MWANANGU AMEKUWA MKUBWA

NA ADELADIUS MAKWEGA

HUKU ndoa ya Uzi na Hedika ikiwa katika mawimbi mazito yaliyopewa ukubwa wa tufani mabegani kwa Hedika, hilo likimfanya ashindwe kuubeba mzigo huo, akitangatanga kuutafuta msaada huo na pa kuutua.
Hali hiyo ilimnyima raha mno Hedika, alikaa na kutafakari je anafanya nini? Je anatokaje katika mawimbi hayo na kuweza kupata faraja na utulivu moyoni mwake? Alikaa na kutafakari hilo faraja yake kubwa ilikuwa ni watoto wake 10 aliozaa na Uzi. 

Huku akitamani Mungu amrudishie ubinti wake na watoto wote 10 warudi tumboni, arejeshewe ubikira wake atafute mchumba mwingine, lakini wapi Mwanakwetu, hayo yalikuwa ndoto huku ndimi zake zikiona.

Hedika aliwakumbuka wanaume kadhaa aliowakataa enzi hizo, miaka imeenda na hilo halisaidii kulitatua linalomkabili.

Hedika alitafakari na kusema kuwa ili ayapumzishe mawazo yake basi aitafute ahuweni na jibu lilikuwa kufunga safari kwa mwanae pekee wa kiume Ksaveli huko Mpwawa jijini Dodoma.

Hedika alikata tiketi yake ya treni, hakuna wa kumuaga wala wa kumuuliza anakwenda wapi zaidi ya watoto wake, moyoni mwake akitamani mwanaume wa kumuuliza wapi uendako, lakini Angelina Mchiwawo mwanamke wa Kimakonde ameuteka moyo wa Uzi.

“Mke wangu unafungasha kuelekea wapi.” Swali hilo lilikuwa adimu mithili ya nyota ya jaha. 

Alisafiri kwa treni hadi huko na kushuka kituo cha treni cha Gulwe na kuanza safari hadi Kijiji cha Tambi, hapo ndipo mwalimu Ksaveli alikuwa akifundisha. Ksaveli alimpokea mama yake hadi nyumbani kwake.

Hedika alijaribu kumuelezea mgogoro baina yake na mumewe Uzi Bini Petero, Ksaveli akiwa kimya hata la kutamka wala la kufanya maana baba na mama yake aliwakuta wanapendana na yeye kuzaliwa akiiamini kukaa kimya ni suluhu, wazazi wake wote anawapenda.

Novemba 12, Hedika alikuwa Mpwapwa ilikuwa ni siku ya Jumamosi, naye Ksaveli alikwenda kusali jumuiya yake ya Mtakatifu Cesilia, ibada ilifanyia nyumba jirani na Ksaveli. 

“Mama twende kusali katika jumuiya yetu na wenzangu wakakutambue.” Ksaveli alitoka na mama yake hadi katika jumuiya hiyo na kukuta waamini wamekaa vitini kusubiri kusali.

Muongozaji alisalisha vizuri ukafika wakati wa kusoma masomo ya siku hiyo.

“...Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao, waliokushuhudia upendo wako mbele ya kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa Mungu. 

Kwa maana, kwa ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa. Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli....” 3 Yohane. 1:5 – 8.

Msomaji akasema hilo ni Neno la Bwana , Wanajumiya waliitikia tumshukuru Mungu. Mara wanajumuiya hii walisimama, huku msomaji akiwa bado yu mbele yao na kusema tusikilize injili ya leo.

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa. 

Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji Fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 

Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, japokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

Bwana akasema, sokilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?- Luka 18:1-8. Msomaji akasema hilo ni Neno la Bwana, wanajumuiya wakasema Sifa kwako Ee Kristo.

Wanajumiya hii waliketi na kukaribishwa tafakari ya masomo hayo ya siku hiyo. Mwanajumuiya hii aliyesoma masomo haya mawili aliisoma tafakari ya masomo hayo yalikuwapo katika mwongozi wa kitabu cha kanisa hilo, halafu kukawa kimya huku ikitakiwa hata mtu mmoja aliyeelewa masomo hayo atoe tafakari ya masomo hayo. 

Kwa hakika tafakari nyingi zilitolewa juu ya masomo haya kila mmoja akitazama namna maisha ya dunia yanavyopaswa kuwa na malipo ya Mungu kwa wanadamu hapo baadaye kwa yoyote yule atakayemlilia pasi na kuchoka.

Ksaveli alisikiliza masomo na tafakari zote kwa umakini mkubwa akaamua na yeye atoe tafakari asubuhi hiyo. Akisema ndugu zangu katika imani, Kristo! Wanajumuiya wakaitika tumaini letu.

“Mwandishi wa Injili ya leo amezungumzia juu ya kadhi, kadhi akiwa ni mtu aliyesomea elimu ya sheria za dini na jukumu lake ni kutoa haki kwa mujibu wa sheria hizo, Injili hii inamuonesha kadhi akiwa upande wa kutoa haki, huku mama mjane akiwa upande wa kuidai haki hiyo. Mwandishi anampambanua kadhi huyu kuwa ni dhalimu akimaanisha ni muonevu, katili, mwovu, jahili, habidhi hana kabisa uungwana, ustaarabu na ustahifu.”

Ksaveli akawaambia kuwa mwandishi wa Injili hii anatutaka kila mmoja wetu kutazama katika watu tunaowaona ni waovu kwa kipimo chetu cha kibinadamu na hata cha Mungu wapo ambao tunawadai stahiki zetu, anatukumbusha kwanza kuwatambua na kwa kufanya hivyo anahimiza kuondoa upofu na kuona stahiki hizo, pili kuzidai stahiki hizo na hivyo ububu utaondoka , mwisho kuzidai pasi na kuchoka hadi zipatikane.

Hivyo mahabidhi (madhalimu) wataona wanasumbuliwa kwa kudaiwa haki za watu na watachoshwa na madai hayo na punde wakiona wanakerwa na kusumbuliwa mwisho haki za wanyonge zitapatikana.

Kwa desturi yake Ksaveli si muongeaji, siku hii katika Jumuiya hii walistajabu mno.

“Hata katika ngazi ya familia, mama anawajibu wa kudai haki zake za msingi kwa mumewe bila yakuchoka, mathalani baba ameiacha familia na kwenda kuanzisha mji mwingine , mama asikae kimya anawajibu wa kudai haki zake za msingi za ndoa haki za watoto wake iliawaze kupata huduma hizo.

Mama anaposema kwa kuwa mimi kaniacha, sihangaiki naye hilo ni kosa kubwa na huko ni kutokutimiza wajibu wako wa kudai haki za watoto na haki zako, lakini pia yule anayeachwa ataendelea kufanya mambo yake .”

Hata baba anawajibu wa kudai haki zake za msingi kwa mkewe siyo kusema mwanamke mwenyewe kazi kushinda vilabuni, wala sihangaiki naye, shauri ni lake, nako huko itakuwa ni kutokutimiza wajibu.

Mwalimu Ksaveli mtoto wa mwalimu Uzi alimalizia kwa kusema kuwa hata katika siasa pale unapowasonta vidole hawa na wale ni waovu , hawa wameiba kura, hawa wameiba kile, hawa madhalimu. Hilo si kosa lakini katika huo huo udhalimu wao unaowasonta wakiwa viongozi wako unapaswa kudai haki zako kwao na siyo kukaa kimya. 

Kiongozi dhalimu lazima akupatie maji, kiongozi dhalimu akupatia elimu bora kwa watoto wako udhalimu huo huo ulete barabara bora na udhalimu huo huo ulete utawala bora na haki zingine za raia.Kumsonta kidole dhalimu kunaweza kumto hukoa udhalimuni na kuwa mstahiki.

Mwanakwetu wanajumuiya hii walishangazwa sana kumbe Ksaveli, mwalimu mgeni naye anaweza kutafakari vizuri neno namna hiyo, naye Hedika akisema kuwa mwanangu sasa amekuwa mkubwa.

“Kumbe sipaswi kumkasilikia tu mume wangu Uzi, bali napaswa kuhakikisha na mimi napata haki zangu za msingi na za wanangu kutoka kwake, kwani hata kwa dhalimu kuna haki zetu lazima tuzidai.”

Tafakari iliiisha ukawa muda wa kutoa sadaka. “…Toa ndugu , toa ndugu, toa ndugu, toa ndugu, ulichona nacho wewe, Bwana anakuona mpaka moyoni mwako, toa ndugu , toa ndugu, toa ndugu, toa ndugu, toa ndugu ulicho nacho na wewe Bwana anakuona mpaka moyoni mwako.

Wiki nzima Bwana Yesu, Wiki Nzima Bwana Yesu amekulinda vema, sasa nawe ndugu yangu Ujifikirie.

…Toa ndugu , toa ndugu, toa ndugu ,toa ndugu, ulichona nacho wewe, Bwana anakuona mpaka moyoni mwako, toa ndugu , toa ndugu, toa ndugu, toa ndugu ulicho nacho wewe Bwana anakuona mpaka moyoni mwako…”

Ulikamilika wimbo huo wa sadaka huku kila mwanajumuiya hii ya Mtakafifu Cesilia akitoa sadaka yake, sadaka ilibarikiwa na muda wa matangazo ulifika huku Hedika mama wa Ksaveli na mke wa Uzi akitambulishwa kwa wanajumuiya hii.

(Hii ni sehemu tu ya simulizi iliyopo katika Muswada wa Riwaya UZI BINI PETERO.)

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news