MABALOZI, VUTIA WAWEKEZAJI: Zanzibar hii ya kwetu, mitaji twahitajia

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 18, 2022 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje kujenga uhusiano wa karibu na taasisi za umma na binafsi za pande zote mbili za Jamhuri ili kuiwezesha Tanzania kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ya uwakilishi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito huo wakati akizungumza na mabalozi wa Tanzania katika mkutano wao unaondelea jijini Zanzibar.

Amesema, katika utendaji wa kila siku, ni muhimu mabalozi hao wakahakikisha vipaumbele vyao vinaendana na vile vilivyopo katika Mpango wa Serikali zote mbili na kuzingatia Dira ya Mandeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050; Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Mwaka 2021-2026 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pia Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, viwanda, kilimo, ufugaji na uchumi wa buluu zinaendelea kuchangia uchumi wa Zanzibar, lakini pia Serikali yake imeendelea kuboresha sekta mbalimbali kwa kuondoa urasimu katika sekta ya uwekezaji na ufanyaji biashara ili kuiwezesha Zanzibar kufikia mapinduzi ya uchumi.

Ameongeza kuwa, Serikali yake ya Awamu ya Nane kwa sasa inatekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo inalenga kuhakikisha kunakuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari ili kuinua hali ya maisha ya Wazanzibari kupitia sekta za Uchumi wa Buluu ikiwemo utalii, Ujenzi wa Bandari, uvuvi na ufugaji wa samaki, ukulima wa mwani, nishati ya mafuta na gesi pamoja na biashara ya usafirishaji wa baharini.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo, klichobakia ni mabalozi kuwajibika, endelea;

1.Ni miaka miwili tu, sisi tunashangalia,
Kwa jinsi Rais wetu, anavyotutumikia,
Anafanya mambo kwatu, Zanzibari yavutia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

2.Hussein Mwinyi ni wetu, huku twamfagilia,
Jinsi anafanya vitu, watu akiangalia,
Figisufigisu zetu, zote sasa zaishia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

3.Hata mazingira yetu, mitaji kuivutia,
Kaboresha yako kuntu, wengi wanafurahia,
Kitaka wekeza kwetu, fasta twahudumia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

4.Wataka vibali kwetu, mtaji kutushushia,
Kuzungushwa huku kwetu, kwa kweli kumefifia,
Siku moja huko kwetu, kibali wajipatia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

5.Siasa za huku kwetu, vitu tunafwatilia,
Kusifiasifia tu, huwezi ukasikia,
Kwa sababu vitu kutu, sote tunavichukia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

6.Zanzibar hii ya kwetu, mitaji twahitajia,
Watu wawekeze kwetu, na mali kujichumia,
Na serikali yetu, kodi itajipatia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

7.Kingine kizuri kwetu, mitaji ikitujia,
Ajira kwa watu wetu, nyingi watajipatia,
Kwa hiyo uchumi wetu, juu utainukia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

8.Buluu uchumi wetu, kwa kweli unavutia,
Mitaji ifike kwetu, fursa zinavutia,
Chagua kama viatu, pale wanajitakia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

9.Bahari ni mali yetu, fursa zinajazia,
Utalii huku kwetu, fukwe nyingi zavutia,
Na viwanda nchi yetu, mahali tajipatia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

10.Enyi mabalozi wetu, wito mmesikia,
Toka kwa Rais wetu, wenyewe kawaambia,
Ilete furaha kwetu, kwa kazi kutufanyia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

11.Mwinyi Rais wa watu, heri tunakutakia,
Fika miaka mitatu, mengi tukifurahia,
Na mitano iwe kwatu, kiti ukikikalia,
Kazi kwenu mabalozi, vutia wawekezaji.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news