WAMESAFISHA UWANJA:Kipindi chatufundisha, hili Kombe la Dunia

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 23,2022 katika Uwanja wa Taifa Qatar (Khalifa International Stadium) mashabiki wa timu ya Taifa ya Japan waliuonesha ulimwengu kuwa,ushabiki wao si kwa ajili ya kujinufaisha pekee tu bali pia kuhakikisha mazingira yanayowazunguka na wanayoyatumia kushiriki michezo yanakuwa safi na salama.

Ni katika mwendelezo wa michuano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) inayoendelea nchini Qatar.

Katika uwanja huo,baada ya Japan kuwakung'uta Ujerumani mabao 2-1, mashabiki walitumia muda wao kufanya usafi ikiwa ni hatua moja wapo muhimu ya kuhakikisha hakuna vifungashio vya chakula, vitambaa, vikombe vitupu vya vinywaji, vinavyoachwa baada ya watu kuvitekeleza uwanjani.

Pia Wajapan walifanya vivyo hivyo kwenye Kombe la Dunia nchini Urusi miaka minne iliyopita zikiwemo mechi nyingine zilizofuata. Huko Japan, usafi ni sehemu ya utamaduni wao kuanzia utotoni na huwa wanajisikia fahari sana kutekeleza jukumu hilo muhimu katika maisha yao ya kila siku.

Hilo lilikuwa ni moja wapo ya matukio ya kuvutia zaidi Duniani na somo kubwa kwa jamii, ikizingatiwa kuwa, Dunia kwa sasa inapambana kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama ili kuhakikisha jamii inayashinda magonjwa ya milipuko.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, hiki ni kipindi cha kutufundisha, kwani hadi siku 28 za kombe la Dunia kutamatika huko nchini Qatar, wenye macho na masikio watajifunza mengi yaliyo mema kwa ustawi bora wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla, endelea;


1.Hadi litakapokwisha, hili Kombe la Dunia,
Takuwa tumejilisha, elimu ya kusalia,
Imani kuimarisha, na mengi ya kutumia,
Walivyopata ushindi, wamesafisha uwanja.

2.Qatar walishatukosha, Imani kushikilia,
Ushoga kuupindisha, kwao usije ingia,
Waliowajaribisha, nao liwafanyizia,
Walivyopata ushindi, wamesafisha uwanja.

3.FIFA wakafurahisha, msuli kutunishia,
Ya Ulaya wakabisha, ya Qatar kukumbatia,
Hii yatuelimisha, ya kwetu kujikingia,
Walivyopata ushindi, wamesafisha uwanja.

4.Lingine la kushtusha, la Saudi Arabia,
Kina Messi mewashusha, pua wakaangukia,
Siku wameadhimisha, kwao jipumzikia,
Walivyopata ushindi, wamesafisha uwanja.

5.La Wajapani komesha, lile wametufanyia,
Jerumani kuwawasha, wakaondoka walia,
Shangwe kuzikamilisha, uwanja wakafagia,
Walivyopata ushindi, wamesafisha uwanja.

6.Hili linatufundisha, mazingira jilindia,
Uchafu kuharamisha, mpirani kiingia,
Vitu tunarusharusha, bora kujisafishia,
Walivyopata ushindi, uwanja wamesafisha.

7.Uwanja wameshafisha, taka mbali fagilia,
Kwa kweli watufundisha, vizuri igilizia,
Ni shangwe wajizungusha, ushindi kujipatia,
Walivyopata ushindi, uwanja wamesafisha.

8.Kingine chafurahisha, vigogo wanafulia,
Argentina kuzamisha, metikisika dunia,
Mikeka walobebesha, wametoka wanalia,
Walivyopata ushindi, uwanja wamesafisha.

9.Na Ujerumani kwisha, Japan kamalizia,
Japan kufurahisha, katika kushangilia,
Makopo wamesafisha, uwanja uwe sawia,
Walivyopata ushindi, uwanja wamesafisha.

10.Kipindi chatufundisha, hili Kombe la Dunia,
Hata wiki haijesha, mengi tumejipatia,
Kesho yaweza tuvusha, yetu tuimarishia,
Walivyopata ushindi, uwanja wamesafisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments