Mama Mariam Mwinyi awaeleza mabalozi kilimo cha mwani kilivyo muhimu

NA DIRAMAKINI

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi amesema kilimo cha zao la mwani kina manufaa makubwa kwa afya na uchumi wa Wazanzibari.
Mama Mariam Mwinyi amesema hayo Ikulu ndogo Migombani, alipozungumza na Ujumbe wa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaelezea juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), sambamba na utekelezaji wa programu ya miaka mitatu ya taasisi hiyo.

Amesema, wastani wa asilimia 80 ya wakulima wa kilimo cha mwani ni wanawake, huku akibainisha malengo ya kuliongezea thamani zao hilo ili kuleta tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Mama Mariam amewafahamisha mabalozi hao changamoto mbalimbali zinazowakabili walengwa wa programu hizo kwa maana ya wanawake, vijana na watoto ikiwemo vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia pamoja na azma ya kuwapatia taulo za kike wanafunzi wa kike walioko shuleni.

Amesema, pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji, bado hali sio nzuri, akibainisha kuwepo wimbi kubwa la vitendo hivyo hapa nchini, huku tatizo hilo likichangiwa kwa kiasi kikubwa na jamii (waathirika) kutokana na aibu pamoja na muhali.

Aidha, amesema kumekuwa na juhudi za kuimarisha afya za vijana kwa kufanya mazoezi, lengo likiwa ni kuhakikisha Taifa linakuwa na wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi.
Mama Mariam alieleza kuwa, ZMBF imekuwa katika juhudi za kukabiliana na vifo vya mama na watoto kupitia Ppogramu yenye lengo la kuielimisha jamii umuhimu wa lishe bora kwa watoto.

Amesema, malengo yamelekezwa kwa watoto hususani walio chini ya umri wa miaka mitano, huku mkazo ukiwekwa katika uimarishaji wa afya ya mama kabla ya uzazi .

Naye Kiongozi wa Mabalozi hao, Asha Rose Migoro amepongeza juhudi zinazochukuliwa na taaasisi hiyo ya ZMBF na kuahidi kushirikiana an washirika wa maendeleo katika nchi wanazofanyia kazi, ili kufanikisha malengo ya taasisi.

Amesema, takribani nchi zote zenye uwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeweka vipaumbele katika ushughulikiaji wa masuala ambayo ZMBF imelenga kuyatekeleza.

Post a Comment

0 Comments