🔴LIVE:Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania, Waziri Mchengerwa afunguka

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania linalofanyika nchini na kusisitiza kuwa tamasha hilo linaimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mhe. Mchengerwa amezindua tamasha hilo leo Novemba 18, 2022 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambapo amesema, Tanzania ni nchi pekee Afrika iliyohakikisha nchi nyingine za bara hilo zinakua huru.

"Tanzania ndio nchi pekee yenye historia ya uhifadhi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, vijana wanapaswa kutambua kuwa Taifa letu lilitoa machozi, jasho na damu kuhakikisha Afrika Kusini na Mataifa mengine ya Afrika yanakua huru,"amesema Mhe.Mchengerwa.

Ameongeza kuwa,tamasha hilo litaimarisha undugu wa nchi hizo na kukuza Sekta za Utamaduni na Sanaa ikiwa ni pamoja na kutangaza Utalii, Mila na Desturi za nchi hizo, ambapo amesisitiza wadau wa sekta hizo kujitokeza kuuza na kuonesha bidhaa zao katika msimu wa Tamasha hilo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe. Samia imeendelea kuboresha sekta hizo ambazo zimeajiri vijana wengi, huku akitoa wito kwa Sekta Binafsi kuunga mkono juhudi hizo.
Aidha, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa Idara ya Utamaduni kuhakikisha inaandaa matamasha yenye sura ya kimataifa ambayo yatahusisha nchi nyingi zaidi.

Awali, Naibu Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini, Mhe. Mcawe Mafu alisema nchi yake imeleta Tamasha hilo limeletewa Tanzania kwa kuwa nchi hizo ni ndugu wa muda mrefu.

Amesema Tamasha hilo litahusisha Sanaa za maonesho, mila na desturi, ngoma za asili pamoja na Semina kuhusu historia ya nchi hizo.

Post a Comment

0 Comments