Ligi Kuu ya NBC yazidi kuwa moto

NA DIRAMAKINI

MBEYA City wametoa sare ya kufungana bao 1-1 na Simba SC ya jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi ya NBC Tanzania Bara.

Wenyeji hao waliwakaribisha Wekundu wa Msimbazi Novemba 23, 2022 katika dimba la Sokoine lililopo jijini Mbeya.

Simba SC walitangulia kwa bao la kiungo Muzamil Yassin dakika ya 15, kabla ya Tariq Seif kuisawazishia Mbeya City dakika ya 79.

Kwa matokeo hayo, Simba inafikisha alama 28 katika mchezo wa 13, ingawa inabaki nafasi ya tatu, ikizidiwa alama moja moja na zote, Yanga iliyocheza mechi 11 na Azam FC mechi 13.

Wakati huo huo, bao pekee la mshambuliaji Meddie Kagere dakika ya 40 limetosha kuipa Singida Big Stars ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC.

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao wenyeji hao wamewakaribisha wana Kinondoni katika dimba la LITI lililopo mkoani Singida.

Kwa ushindi huo, Singida Big Stars inafikisha alama 21 katika mchezo wa 12 na kusogea nafasi ya nne, wakati KMC inabaki na alama zake 14 za mechi 13 katika nafasi ya 10.

Novemba 22, 2022 katika mwendelezo wa michuano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Fiston Kalala Mayele dakika ya 42 na 67 aliipa Yanga SC ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Dodoma Jiji FC.

Ni kupitia mtanage ambao uliwakutanisha miamba hao wa soka mmoja kutoka jijini Dar es Salaam na mwingine kutoka Jijini Dodoma katika dimba la LITI mkoani Singida.

Mayele alifunga bao la kwanza akimalizia krosi ya Tuisila Kisinda kutoka upande wa kulia na la pili akimalizia pasi ya winga chipukizi, Dennis Nkane.

Kwa sasa, Mayele anafikisha mabao nane na kupanda kileleni kwenye chati ya ufungaji kwa bao moja zaidi ya Sixtus Sabilo wa Mbeya City.

Aidha,Novemba 21, 2022 Mtibwa Sugar waliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanage ambao ulipigwa katika dimba la Manungu Complex huko Turiani mkoani Morogoro ambapo mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa na Ismail Mhesa dakika ya 45 na Onesmo Mayaya dakika ya 48, wakati la Polisi lilifungwa Ambroce Awio dakika ya 35.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news