NGOJA TUSUBIRI-NETIONE

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIKU moja nilialikwa katika shule fulani kuwa mzazi rasmi kwa watoto wanaohitimu kidato cha nne huko Lushoto. Nilipofika hapo jukumu langu lilikuwa kusema maneno machache huku walimu wa shule hii wakiniongoza.

Wakati mahafali haya yanaendelea nikapewa jukumu yla kusimamia kidogo harambee, kwa kuwa niliwahi kuwa mtumishi wa serikali eneo hili niliwaomba watumishi kadhaa wa umma niliowahi kufanya nao kazi waje kuniunga mkono.

Watumishi kadhaa wa umma waliinuka walimu, wauguzi, maafisa kilimo, watumishi wa mahakama, madiwani na mbunge wa jimbo hilo la Lushoto Mhe.Shabaan Shekilindi, jumla kuu ya fedha taslimu ilikuwa milioni mbili na ahadi ni milioni moja na laki nne.

Nilipotoka pale nikawa natafakari na kubaini unaposema serikali kwa ujumla wake mahakama, bunge zinaingia moja kwa moja.

Hiyo ndiyo dhana sahihi hata leo mwananchi akienda mahakamani anapokosa haki yake hasira yake anaweza kuihamishia kwenye uchaguzi, kwa kuwa hawezi kumuadhibu hakimu au jaji, lakini mwenyekiti wa kijiji, diwani, mbunge na hasa rais sanduku la kura linakuwa muamuzi, mwisho wa siku.

Kosa wanaloadhibiwa hawa watu wanne inawezekana limefanywa na mahakama. Katika hii mihimili mitatu, mihimili miwili Serikali na Bunge pekee sanduku la kura huwa ni kipimo, wakati mahakama inakuwa kando ikitazama mchezo unavyokwenda.

Kwa nini ninasema hilo? Novemba 9, 2022 nilitumiwa katuni ya Kipanya kama inavyojieleza hapo juu. Chini ya katuni hiyo yaliambatana na maelezo haya,

“Nadhani kamati iliundwa Oktoba 12, 2022 maana hiyo katuni ilichorwa Oktoba 13, 2022.” Kuonesha msisitizo Novemba 15, 2022 ndugu huyu akatuma ujumbe huu,“Hivi hii tume (kamati) ya uchunguzi wa mambo ya Shule ya Sheria kwa vitendo itakuja na majibu kweli, siku 30 zimepita.”

Mawasiliano hayo yanatoa taswira ya kiu aliyonacho ndugu huyo, hamu kubwa yakupata matokeo ya kamati hii, ndani ya juma moja baadaye ndugu huyu anatilia mashaka kamati hiyo kuwa kama inaweza kuwa suluhu ya kadhia hiyo.

Mwanakwetu nilimtafakari mno ndugu huyu, aliye njia panda na ninasema nini? Dkt.Harisson Mwakyembe binafsi ninamfahamu kwa karibu akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Yeye kama mwanahabari hilo sina mashaka nalo kabisa, lakini mashaka yangu kwa ndugu yetu huyo yapo kwa yeye kama mwanasheria na yeye kama mhadhiri wa sheria, hapo nina mashaka makubwa mno.

Kwa nini Mwanakwetu ninaliweka doa jeusi kwa kondoo mweupe wakati sikukuu imekaribia? Inawezekana yote yaliyoifikisha hapo shule ya sheria kwa vitendo Dkt.Harisson Mwakyembe anayajua vizuri, anayafahamu kwa kina na aliweka baraka zake kufanyika.

Siamini baraka hizo alizoziweka akiwa na mamlaka makubwa anaweza kuthubutu kuzilaani akiwa mamlaka madogo ya mwenyekiti wa kamati ya kadhia hii.

“… hii timu ya watu saba watakabidhiwa hadidu za rejea na Katibu Mkuu na timu itaripoti kwa Katibu Mkuu na itawasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu, kwa mujibu wa hadidu za rejea watakazopewa… na ikikamilisha ripoti yake nakuomba Katibu Mkuu umuagize Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo aitishe mkutano kama huu, ili mwenyekiti aje awape findings siyo sisi tena, ( mweyekiti aje awape findings ) na maswali andaeni meeengi sana kwa huyo mwenyekiti.” Waziri wa Katiba na Sheria mhe. Dkt Damas Ndumbaro.

Mwanakwetu mkumbuke yule mbunge wa Lushoto Shaaban Shekilindi na madiwani wake, wakumbuke wale watumishi wa mahakama wa Lushoto wakumbuke pia wale watumishi wa umma walimu na wauguzi walivyoniunga mkono katika harambee ya mahafali ile waliificha aibu ya mzazi rasmi, kadhia hii siyo ya kumuachia mzazi rasmi ataabike na harambee yake, akipata aibu mzazi rasmi tumepata sote.

Watu wana kiu ya kujua harambee yetu imekusanya kiasi gani? Wasambaa wanasema, netione ( ngoja tusubiri).

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Post a Comment

0 Comments