Mashabiki Yanga SC wafungiwa miezi mitatu kwa kuwavamia waamuzi

NA DIRAMAKINI

MASHABIKI na wanachama wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Israel Suma, Kais Mwasongwe, Soud 'Tall' na Mohamed Mposo wamefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kuwavamia waamuzi wa mchezo kati ya klabu hiyo na Simba SC.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 8, 2022 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Adhabu hiyo imetolewa, baada ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligii Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Novemba 4, 2022 kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi na kufanya maamuzi.

Imeelezwa kuwa, katika mechi Namba 64 ambayo iliwakutanisha Yanga SC na Simba SC katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Oktoba 23, 2022 mashabiki na wanachama hao walifanya tukio hilo, wakiwa wanaelekea chumbani wakati wa mapumziko, kabla walinzi wa uwanjani (stewards) hawajaingilia kati na kuwaondoa.

"Mashabiki na wanachama hao ambao wanatumia na Klabu ya Young Africans kama maafisa wasaidizi wa usalama, walionekana kupitia picha jongeo (video) zilizonaswa na kamera uwanja wa Benjamin Mkapa,wakifanya kitendo hicho wakiwa katika njia ya kuelekea vyumba vya kuvalia,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news