na ya fedha, usahihishaji mbaya wa mitihani, kukosekana kwa uwazi katika utoaji wa matokeo ya mitihani na utaratibu
mbaya wa rufaa kulalamikia matokeo nk.

Wengine vilevile walijitokeza kuvilalamikia baadhi ya vyuo vikuu kwa kushindwa kuwaandaa wahitimu wao vizuri kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na wahadhiri wa kutosha na wenye sifa za elimu stahili, na vyuo vingine vililalamikiwa kwa kudahili wanafunzi wa kusomea sheria kibiashara, bila kuzingatia ufaulu mzuri wa mitihani ya kidato cha sita na nne ili mwanafunzi aweze kuhimili mchakamchaka wa shahada ya kwanza ya sheria.

Hoja zingine ziliwahusu baadhi ya wanafunzi kutokuwa na msingi mzuri wa kuimudu lugha ya kufundishia -Kiingereza na wengine kukosa ari na bidii stahiki ya kujisomea.

Kamati ilisikiliza hoja zote. Baada ya kufanya uchambuzi na tathmini ya kila kilicholetwa mbele yake, Kamati imebaini yafuatayo na kuyatolea ushauri:

1. Taarifa za matokeo ya mitihani ya Kundi la 33 LST hakika kama nilivyoeleza awali, izilizua tafrani miongoni mwa wananchi waliokuwa wanaufuatilia kwa karibu mjadala ulioibuka, wengi wakajenga fikra hasi kwamba pengine vijana wao wanaonewa, wanazuiwa kwa makusudi wasiwe mawakili.

Kamati inaamini kuwa laiti wananchi wangepewa picha yote kwa kiada, kusingelitokea mjadala mkubwa kama ulivyotokea.

Wananchi wengi tuliopata nafasi ya kubadilishana nao mawazo walifananisha mfumo wa ufaulu katika Taasisi hii na ule wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu. Shule za Msingi na Sekondari, mtoto akifeli mtihani wa mwisho ndiyo kwaheri.

Vyuo Vikuu, unapewa nafasi ya kufanya tena mitihani uliyoshindwa, baada ya hapo, vilevile ni kwaheri. Lakini katika Taasisi hii ya kitaaluma, unafanya mitihani ya masomo 10, ukifaulu yote katika mkao wa kwanza, hongera!
Ukishindwa kufaulu somo moja, mawili, matatu nk unayo fursa ya kurudia mitihani uliyofanya vibaya katika mkao wa pili ambao unaitwa Supplementary.

Ukishinda, hongera! Ukishindwa bado milango ya Taasisi inaachwa wazi ujaribu tena na tena na tena mpaka utakapofanikiwa.

Mkao wa Pili (Supplementary), mara zote hupelekea watahiniwa wengi zaidi kufaulu kuliko mkao wa kwanza. Takwimu zinathibitisha hilo. Mfano ni:

>Kundi la 31 la mwaka 2020/2021 ambapo wanafunzi 27 pekee kati ya 516 walifaulu katika mkao wa kwanza. Mkao wa pili (Supplementary) walifaulu 157 (kutoka 31);

>Kundi la 29 la mwaka 2019/2020, waliofaulu katika mkao wa kwanza walikuwa 54 kati ya wanafunzi 620. Ufaulu katika mtihani wa marudio ulipanda hadi kufikia wanafunzi 179 kutoka 54;

>Kundi la 22 la mwaka 2016/2017 waliofaulu mkao wa kwanza ni 53 kati ya 502. Katika mtihani wa marudio walifaulu 233 kutoka 53;

>Kundi la 19 la mwaka 2015/2016 walifaulu 80 katika mkao wa kwanza kati ya wanafunzi 528. Katika mtihani wa marudio walifaulu 279 kutoka 80;

>Kundi la 12 la mwaka 2012/2013 walifaulu wanafunzi 56 kati ya 338. Katika mtihani wa marudio walifaulu 206, karibu darasa zima!

>Kundi la 1 la mwaka 2008/2009 walifaulu wanafunzi 38 kati ya 274. Katika mtihani wa marudio wanafunzi 158 walifaulu kutoka 38.

Hii ndiyo hali halisi katika taasisi zote za kitaaluma hapa nchini na nje. Kwa mujibu wa Baraza la Madaktari la Tanganyika (MCT) kwa mfano, madaktari walio kwenye mafunzo ya udaktari kwa vitendo (ambao tayari wamehenya miaka 5 vyuo vikuu) bado wana wastani wa asilimia 40 tu kufaulu katika mkao wa kwanza wa mitihani yao.

Unaweza kusema huu ni uonezi, sawa. Lakini kuna siku utakumbuka faida za kuwa wakali katika kuchuja weledi, siku uko hospitali umelazwa, umekatwa mguu wa kushoto uliokuwa mzima, umebakizwa wa kulia wenye mgogoro!

Mwanasheria huyu huyu anayepita Law School, ndiye wakili wako wa kesho, hakimu wako wa kesho na jaji wako wa kesho kutwa.

Kuna siku utamkumbuka Jaji Benhaj, Mkuu wa Law School, siku uko mbele ya kijana aliyepita Law School kijanjajanja, lakini amebeba hatma ya haki yako, hatma ya maisha yako mikononi mwake. Unajua alikuwa kilaza, hajui hata tofauti ya ratio decidendi na obiter dictum.

Wafwa! Ukali, umakini katika kuchuja weledi hauko katika udaktari tu na uwakili. Hali hii inajitokeza vilevile kwenye mitihani ya kitaaluma ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu ambapo, katika mitihani iliyofanyika Novemba, 2021 watahiniwa 961 tu kati ya 5,809 walifaulu mitihani ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu
Tanzania (NBAA). Ufaulu huo ni sawa na asilimia 23.1.

Nchini Kenya, Wanasheria 290 kati ya 1,572, waliofanya mitihani ya uwakili mwaka 2018 walifaulu, sawa na asilimia 18.4.

Aidha, Nchini Uganda, kati ya wanasheria 1,474 waliofanya mitihani ya uwakili mwaka 2019/2020 ni wanasheria 145 pekee waliofaulu sawa na asilimia 9.8 ya wanafunzi wote.

Jamii inapaswa kutambua kwamba, LST inachuja kada ya kuja kulinda haki yangu na yako katika jamii. Hivyo LST, haina budi kutekeleza wajibu wake kwa weledi wa hali ya juu bila kuchakachua ubora.

Uzoefu unaonesha kuwa, mwanasheria mwenye ujuzi hafifu, daima atakimbilia njia za mkato, ikiwemo rushwa katika kushinda kesi kama wakili au kuamua kesi kama hakimu.

USHAURI WA KAMATI

Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, inabeba uzito mkubwa katika jamii yetu hivyo inao wajibu wa kujenga jukwaa la mawasiliano ya karibu na wananchi kupitia njia mbalimbali, vikiwemo vyombo vya habari kuelezea shughuli zake na kupokea maoni ya wanachi.

Katika hali kama hiyo, taarifa yoyote kuhusu Taasisi itawafikia wananchi ambao tayari wana uelewa na kinachoendelea katika Taasisi.

2. Pamoja na milango ya Taasisi kuwa wazi kwa kila mwanasheria anayetaka kuwa Wakili, Kamati imebaini uwepo wa hisia hasi upande wa wanafunzi katika Taasisi na wanasheria kwa ujumla kwamba, baadhi ya wakufunzi wa LST hawawatakii mema wanafunzi na hivyo wanawafelisha wanafunzi kwa makusudi.

Kamati ilipokea majina ya wakufunzi wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo na kuwapa nafasi ya kujieleza kuendana na misingi ya Haki Asili.

Walikana kuhusika na vitendo hivyo na kutaka waliotoa tuhuma hizo watoe ushahidi kwa mamlaka za juu za Taasisi. Vile vile, Kamati ilichunguza mfumo wa usahishaji wa mitihani katika Taasisi kama unatoa fursa kwa
wakufunzi kufanya uonevu kwa mwanafunzi yeyote. Uongozi wa Taasisi uliithibitishia Kamati kwa ushahidi kwamba mitihani yote ya LST husahihishwa na wasahihishaji watatu tofauti.

Pamoja na wasahihishaji hao watatu, kila somo lina msahihishaji kutoka nje ya Taasisi (External Examiner) ili kujiridhisha kuhusu utungaji wa maswali na usahihishaji wa karatasi za mitihani.

Aidha, kila mtihani una mwongozo wa usahishaji na wanafunzi wote hawatumii majina yao bali namba mahsusi katika mitihani yote.

USHAURI WA KAMATI

Pamoja na wadau kuwasilisha malalamiko ya rushwa, uonevu au upendeleo katika utungaji au usahihishaji wa mitihani, hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha tuhuma hizo.

Hata hivyo, kwa kuzigatia unyeti wa Taasisi na wajibu ilionao ambao unahitaji uadilifu wa hali ya juu, Kamati imewasilisha Majina ya Wakufunzi waliotajwa kwa uongozi wa juu wa Taaasisi ili uweze kufuatilia mienendo yao. 

Tuhuma zikiendelea, Kamati inashauri wakufunzi hao wahamishiwe katika Idara zingine za serikali ili kulinda taswira ya Taasisi.

3. Kamati imeshuhudia hekaheka za wanafunzi wakiingia kwenye kumbi za mihadhara na madarasani kwa ajili ya kushiriki vipindi, semina na mafunzo mbalimbali kwa vitendo, mathalani mahakama za mafunzo (moot courts), kesi za kugeza (mock trials) na maigizo ya uhalisia (simulations) kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.

Hali hii ya kukimbizana na masomo inataka iwepo huduma ya chakula jirani ili mwanafunzi aweze kupata huduma hiyo pale atakapohitaji na kurejea darasani mara moja.

Huduma ya chakula katika mazingira ya kitaaluma kama haya, yamepewa kipaumbele kwenye Taasisi zinazotoa mafunzo ya namna hii katika nchi za Kenya na Uganda.

Kamati vilevile, ilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanafunzi hususani watoto wa kike wanaotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam ambao wanadai kuishi katika mazingira magumu sana.

Hali hii imetokana na Taasisi ambayo inahudumia nchi nzima kutokuwa na hosteli walau chache kwa wanafunzi wanaotoka mbali na mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha, Kamati ilibaini kuwepo kwa baadhi ya miundombinu ya Taasisi iliyochakaa kutokana na kutokufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara kwa mfano: kutokufanya kazi kwa kangavuke (generator), uchakavu wa viti vya kukalia, mifumo ya sauti katika kumbi za mihadhara kutokufanya kazi vizuri, kumbi za mikutano kuvuja, mifumo ya
tehama na viyoyozi kutokufanya kazi vizuri na baadhi ya vyumba vya semina kutokuwa na vifaa vya kazi kwa vitendo kama vile vizimba vya kujifunzia. Hali hii ina athari kwenye mfumo mzima wa uendeshaji wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo LST.

USHAURI WA KAMATI

Kamati inaona kuwa ni wajibu wa Taasisi kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi ili muda mwingi wautumie kwa masomo na si kutafakari kuhusu wapi wapate chakula na wapi wapate malazi.

Kamati inashauri kuwa, Taasisi itumie utaratibu wa PPP na mwingine itakaoona unafaa kujenga mgahawa mkubwa katika eneo la chuo na kushawishi Sekta binafsi kujenga ndani ya Taasisi au jirani na Taasisi hosteli kwa wanafunzi wanaotoka njeya Dar es Salaam huku kipaumbele kikiwekwa kwa walemavu na watoto wa kike.

Aidha, kuhusu ukarabati wa miundombinu, Kamati inampongeza Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro kwa kuanzisha mchakato ndani ya Serikali wa kuipatia LST Voti yake,hatua ambayo itaiongezea Taasisi uwezo wa kifedha, pamoja na mambo mengine, kuifanyia matengenezo miundombinu yake.

Kamati inamtakia Mhe. Waziri kila la kheri katika azma hiyo kwani hali ya Taasisi kifedha si nzuri. Taasisi haina bajeti ya maendeleo na sehemu kubwa ya mafunzo kwa vitendo huendeshwa na wakufunzi toka nje ya taasisi ambao kwa sasa wamefikia takribani 84. Wakufunzi wa ndani wako 15 tu.

4. Kamati ilibaini kutokuwepo kwa Mahakama ya kufundishia kwa vitendo ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa kushuhudia wenyewe mashauri yanavyoendeshwa mahakamani, nyaraka zinazotegemewa na weledi katika kujenga hoja na utetezi.

Kamati ilibaini zaidi kuwa, Mahakama iliyojengwa katika Taasisi kama sehemu ya miundombinu ya kuendeshea mafunzo kwa vitendo bado inaendelea kutumiwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo haina mchango wowote katika mafunzo ya uanasheria kwa vitendo kutokana na unyeti wa mashauri
yanayoendeshwa hapo ambayo kiusalama hayaruhusu watu wengi pamoja na wanafunzi kusogelea karibu.

USHAURI WA KAMATI

Kamati ina taarifa kwamba, uwepo wa Divisheni ya Mahakama Kuu ndani ya Taasisi, ulitokana na makubaliano ya pamoja kati ya Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Katiba na Sheria kipindi ambacho Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitakiwa ianze kazi lakini ikiwa haijatengewa eneo au mahali penye usalama wa kutosha kuweza kuendeshea shughuli zake.

Hivyo, ikaamuliwa Mahakama hiyo ianze kazi ndani ya eneo la Taasisi kwa muda na baadaye iipishe Mahakama ya Wilaya ambayo itatumika kikamilifu katika kuendeshea mafunzo kwa vitendo na kuruhusu mfumo wa kielektroniki unaounganisha Mahakama na madarasa kuanza kufanya kazi na kuwezesha wanafunzi kushuhudia mienendo ya mashauri wakiwa madarasani.

Hivyo, Kamati inatoa rai kwa Wizara na Mahakama ya Tanzania kuitafutia Divisheni hiyo ya Mahakama Kuu mapema
iwezekanavyo sehemu nyingine ili kuruhusu, kwa ushirikiano na Mahakama ya Tanzania kuanzishwa kwa Mahakama ya Wilaya itakayotumika kikamilifu katika kuimarisha mafunzo ya uanasheria kwa vitendo LST.

5. Kamati ililalamikiwa na wanafunzi kuwa LST kwa mujibu wa Kanuni za rufaa za Taasisi zilizochapishwa katika GN. 172 ya mwaka 2011 inatoa fursa kwa wanafunzi kukata rufaa ndani ya siku 14 tangu kutangazwa kwa matokeo endapo hawakubaliani na matokeo ya mitihani waliyofanya kwa sababu ya uonevu katika usahishaji namakosa katika kujumlisha alama za ufaulu.

Lakini wanafunzi wanadai kuwa fursa hiyo, siyo fursa chanya ila ni kiini macho kwasabu kubwa mbili: mosi, mwanafunzi anaruhusiwa kukata rufaa bila kuona karatasi yake ya mtihani ilivyosahihishwa au bila kuelezwa na
msahihishaji swali gani alishindwa kulijibu vizuri.

Pili, mwanafunzi anaruhusiwa kukata rufaa akilalamikia ukokotoaji wa alama za ufaulu bila kuona karatasi yake ya mtihani ilivyosahihishwa.

Kanuni tajwa zimebainisha muda wa kukata rufaa, lakini hazijabainisha muda ambao rufaa hiyo itashughulikiwa na namna matokeo ya rufaa yatakavyomfikia mlalamikaji.

Aidha, wanafunzi walilalamikia utaratibu wa LST kukaa na mitihani iliyokwishwa fanyika kwa zaidi ya miezi saba bila kutoa majibu kwa wanafunzi.

Hali hiyo inawafanya wanafunzi wasijue udhahifu na ubora wao na namna ya kujipanga. Vilevile, wanafunzi walilalamikia mfumo wa utoaji wa matokeo kielektoniki kuwa unatoa matokeo yenye mkanganyiko.

Mathalani, kubadilika badilika kwa alama za ufaulu na kusababisha taharuki kwa watahiniwa. Pia, Kamati ilipokea malalamiko kuhusu kuwepo kwa mgongano wa kiutendaji ndani ya Bodi ya Uendeshaji wa Taasisi katika
kushughulikia rufaa za wanafunzi.

Bodi hiyo inathibitisha matokeo ya mitihani na majibu ya rufaa kutoka kwenye Kamati ya mafunzo na Mitihani, na wakati huo huo Bodi hiyo inafanya kazi kama chombo cha mwisho cha maamuzi ya rufaa.

USHAURI WA KAMATI

Kamati imeuona msingi wa hoja wa malalamiko ya wanafunzi kuhusu mchakato wa rufaa dhidi ya matokeo ya mitihani yanayolalamikiwa, kwamba utaratibu haujakaa vizuri kwani haumpi haki mlalamikaji kujua kwa uhakika msingi wa malalamiko yake.

Vilevile, Kanuni za Rufaa tajwa haziilazimu Taasisi kushughulikia rufaa na kutoa majibu kwa mwanafunzi katika kipindi mahsusi.

Kuhusu chombo kimoja ambacho ni Bodi ya Taasisi kuidhinisha taarifa za rufaa na wakati huohuo kuwa chombo cha mwisho cha rufaa, Kamati nayo inauona mkwamo bayana wa uwajibikaji hapo.

Hivyo, Kamati inashauri kuwa, Kanuni tajwa zifanyiwe marekebisho ili mosi, ziweke sharti litakalomtaka mkufunzi wa somo ambalo mwanafunzi ameshindwa kuainisha maswali ambayo mlalamikaji alishindwa na alama alizopata.

Pili, Kanuni ziainishe muda mahsusi wa kushughulikia rufaa na kutoa matokeo kwa mlalamikaji. Kanuni hizo ziweke sharti kuwa matokeo ya mitihani yakitangazwa, michakato yote ikiwa ni pamoja na rufaa za mitihani iwe imekamilika.

Kuhusu Taasisi kukaa na mitihani muda mrefu kabla ya kusahihishwa, Kamati haijaridhishwa na sababu za Taasisi
kukaa na mitihani ya wanafunzi kwa zaidi ya miezi saba mithili ya fedha kwenye benki. Hali hii inawanyima fursa wanafunzi kujua matokeo yao mapema na kubaini udhaifu na uhodari wao.

Aidha, kutokana na mlundikano mkubwa wa karatasi za mitihani, ambapo takribani vijitabu 15,192 husahihishwa pamoja kwa siku 14 tu tena baada ya miezi kadhaa kupita, kunaruhusu makosa mengi ya kibinadamu upande wa wasahihishaji kutokea na kuathiri matokeo ya wanafunzi.

Kamati inashauri kuwa Taasisi iondokane na utaratibu huo usio na tija na usio wa kawaida katika Taasisi za kitaaluma na kuhakikisha watahiniwa wanapata matokeo ya mitihani wanayofanya mapema iwezekanavyo. Kamati vilevile inaishauri Taasisi, kuimarisha mifumo yake ya TEHAMA haraka iwezekanavyo, ili kuondokana na matatizo ya mkanganyiko wa matokeo kielektroniki.

Mkanganyiko huo umechangia kuwepo kwa hisia hasi za kuonewa kwa upande wa wanafunzi.Ili kuondoa mgongano wa kimajukumu na kiuwajibikaji katika kushughulikia rufaa za wanafunzi wasioridhika na matokeo,
Kanuni za rufaa zifanyiwe marekebisho kwa kuondoa jukumu la Bodi ya Taasisi kuidhinisha taarifa ya rufaa iliyowasilishwa na wakati huo huo kuwa chombo cha rufaa kwa mwanafunzi ambaye hajaridhika.

Aidha, Bodi isiidhinishe matokeo ya mitihani kabla ya mchakato wa rufaa kukamilika. Mabadiliko hayo ya kikanuni yafanyike mapema ili kurejesha imani ya wanafunzi kwenye mfumo wa utahini na matokeo wa Taasisi.

6. Kamati vilevile ililalamikiwa kuwa, Taasisi inatumia muda mrefu kwa masuala ya nadharia ambayo yalipaswa kufundishwa vyuo vikuu na masuala hayo yanajitokeza kwenye mitihani ya Taasisi kupima uwezo wa wanafunzi wa Mafunzo ya uanasheria kwa vitendo.

Taasisi inajitetea kuwa, nadharia siyo kipaumbele katika mtaala wake ila wakufunzi wanalazimika mara nyingine kurejea kwa muda kwenye nadharia ili madarasa yao yasikatike kutokana na uelewa wa sheria unaopishana sana miongoni mwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali.

Pamoja na utetezi huo, Kamati inasisitiza kuwa madhumuni ya kuanzishwa Taasisi hii, lazima daima yazingatiwe. Mafunzo uwandani na mengine ya vitendo kupitia mahakama za mafunzo (moot courts),kesi za kugeza (mock trials) na maigizo ya uhalisia (simulations) havina budi kutawala kwenye mtaala wa Taasisi, kwenye shughuli za kila siku na kwenye mitihani.Aidha, Taasisi inaungana na wadau wengine wa sheria kulalamikia:

(a) Uhuria usio na tija wa kila chuo kuwa na uhuru wa kupanga muda wa kukamilisha shahada ya sheria kati ya miaka mitatu (03) au minne (04) pamoja na ushahidi wa kutosha wa kushuka kwa kiwango cha elimu mashuleni na vyuoni na ushahidi wa Taasisi kuhusu viwango tofauti vya uelewa wa elimu kwa wahitimu wa sheria;

(b) Udahili wa wanafunzi wengi kupita uwezo katika vyuo vinavyofundisha sheria na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, kunasababisha uwiano mbaya kati ya waalimu/wakufunzi na wanafunzi na hivyo kuathiri ufundishaji na usimamiaji wa masomo/mafunzo;

(c) Uhuria wa kila mhitimu wa sheria kujiona ana haki kupokewa na Taasisi ya mafunzo ya elimu ya uanasheria kwa vitendo na hivyo kuiweka Taasisi kwenye wakati mgumu kuwazuia baadhi ya waombaji;

(d) Uwezo mdogo wa wanafunzi wengi wanaoruhusiwa kusoma sheria na baadae kujiunga na Taasisi katika kumudu lugha ya kufundishia ya Kiingereza. Tatizo hili lina athari kubwa sana katika uelewa wa masomo na kujieleza;

(e) Uamuzi wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kushusha vigezo vya ufaulu katika mitihani ya kidato cha sita kutoka alama 8 (B mbili kwa masomo mawili) hadi alama 4 (D mbili kwa masomo mawili) ambako kumewezesha vijana wasio na uwezo kabisa wa kumudu kusoma masomo ya sheria kudahiliwa;

(f) Kipengele cha sheria kilichowekwa kwenye Sheria ya kuanzishwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo ya mwaka 2007 kwamba, bila kupitia LST kwa mafunzo ya vitendo, mtu hana sifa ya kuwa wakili au kuajiriwa katika
utumishi wa umma. Kifungu hicho cha 12 (3) cha sheria tajwa, kimesababisha mafuriko makubwa LST kwa wahitimu wa sheria hata wale ambao hawana mpango kabisa kuingia mahakamani kufanya kazi za uwakili;

(g) Mtaala wa Taifa wa Elimu ya Sheria wa mwaka 2010 kukaa miaka mingi bila kuhuishwa na hivyo kutoendana na wakati, na

(h) Vyuo vingi vya sheria nchini, kutozingatia masharti ya uwiano kati ya waalimu na wanafunzi, sifa za waalimu na idadi yao na piramidi ya elimu.

USHAURI WA KAMATI

Kamati imeziainisha changamoto zote nane nilizozitaja, kuwa za Kimfumo na Kisera na hivyo utatuzi wake hauna budi kuwa wa kimfumo na kisera kama ifuatavyo:

Mfumo na ubora wa elimu ya sheria nchini na ule wa uanasheria kwa vitendo unasimamiwa kisheria na Baraza la Elimu ya Sheria (CLE) nchini.

Kifungu cha 5B cha Sheria ya Mawakili Sura ya 341 kinalipa Baraza mamlaka ya kusimamia na kuishauri Serikali kuhusu elimu na taaluma ya sheria nchini.

Hivyo basi, changamoto zote nilizoziainisha kuhusu muda wa shahada ya sheria, udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya sheria, vigezo vya udahili vyuoni na kwenye taasisi, viwango vya chini vya kudahiliwa vyuo vikuu (Minimum qualifications), hatua za kuimarisha uelewa wa lugha ya Kiingereza kwa wanaotaka kusoma sheria, kumaliza utata uliojitokeza wa kumtaka kila mhitimu wa shahada ya sheria apitie LST, Mtaala wa Taifa wa Elimu ya Sheria na Mtaala wa Elimu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo kuhuishwa na kusimamia sharti la uwiano wa waalimu
na wanafunzi kwenye vyuo vikuu na kwenye Taasisi,

CHANGAMOTO ZOTE HIZI ZINAYO MAMLAKA YAKE MAHSUSI YA KUZITATUA, NAYO NI C.L.E.

Hata hivyo, chombo hiki kikongwe cha kitaaluma ambacho kilianzishwa rasmi na sheria ya Bunge mwaka 1963, mpaka leo hakina Sekretariet yake, Ofisi wala Bajeti.

Matokeo yake ni kuibuka kwa changamoto zote nilizoziainisha, kwani Baraza ambalo linapaswa kuwa kitovu cha uratibu wa elimu na weledi katika tasnia ya sheria bado halijawezeshwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria kikamilifu.

Hivyo, Kamati inashauri kwamba wakati sasa umefika kwa Serikali kuliundia Baraza la Elimu ya Sheria nchini Sekretarieti yake, ofisi zake na kuipa bajeti yake na hivyo kuliwezesha kutekeleza majukumu yake yote yaliyoainishwa kisheria na hili halina budi kukamilika mapema iwezekanavyo ili Baraza liweze kutekeleza yafuatayo:

(a) Kukaa chini na TCU kupandisha vigezo vya ufaulu wa mitihani ya kidato cha Sita na Nne kwa watakaotaka kusoma sheria vyuo vikuu. (Kwa kidato cha nne msisitizo uwe angalau ufaulu wa masomo manne ikiwemo Kiingereza na Kiswahili),

(b) Kukaa chini na vyuo mbalimbali ili kuhakikisha somo la Stadi za lugha (communication skills) linakuwa sehemu muhimu ya masomo ya shahada ya kwanza ya sheria.

(c) Kuanzisha mtihani maalumu wa kuingilia LST (Pre-Entry Examination, kama ilivyo kwa wenzetu Afrika Mashariki) ambao utasimamiwa na CLE.

(d) Kupokea maombi ya kuingia LST kwa wahitimu wale tu ambao baada ya kumaliza shahada ya kwanza ya sheria, waliamua kujiunga na kampuni za mawakili na kazi zozote za kimahakama kupata uzoefu wa kisheria si chini ya kipindi cha mwaka mmoja.

(e) kuhuisha mtaala wa Taifa wa Elimu ya Sheria na wa Elimu ya Sheria kwa Vitendo kuendana na wakati,
(f) Kuhakikisha sharti la uwiano wa waalimu/wakufunzi na wanafunzi linazingatiwa na vyuo husika na Taasisi,
(g) Kuhakikisha vyuo vyote vya sheria, vina ikama stahili iliyopitishwa na CLE kwa kuzingatia pyramid ya elimu.
(h) Kuhakikisha kuwa, vyuo vyote vya sheria nchini vinatoa shahada ya kwanza ya sheria kwa kipindi cha miaka minne na,
(i) Kukaa chini na Shule za Sheria, Vitivo pamoja na Taasisi kukubaliana kuhusu masomo ya msingi ya kufundishwa
katika mwaka wa nne wa shahada ya kwanza ya sheria.

7. Kamati imebaini kwamba, hakukuwa na utayari kutokea mwanzoni kuipa CLE mamlaka kamili ya kusimamia tasnia ya sheria nchini, hasa kwa kuzingatia kwamba toka mwaka 1963 CLE halikuwahi kuwezeshwa ili ifanye kazi kama mabaraza mengine ya kitaaluma.

Uongozi wa CLE wenyewe ambao unahusisha viongozi wa juu katika tasnia ya sheria yaani, Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanashiriki katika shughuli za CLE kupitia kwa wawakilishi. Hii ni ishara tosha ya udhaifu wa CLE.

USHAURI WA KAMATI

Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali washiriki wao wenyewe kwenye vikao vya CLE. Hivyo, Kamati inatoa rai kwa Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Mawakili, Sura ya 341 ili kuondoa kipengele cha Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushiriki kwa uwakilishi. Hawa ndiyo nguzo kuu ya sheria nchini.

Kamati inashauri vile vile kuwa, juhudi za kuifufua CLE ziendane na utungaji wa sheria mahsusi kuhusu CLE ambayo itaainisha mambo muhimu, pamoja na mengine, yafuatayo:

(a) Utu wa kisheria wa Baraza (Legal personality of the Council) ili baraza liweze kukopa, kukopesheka, kushitaki, kushtakiwa, kumiliki mali kwa jina lake nk.

(b) Kuwa na mamlaka ya kusimamisha ufundishaji wa sheria kwenye chuo chochote ambacho hakizingatii masharti ya uendeshaji wa kozi ya sheria.

(c) Kutunga kanuni zitakazosimamia uendeshaji wa elimu ya sheria nchini nk.
(d) Marekebisho yafanyike katika kifungu cha 12 (3) cha Sheria ya LST, Sura 425 ili kuondoa sharti linalodhaniwa kuwa linamtaka kila mhitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kujiunga na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo ili kupata sifa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma kufanya kazi ya kisheria.

Kamati inashauri vilevile kuwa badala ya kurekebisha sheria ambayo vifungu vyake vya 2 na 12 vikisomwa kwa pamoja vinaeleweka kwa urahisi na wanasheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atoe ufafanuzi wa tafsiri sahihi ya vifungu husika, ambao utafuatwa na Taasisi zote za serikali na binafsi.

Huu kwa muhtasari, ndio ushauri tuliokuletea Mhe.Waziri.

Naomba kuwasilisha.
-----

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news