MAZITO KUHIMILIKA: Pole kwa wahusika wote

NA MWANDISHI WETU

LEO Novemba 6, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa leo amewasili mkoani Kagera kushuhudia zoezi la uokoaji linaloendelea kufuatia ndege ya Precision Air kupata ajali ilipokuwa ikikaribia kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Pia Mheshimiwa Majaliwa amewajulia hali wahanga wa ajali hiyo, wanaopata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.

Akizungumza katika eneo hilo, Waziri Mkuu amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa wote walioguswa na ajali hilo na kwamba Serikali itaendelea kutoa huduma stahiki kwa majeruhi wote.

Waziri Mkuu amewataka wananchi wawe na subira katika kipindi hiki ambacho Serikali itafanya uchunguzi kupitia vyombo vyake ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, subira yavuta heri huku akitoa pole kwa wahusika wote, endelea;


1. Ni moshi wapeperuka,
Maisha yavo katika,
Marefu yanafupika,
Ndiyo hivyo twaondoka.

2. Vigumu sahaulika,
Yetu yaliyotendeka,
Maisha yanaandika,
Mambo yanayosomeka.

3. Kifo tusingekitaka,
Huzuni navyotufika,
Ni hakuna kukwepeka,
Hivyo hivyo chatufika.

4. Ni bora kupumzika,
Mateso kumalizika,
Ila kinavyotufika,
Kifo tunahamanika.

5. Tuzidi kuimarika,
Rabuka tukimshika,
Kufanya ya kupendeka,
Ili tujefarijika.

6. Yale yasahaulika,
Kwetu sisi kuyashika,
Roho wake mtukuka,
Atufanye kukumbuka.

7. Tuache kuzubaika,
Hata miili kuchoka,
Kufanya yasotakika,
Kikwetu yale sulika.

8. Tusikilize Rabuka,
Machozi yamiminika,
Jinsi tumetetereka,
Nguvu mwili kuvunjika.

9. Pole wote wahusika,
Taifa lasikitika,
Dunia imeshituka,
Hatari ilotufika.

10. Na waliosalimika,
Pona na kuimarika,
Nyumbani muweze fika,
Na ibada kufanyika.

11. Haya yanapotufika,
Ni vema tukakumbuka,
Kwetu hatujakufika,
Tu njiani twatabika.

12. Tutakuja pumzika,
Mwisho utakapofika,
Tuungane na Rabuka,
Kama vile alisema.

13. Mazito kuhimilika,
Ila ndiyo yamefika,
Wala tusingeyataka,
Ndiyo hivyo yamefika.

14. Mioyo imeshtuka,
Kwahapa tulipofika,
Mungu wetu mtukuka,
Na hali yetu husika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
6/11/2022

Post a Comment

0 Comments