NI KISASI NA SAMAKI: Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma

NA LWAGA MWAMBANDE

TAFITI mbalimbali zinaonesha kuwa, samaki ni moja wapo ya vyakula bora ambavyo vina faida za kiafya, hivyo unashauriwa kuvipa kipaumbele katika ratiba yako ya mara kwa mara ya chakula.

Picha na Activechef.

Samaki zimejaa asidi ya mafuta ya omega-3 na vitamini kama vile D na B2 (riboflauini). Pia, samaki wana kalsiamu na fosforasi nyingi na ni chanzo kikubwa cha madini kama vile chuma, zinki, iodini, magnesiamu na potasiamu.

Virutubisho hivyo,husaidia kuweka mwili wako imara na pia kusaidia katika ukuzaji wa mwili na kuboresha utendaji wa utambuzi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,ni haki yako kula aina ya samaki umtakaye kwa kuzingatia kuwa, Mungu ameijalia Tanzania aina mbalimbali ya samaki kuanzia baharini, maziwa, mabwawa na hata wanaofugwa katika kaya mbalimbali nchini, endelea;

1.Kama nikifika Mwanza, ni kisasi na samaki,
Nikifika ninaanza, ni kwa supu ya samaki,
Mchana ninajipoza, ni mtama na sakaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

2.Na zile nyama zingine, huku Mwanza sizitaki,
Hizo ntakula kwingine, huku wala silaiki,
Acha nipate unene, sasa huo naafiki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

3.Ni Ziwa Victoria, limejazia samaki,
Si kwa chombo kupakia, wanavua unacheki,
Hapo wajichagulia, yupi wa kula samaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

4.Tena ninafurahia, sifa ya kwake samaki,
Wala huwezi sikia, ana madhara samaki,
Afya wasisitizia, kwamba tuwale samaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

5.Kama ukifika Mwanza, jaribu onja samaki,
Tena vema ukaanza, mchemsho wa samaki,
Ni tumbo litakuponza, utabakiza samaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

6.Wataka wa kukaangaa, yupi kwako anatiki,
Makange yatapakaa, ni mapishi ya samaki,
Kula changamoto kaa, nakwambia hubanduki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

7.Ukitaka wa kupaka, utampata samaki,
Vijiwe vingi tachoka, watengeneza samaki,
Vingine kula nachoka, lakini siyo samaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

8.Hii ni nyama nyeupe, kiafya sana yatiki,
Itafune uichape, viini wavimiliki,
Ukishakula usepe, tamu yake haitoki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

9.Huu utajiri wetu, ziwa na hawa samaki,
Kwanza ndiyo afya yetu, tunapokula samaki,
Pia ni ajira kwetu, tunapovua samaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

10.Tulitunze ziwa letu, tuzidi kula samaki,
Haya mazingira yetu, vizurizuri yabaki,
Uchafuzi huku kwetu, kwa kweli hatuutaki,
Sangara na hawa sato, kwa kweli wananikoma.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments