Mary Chatanda amng'oa Kabaka uenyekiti UWT,Zainabu Shomary ndiye makamu

NA DIRAMAKINI

MARY Chatanda ameibuka kidedea katika nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.

Awali wagombea waliopitishwa na Halmashauri Kuu alikuwa ni Gaudentia Kabaka ambaye alikuwa anatetea nafasi yake, Kate Kamba, Dkt.Wemael Chamshama, Mariam Lulinda na Mary Chatanda.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 28, 2022 wakati wa Mkutano Mkuu wa 10 wa UWT kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma mchuano mkali ulionekana kwa Gaudentia Kabaka, Kate Kamba na Mary Chatanda.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri Mkuu mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alimtangaza Chatanda kwa ushindi wa kura 527 huku Mwenyekiti aliyemaliza muda wake,Gaudentia Kabaka akiambulia kura 219 huku Kate Kamba akiambulia kura nane tu kati ya kura 756. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UWT imekweda kwa Zainabu Shomary.


Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kutoridhishwa na kasi ya kujiunga kwa wanachama wa UWT na uendeshaji wa miradi yake ya kiuchumi.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa uchanguzi wa UWT jijini Dodoma ambapo amesema kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 jumuiya hiyo imeingiza wanachama wapya 86,288 ambao hawaridhishi.

“Ukichukua idadi hiyo ukiigawa kwa mikoa 32 na kujua mikoa mengine ni midogo sana kama ile ya Zanzibar unapata wanachama 2,697 tu, sasa hii sio kazi nzuri sana,”amesema Mheshimiwa Samia.

Pia Mheshimiwa Samia amesema jumuiya hiyo ilikuwa na muda wa kutosha wa kuongeza wanachama wengi zaidi wakati nchi ilipokuwa haina hekaheka za kisiasa na kutumia makongamano kujitangaza.

Akizungumzia upande wa miradi ya kiuchumi, Rais Samia amesema miradi hiyo haijaipa UWT nguvu kubwa ya kiuchumi hivyo kuwa na tabia ya kushika na kuacha miradi hiyo.

Amesema miradi inayoendeshwa na Jumuiya hiyo mingi ni ya vibanda, mashine za kusaga na mingine midogo ambayo haijaipa nguvu kiuchumi UWT. “Wito wangu kwa Jumuiya ni kwenda kufanya miradi mikubwa itakayoipa Jumuiya nguvu ya kiuchumi,” amesema Samia.

Rais Samia amesema aliona wakati wa maandalizi ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi huo namna kamati mbalimbali zilifatwa kuangalia upatikanaji wa fedha.

“Baadae nikasema msisumbuke kwa hiyo chama na mimi tukatoa fedha mambo yakaenda, hii inaonesha kuwa miradi tuliyonayo bado haijawa miradi ya kutupa nguvu ya kiuchumi kwenye Jumuiya,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news