MWANAFUNZI MWENYE MWANDIKO MZURI

NA ADELADIUS MAKWEGA

SHULE ya Msingi Mtoni Kijichi ni shule iliyopo jirani sana na Bahari ya Hindi-Dar es Salaam huku kwa miaka mingi ikipokea wanafunzi kutoka Mtoni Kijichi na eneo kubwa la Mbagala, wanafunzi wengi waliokosa nafasi shule za Mbagala , Mtoni, Vijibweni na Kurasini waliweza kusoma huko japokuwa ilikuwa ni safari ndefu sana kwa mguu na hata ngalawa.

Wenyeji wa asili wa Mtoni Kijichi tangu enzi ni Wandengereko na Wamakonde wakijishugulisha na uvuvi kidogo na kilimo cha kawaida.

Wanafunzi waliokuwa wanatoka Mbagala walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika shuleni hasa hasa kwa kutumia njia ya mkato ambayo ilianzia Mbagala Sabasaba (sasa Mbagala Mpili), wanashuka Bonde la Mzee Mafko, wanapita Shamba la Maua la Kadozo (Magoa) kisha wanapita kando kando ya Mbagala Spritual Centre, kando ya mashamba ya miwa na mipunga, wanapanda mlima wa Kijichi wanafika shuleni hapo na hii ni safari ya asubuhi na alasiri kila siku Jumatatu hadi Ijumaa.

Mwaka 1986 shule hii darasa la kwanza iliwapokea watoto wawili kusoma shuleni hapo Lydia Mwambene na Mohamed Mwarami na mwaka 1990 ilimpokea mwanafunzi mmoja anayefahamika kama Bartazary Milanzi wote kutoka Mbagala Kizinga, huku tangu awali walikuwepo wanafunzi wengi wanaotoka Mbagala Kizinga kusoma Kijichi kama Martini Mkapa na Mwanakwetu.

Wanafunzi hawa wakiwa watoto walipita njia hiyo iliyohitaji hekima na ubabe muda mwingine ilikuweza kufika salama shuleni na kurudi nyumbani salama salimini.

Bartazary Millanzi (Kushiwa- sasa ni Baharia) na wenzake waliokuwa wanakaa Mbagala Misheni kuna siku walikata miwa katika shamba la mkulima mmoja na kula kwa sababu ya njaa ya darasa la kwanza maana walizoe kushinda nyumbani sasa wanatembea umbali mrefu zaidi ya saa moja njiani kwa mguu, wenye shamba wakawa wanawawinda kweli kweli.

“Kuna watoto wamekata miwa yetu hapa shambani wanasoma Mtoni Kijichi tunawatafuta, waambieni tunawasaka ama zao ama zetu,”niliambiwa Mwanakwetu.

Hawa darasa la kwanza siku iliyofuata kwa kuwa walifahamu lililotokea wakabadilisha njia na kupita njia ndefu, wakafika shuleni vizuri wakasoma, saa tano wakaruhusiwa, kurudi nyumbani, watoto hawa wakakubaliana jamani tusiondoke tutapita njia ndefu hadi lini? Tumngoje kaka tuondoke naye.

Nilipotoka darasani tukasimama mstarini tukaruhusiwa kurudi nyumbani, nikiwa naondoka nikakutana nao-Kushiwa na wenzake watatu. Nikawauliza nyie vipi?Mnatoka saa tano mpaka saa hizi mnafanya nini? Wakanijibu kuwa tulikuwa tunakungoja tuondoke sote.

Kwa bahati nzuri huyu Kushiwa familia yake yote nilikuwa naifahamu muda mrefu, nikasema twendeni, tukaanza safari hiyo ya kurudi nyumbani.

Sasa kundi likawa kubwa Mwanakwetu (VII) , Mikidadi Chite(VI), Lydia Mwambene(V), Mohamed Mwarami (V) Bartazary Millanzi (Kushiwa) na wenzake watatu (I).(Namba za Kirumi Kwenye Parandesi ni Madarasa waliyokuwa wakisoma wakati Huo).

Tukawa tunakwenda nyumbani kushoto kulia na wengine kulia kushoto njia ile ile, mara baada ya nusu saa tukafika katika mashamba ya miwa na mpunga, jamaa wakatokea wakataka kuwakamata na kuwapiga akina Kushiwa na wenzake, tukawazuia.

“Hawa wamevunja miwa yetu, lazima walipe.” Wakaulizwa miwa mingapi ? “Miwa minne angalia haya mashina hasa huyu bwana mdogo mweusi .”

Wakimlalamikia Kushiwa. Hawa watoto wadogo wana njaa waacheni, Nakumbuka Mikidadi Chite alisema akatoa shilingi tano akawapa wale jamaa wa shamba la miwa.Ugomvi tukaumaliza hivyo tukaondoka zetu nyumbani.

Wakati tunazungumza na wenye shamba ambao mimi nilikuwa nawafahamu kwani tulikuwa tunasali nao kanisani pamoja lakini sikuwa nimewazoea. Mohamed Mwarami hakusema kitu alikuwa kimya yeye na Lydia Mwambene katika tukio hilo. Wazungumzaji alikuwa Mikidadi Chite na Mwanakwetu hata kwa umri tulikuwa wakubwa kwao.

Ilipofika mwezi wa sita siku ya kufunga shule mwaka 1990 wanafunzi wote tulikalishwa chini ya mwembe dodo mkubwa uliokuwa na kivuli walimu waliwekewa madawati mbele tukasomewa matokeo tangu darasa la kwanza hadi la saba na wale waliofanya vizuri watatu kila darasa walipewa zawadi: peni , kalamu ya risasi na madaftari.

Wanafunzi wa darasa la tano aliyefanya vizuri taaluma alikuwa Mohamed Mwarami. Aliyefanya vizuri kwa darasa la saba nafasi ya kwanza alikuwa Ali Ngondo akachukua zawadi yake akatajwa wa pili na watatu. (Hawa wawili simulizi zao nitazisimulia siku nyingine).

Huyu Mohamed Mwarami, mwalimu mkuu alimsifia zaidi kwa sifa zingine tatu kwanza monita bora, mwanafunzi mtulivu,Golikipa bora wa timu ya shule kwa mpira wa miguu na mwanafunzi mwenye mwandiko mzuri.

Shule nzima ilifahamika kwamba Mohammed Mwarami ni kiongozi darasani (monita), Mohammed Mwarami ana akili darasani, Mohammed Mwarami ni Golikipa Mzuri lakini hili la mwandiko mzuri waliokuwa wakifahamu ni wale waliokuwa wanasoma nae darasa moja akina Lydia Mwambene, mwalimu mkuu ambaye alikuwa mgeni wakati huo aliumwaga mtama kwenye kuku wengi.

Utani sasa ukawa ni huu wa mwanafunzi mwenye mwandiko mzuri, Mwanakwetu nilikuja kufahamu kuwa Mohamed Mwarami anakaa Mbagala Kizinga jirani na kwetu na mama yake akiitwa Mama Mzungu au Nyambonde-Asia Abdala Mandingo (Mluguru/Mndengereko).

Mama huyu alijulikana kwa jina hilo la Mama Mzungu kwa kuwa alizaa watoto wengi weupe sana akiwamo Mohamed Mwarami mwenyewe golikipa wa timu ya shule na mwanafunzi mwenye mwandiko mzuri.

“Wakati Martini Pius Mkapa yupo Mohamed Mwarami golini shule yoyote iligwaya tulikuwa tunashindana nao Kijichi tulishinda tu .” Wanafunzi wa Mtoni Kijichi walinisimulia.
Mwanakwetu akaenda kusoma Tambaza, wakati wote huo Mohamed Mwarami alikuwa akichezea Timu ya AFC Tesema, Abuja FC na Agaton FC zilizokuwa zinafanya mazoezi pamoja.

Baadaye nikaambiwa sasa Mohamed Mwarami anacheza soka Msumbiji, Mungu bahati alipofika kocha Marcio Maximo alimchagua kuwa Golikipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Tanzania ((Taifa Stars) .

Kwa kuwa mwanakwetu ni mwingi wa simulizi nikasema leo ngoja nimkumbuke ndugu yangu huyu Mohamed Mwarami ambaye alikuwa mwanafunzi mwenye mwandiko mzuri.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news