NHC yazindua Sera ya Ubia 2022, maagizo yatolewa

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amezindua rasmi Sera ya Ubia 2022 ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
NHC limekuwa likitekeleza miradi ya ujenzi na umiliki wa majengo kwa njia ya ubia na wawekezaji binafsi au sekta ya umma.

Miradi hiyo ilitekelezwa kwa kufuata Sera ya Ubia ya Shirika ya 1993 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1998, 2006 na 2012.

Aidha, marekebisho mengine yamefanyika mwaka 2022 yakilenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ubia.

Sera hiyo inatarajia kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba ikiwa pia ni juhudi za NHC kuunga mkono maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta na kujenga uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu amezidua sera hiyo leo Novemba 16, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambapo amelitaka shirika hilo kuhakikisha kuwa linachambua na kupitia kwa umakini wawekezaji watakaoleta maombi ya ujenzi wa miradi ya ubia ili kupata wawekezaji wenye uwezo wa kukamilisha ujenzi kwa wakati na viwango.

“Huu ni uamuzi mzuri, unathibitisha kwa vitendo na kuunga mkono maono na maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza mitaji yao ili kukuza uchumi wa nchi yetu. Serikali inafahamu kuwa ushirikishwaji wa sekta binafsi utaongeza kasi ya ujenzi na kuwa chachu ya mabadiliko katika miji yetu,”amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Amesema, ushirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi mbalimbali utaongeza kasi na kuwa chachu ya mabadiliko katika miji nchini, hivyo Serikali itashirikiana na wawekezaji kuondoa changamoto zitakazojitokeza ili azma ya kuwekeza mitaji katika sekta hiyo iweze kutimia.

Mbali na hayo Waziri Mkuu amesema, amefurahi kuona shirika hilo limedhamiria kuishirikisha sekta binafsi katika kujenga nyumba za ghorofa katika maeneo inayoyamiliki ambayo ama yamepitwa na wakati ama yana viwanja ambavyo havijaendelezwa.

Amesema kuwa, tangu kuanza kwa Sera ya Ubia mwaka 2012 shirika hilo limeingia mikataba 194 na sekta binafsi ambapo mikataba 73 ilifutwa kwa sababu ya ukiukwaji wa masharti.

Aidha, mikataba 111 yenye thamani ya shilingi bilioni 300 utekelezaji wake umefanyika ambapo mikataba 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 utekelezaji wake umekamilika na mikataba 30 yenye thamani ya shilingi bilioni 60 utekelezaji unaendelea.
Waziri Mkuu amesema, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ina uhaba wa nyumba milioni tatu na mahitaji hayo yanaongezeka kwa wastani wa nyumba 200,000 kila mwaka.

“Upungufu huo, unachangia wamiliki wa nyumba binafsi kutoza kodi kubwa na wakati mwingine kudai kodi ya mwaka mzima kwa mkupuo mmoja,”ameeleza Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema, lengo la Serikali ni kuwezesha wananchi wengi zaidi kumiliki nyumba zinazojengwa na shirika hilo na waendelezaji wengine wa nyumba, hivyo uamuzi huo wa kuishirikisha sekta binafsi unaenda kuongeza idadi ya nyumba nchini na kupunguza pengo la uhaba wa nyumba.

Wenyeviti wa Kamati

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),Mhe.Naghenjwa Kaboyoka mbali na kuwapongeza NHC kwa maandalizi mazuri ya sera hiyo pia ametoa angalizo.

Amesema, kamati yao kabla ya kupeleka taarifa zao bungeni wataangalia kwanza thamani ya fedha, "Tunaamini sera hii itakuwa kwa manufaa ya Taifa letu nzima,kwa hiyo tutakachozingatia ni kwamba je? Uwekezaji huu utakuwa na tija kwa wananchi? Je utasaidia kuboresha uchumi wa nchi yetu, na utasaidia wale ndugu zetu maskini maana hawa wengine wenye hali nzuri wana uwezo wa kujenga nyumba zao.

"Kwa hiyo tunaomba kwamba, pamoja na kujenga nyumba nzuri,zizingatie kwamba nia ya Bunge ni kusimamia matumizi mazuri ya fedha za umma,hata ardhi ni fedha, kwa hiyo uwekezaji usionekane kwamba sisi tunatoa ardhi tu, ile ardhi ina thamani kuliko hata hela ambayo inawekezwa.

"Kwa hiyo tunaomba shirika letu National Housing likisimamiwa na Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu na Waziri mwenye mamlaka haya kwamba tuhakikishe kwamba tusije tukawatajirisha walio matajiri zaidi na tukasahau wananchi wanyonge,"amesema.

Ardhi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Mhe. Ally Juma Makoa (Mb) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kuruhusu NHC kuweza kupata fedha kwa ajili ya kukwamua miradi ambayo ilikwama muda mrefu na kuanzisha miradi mipya ikiwemo ule wa Samia Housing Scheme ambao unaendelea kutekelezwa Kawe Tanganyika Pakers jijini Dar es Salaam.

Amesema, kamati hiyo ina matumaini na matarajio makubwa kuwa shirika hilo linakwenda kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa na kuendeleza makazi ya kisasa nchini.

"Wito wetu kama kamati Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kuliomba shirika la nyumba kuweka bidii kubwa katika kuhakikisha miradi yote wanayoianzisha inakamilika kwa wakati na ubora unaotarajiwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa tunakwenda kuingia ubia na wabia mbalimbali, pia wito wetu kama kamati tunaliomba shirika lijiimarishe katika sekta ya sheria ili mikataba yote wanayoingia ilete tija kwa taifa letu,"amesema Mheshimiwa Makoa.

PIC

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC), Mheshimiwa Jerry Silaa (Mb) amesema kuwa, kamati hiyo ina matumaini makubwa na uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu na wanatarajia mabadiliko makubwa kupitia Sera ya Ubia ambayo inakwenda kushirikisha sekta binafsi katika kutekeleza miradi mbalimbali nchini.

Waziri Mabula

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angelina Mabula amesema kuwa, maboresho ya Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yamelenga kuongeza ufanisi na tija kwa wabia wa shirika hilo.

Waziri Mabula ameongeza kuwa, shirika hilo litafanya uchambuzi wa kina ili kupata wawekezaji makini ambao watashikiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali na kuhakikisha wanaopata fursa hiyo ni wale wenye uwezo wa kuridhisha wa kukamilisha miradi kwa wakati na viwango.

NHC

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu amesema kuwa, sera hiyo imezingatia fursa za uchumi katika kipindi hiki, mafanikio na changamoto katika sera zilizopita.
Pia amesema, sera hiyo itaongeza uwazi na mtu akitaka kuwezekeza kwenye miradi yao isiwe lazima kumfahamu mtu yeyote ili aweze kupata fursa za miradi ya shirika.

"Watanzania watarajie sera ambayo imezinduliwa leo inaenda kuleta majibu mazuri mengi, hususani upande wa uhaba wa nyumba ambao tunao kama nchi.

"Niseme kuhusu sera yenyewe haya yalikuwa ni matokeo ya maboresho ya sera zote zilizofanyika kipindi cha nyuma na maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2012, lakini hayakwenda kutumika.

"Kwa hiyo mara ya mwisho sera iliyotumika ni ya mwaka 2006 kuanzia mwaka 2010 National Housing tulikuwa hatujaingia kwenye sera yoyote ya ubia, lengo tulitaka tu-review, sera ambayo tuli-review mwaka 2012 tuone mafanikio ya ule uwekezaji, tukawa tumejiridhisha sasa hivi tunakwenda kufanya marejeo mapya ya sera yetu ya uwekezaji ambayo inafanyika mwaka 2022 na ndio imezindiwa leo,"amesema Mkurugenzi Mkuu wa NHC.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu amesema,hayo yanafanyika yakiangalia vitu vitatu.

"Cha kwanza yalikuwa yanakwenda kuangalia mafanikio ambayo tulikuwa tumeyapata kipindi cha kwanza kusudi tuweze kuyalinda.

"Cha pili makosa yaliyokuwepo katika sera zilizopita tuanze kujibu zisiwe na changamoto tena. Na tatu twende kuangalia mahitaji ya mbele miaka 20 au 30 ijayo. Kuna uhitaji gani ili kuhakikisha sera hii haijibu tu mambo ya sasa na nyuma bali kuangalia pia mahitaji.

"Sera hii inajipambanua zaidi, ina product nne ndani yake, kuna product ambayo National Housing tunaanza kuwekeza ardhi tu na mwekezaji anaweza kutafuta fedha.

"Sehemu ya pili National Housing tunachangia ardhi na pesa tunajikita kwenye miradi kuanzia shilingi Bilion 50 na kuendelea kwa maana ya kwamba sio kwamba Mwekezaji lazima awe na shilingi bilioni 50, lakini atakuja na mradi wenye thamani ya shilingi 50 na kuendelea ambao sisi tutachangia ardhi na pesa na yeye pesa kama inatosheleza.

"Na kama haitatosheleza tunakwenda kukopa nje kwa pamoja, nafikiri na tutakuwa tunafungua kampuni ambayo inasimamia, nafikiri hilo ni jambo zuri sana kwa Watanzania wanaohitaji miradi mikubwa na wawekezaji wa Kimataifa wanaohitaji kuwekeza miradi mikubwa zaidi.

"Na tatu,tunaita Revenue Sharing Model hapa mwekezaji anakubali kufanya uwekezaji kwa nia ya kuja kugawana na sisi faida na faida tunasema kiwango cha chini ambacho sisi tunatakiwa tukipate ni mara mbili ya thamani yetu ya ardhi.

"Na ya mwisho ni ile mtu anajenga ili atumie mwendelezo, halafu baadaye jengo linakuwa la kwetu.Hizi sera zinalenga kuwasaidia wawekezaji wote wakubwa kwa wadogo tunalenga zisifanyike mkoa wa Dar es Salaam peke yake bali mikoa yote na miradi ambayo tumeianisha ya mwanzo ni katika mkoa wa Dar es Salaam, lakini kila mkoa tumeainisha at least miradi miwili ya chini na kama kuna mtu anahitaji kuwekeza sehemu nyingine katika viwanja vyetu.

"Lakini sio katika miradi hii ambayo tumeianisha tunaomba awe huru kutuambia kwamba mimi mradi huu sikuuona tutaupitisha kwenye mchakato," amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news