KESHO MKUMBATIANE:Ona yale yote hasi,Ramos na Messi sasa wa pamoja huko

NA LWAGA MWANBANDE

HAKIKA soka si uadui wala uhasama, soka ni burudani na ajira,licha ya Sergio Ramos na Lionel Messi kwa miaka mingi kuwa wapinzani, tumeshuhudia siku za karibuni wawili hao wakitekeleza majukumu yao ndani ya Klabu ya Paris Saint-Germain.
Tuliona beki huyo wa zamani wa Real Madrid akimkaribisha mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona katika mji mkuu wa Ufaransa wa Paris, kwa ajili ya kuanza majukumu yake na mwajiri mpya.

Wakati wengi wetu tukijiaminisha kuwa, miongoni mwao kuna mwenye uadui, hivyo kujenga uhusiano mbaya, majibu yametolewa na Sergio Ramos kuwa yeye na Lionel Messi hakuna ubaya.

Ramos akimzungumzia Messi anasema, "Ni mchezaji mzuri na ni bahati kuwa naye kama mchezaji mwenza. Tumeteseka naye kwa miaka mingi.

"Anaendelea kufanya vyema katika kiwango cha juu. Bado ni mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani. Ni bora kuwa naye kama mwenza kuliko kuwa mpinzani. Lakini mwishowe sisi ni wachezaji ambao tuna malengo sawa, ambayo ni kushinda na kuifanya timu ya Paris Saint-Germain kuwa bora"...Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasema,adui yako wa leo, kesho ni rafiki yako, endelea;

1:Adui yako wa leo, kesho ni rafiki yako,
Leo chapa na fyekeo, kesho mcheza mwenzako,
Kesho kuiona leo, hiyo ni bahati yako,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

2:Yeye hapo mwajiriwa, kazi yake siyo yako,
Nawe pia mwajiriwa, ujuzi wake ni wako,
Kesho mnahitajiwa, mwajiri wake ni wako,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

3:Kama mnanuniana, kufanyiana vituko,
Hata kama mwaonana, kwenu hakuna kicheko,
Kama mnapoteana, kuwa pamoja hakuko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

4:Ona Ramos na Messi, livyopigana viwiko,
Kila mara kwao kesi, kukanyagana ugoko,
Ona yale yote hasi, sasa wa pamoja huko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

5:Dunia yetu duara, makazi huku na huko,
Hivyo binadamu bora, sifanyiane vituko,
Kukwaruzana hasara, mtapokutana huko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

6:Ni akiba ya maneno, wasema wahenga huko,
Yasiyoleta miguno, kati ya kwake na yako,
Ili kesho iwe nono, mnapokutana huko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

7:Mifano ni kedekede, ipo hapa hata huko,
Waliowaona swide, kwa magumu matamko,
Sasa wanacheza rede, na tena wana mshiko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

8:Sasa wanaogopana, kwenye ulingo hawako,
Sababu walijiona, watabaki hukohuko,
Sasa wameshaloana, baada ya tetemeko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

9:Dunia inazunguka, iko hapa iko huko,
Na wewe unazunguka, hubaki huko uliko,
Usingizini amka, na watu fanya kicheko,
Mchukie kwa kiasi, kesho mkumbatiane.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments