MAKOSA MAWILI YA DKT.BASHIRU ALLY KAKURWA

NA ADELADIUS MAKWEGA

NOVEMBA 28, 2022 nilikuwa nafanya kazi moja ya kurekebisha baadhi ya masahihisho ya riwaya yangu moja niliyokuwa naiandika, nilipomaliza kazi hiyo nilipaswa kuitengenezea jedwali la yaliyomo, nikafanya baadhi ya hatua lakini nikawa nimesahau namna ya kutenganisha namba ya Kirumi i,ii, iii, iii,iv…za kurasa za mwanzo ikiwamo dibaji na kurasa za sura za kitabu hicho ambazo zilikuwa namba ya Kiarabu 1,2,3,4…

Mwanakwetu nilikuwa nimesahau kabisa maana mara ya mwisho nilifanya kazi hiyo mwaka 2008 nikiwa mwanafunzi wa shahada ya uzamili.

Mtu na majirani zake, nikatoka hapo hadi kwa jirani, nikaomba msaada huo kwa watu kadhaa, nikamkosa mtu mwenye ujuzi huo, nikiwa nimekata tamaa nikakutana mama mmoja mgeni hapo nilipokuwapo, akanielekeza vizuri sana na mimi kukumbuka hatua zote na kweli kazi yangu ilikamilika.

Mara baada ya kumaliza kazi hiyo tu akaja ndugu mmoja akanisalimu, nikamuuliza vipi Songwe mmemchagua nani kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo? Ndugu huyu akamtaja jina jamaa huyu na kuitaja idara aliyokuwa akiifanyia kazi.

Nikamuuliza Mkola mmemnyima? Ndugu huyu akanijibu kuwa Mkola ni miongoni mwa majina kadhaa ambayo hayakurudishwa.

Kwa kuwa ndugu huyu ni mwana CCM mzuri, ninamfahamu muda mrefu na ni kijana mkweli sana, japokuwa huo ukweli wake huwa unamletea shida kidogo.

Nikamuuliza je? Mna uhakika huyo Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Songwe anaweza kuhimili siasa za mkoa huo?.

“Huyu jamaa anaweza, tunamuamini na hata taasisi aliyokuwa anaifanyia kazi inatupa matumaini kuwa anaweza kuifanya kazi hiyo.” Nikamuuliza ni hayo tu? Akasema ndiyo.

Nikamwambia kwani akichagulia mtu kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, taasisi aliyekuwa anafanyia kazi anakwenda kuitumikia tena au anakwenda kuwatumikia Wanaccm wa Mkoa wenu ? Akakaa kimya ndugu huyu, nikasema kubwa akafanya kazi; kusimamia Katiba ya CCM, kusimamia maamuzi ya vikao na kusimamia ilani ya chama hicho tawala cha siasa. Kazi yake aliyokuwa anaifanya itabaki katika wasifu tu. Nikaagana na ndugu yangu huyu na kuendelea na safari yangu.

Nikatoka nikafika eneo la pili chumba kingine nikakutana na watu wengine wakawa wananitania, “Kaka naona leo umevaa shati kubwa kubwa kama puto,” Nikasema ndiyo,mwingine akasema, “Kaka sijaona bango lako katika mitandao ya kijamii vipi ujachukua fomu ya uongozi wa chama chetu ?” Nikajibu Sijajaliwa kuchukua fomu hiyo.

Ndugu huyu wa pili akaniita kando akasema nami kwa kunong’ona,“Kaka mbona Dkt. Bashiru Ally anazingua? Wakati mama anaupigwa mwingi kweli kweli?”.

Nikamjibu huyu ndugu yangu nikisema kweli Dkt.Bashiru Ally ana makosa, kwa leo ngoja nikwambie makosa mawili tu.

Ndugu yangu huyu akiwa amekaa katika kiti chake akaacha kuandika katika kompyuta yake huku mimi nimesimama akawa ananisikiliza,

La kwanza kabisa Dkt. Bashiru Ally hulka yake siyo mvivu kuongea, sasa kwanini alikaa kimya muda mrefu? Dkt. Bashiru Ally ninayemfahamu mimi, akipigiwa simu na VOA, DW, BBC na vyombo mbalimbali vya habari anaongea na kutoa maoni yake kwa kujiamini. Kama hatoongea na wewe atakwambia,

“Nipigie simu baada ya saa moja nipo nafundisha/ nipo kikaoni.” Sasa imekuwaje akawa kimya kwa muda mrefu? Katika hali zozote hulka yako usiipoteze. Kwa kukaa kimya alifanya kosa kubwa na hapo tukawa na Dkt.Bashiru Ally wawili; Mkiya wa sasa na mwongeaji yule wa zamani.

Nikaendelea kumwambia ndugu huyu huku akinitazama kwa umakini mkubwa, kosa la pii la Dkt Bashiru Ally pahala alipoongelea hoja zake, huyo aliyemteua kampeleka Bungeni na anafahamu fika kwamba huyu ndugu akienda huko ataongea hoja hizi nzinto nzinto na zilipaswa kusikika Bungeni na Wabunge wengine tungeona maoni yao juu ya ndugu yao na maoni yao yangenukuliwa katika karatasi za Bunge.

Ndugu yangu huyu akawa ananisikiliza kwa makini mno, “Kabla ya ASP na TANU, wakati wa Sultani Jamshidi Bini Abdullah na Gavana Edward Twining watu wa Zanzibar na Tanganyika walikuwa kwanza na ajenda zao nyingi zilizokosoa utendaji wa serikali hizo , hizo ajenda ndizo zilizozaa hivyo vyama na badaye ndiyo ikazaliwa CCM.

ASP na TANU wazee wetu walikutanishwa na ajenda, bila ya ajenda mpaka sasa tungekuwa chini ya tawala zenye nasaba ya ndugu hao wawili yaani Sultani na Gavana. Viongozi wa sasa wa CCM watake wasitakewa lazima watambue kuwa chama hiki ni mtoto wa AJENDA.

Alilolisema Dkt Bashiru Ally ni juu ya wakulima wadogo wadogo akiwa na MVIWATA inayoongozwa Stephern Ruvuga. Swali la kujiuliza je ajenda hiyo ya wakulima wadogo wadogo siyo ajenda ya kudumu tangu ASP na TANU?

Cha kufanya siyo kumchukulia hatua Dkt Bashiru Ally kwani ndugu huyu anatukumbusha ajenda ya wakulima wadogo wadogo ambao ni mimi na wewe, ndiyo wenye CCM yao, ndiyo waliompigia makofi Dkt. Bashiru Ally katika mkutano ule wa MVIWATA, hii ni ajenda ya chama chetu, kwa kuwa ameshasema jukumu langu mimi na wewe tunapaswa kumkumbusha kuwa ndugu yetu huyu amekaa kimya sana hadi tunadhani tuna Dkt.Bashiru Ally wawili pia tunamuomba hayo aliyoyasema MVIWATA akalonge pia katika vikao vya Bunge.

Mwanakwetu nikiwa nimevalia shati langu kama puto nikakamilisha kilichonipeleka hapo nakurudi kwetu madongo poromoka.

makwadeldaius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news