MMEWAKILISHA VEMA

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 9, mwaka huu licha ya Simba Queens kuaga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani ikiwa imefuzu nusu fainali, imedhirisha wazi kuwa, Tanzania kuna vipaji vingi vya soka kuanzia upande wa wanawake na wanaume.

Udhirisho huo, unaendelea kutoa hamasa kwa wadau ikiwemo Serikali kuendelea kuwekeza zaidi kwa vipaji hivyo ili viweze kuipeperusha bendera ya Taifa letu katika anga za kimataifa.

Simba Queens kuchapwa bao 1-0 na mabingwa watetezi, Mamelodi Sundown katika dimba Prince Moulay EL Hassan jijini Rabat nchini Morocco, hiyo si mwisho wa safari yao, bali ni mwanzo wa maandalizi mapya kwa ajili ya kusonga mbele zaidi.

Aidha, kuishia nusu fainali, Simba Queens itazawadiwa kitita cha dola za Kimarekani 200,000 (zaidi ya shilingi milioni 440 za Kitanzania). Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,Simba Queens wametuwakilisha vema, hivyo warudi kifua mbele, endelea;


1.Pongezi kwa Simba Queens, hapo mlipoishia,
Na nyie hatuna kesi, hapa kwetu Tanzania,
Mlivyapaa kwa kasi, kwa kweli historia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

2.Ni ya kwanza Tanzania, huko CAF kuingia,
Tena si tu kuingia, kombe mmeshindania,
Hapo mlipofikia, kongole za kuzidia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

3.Pesa lengo mlilifikia, hapo mlipoishia,
Ndivyo tuliazimia, hapo mlipofikia,
Kweli twawafagilia, meibeba Tanzania,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

4.Mwaka huu Tanzania, kimichezo twaringia,
Makubwa yameingia, mbele ya Mama Samia,
Ni mengi ya kusifia, machache ntakutajia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

5.Simba Queens Tanzania, CAF nusu mefikia,
Hiyo ni historia, to Simba twasikia,
Zamani livyoingia, Misri ikaishia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

6.Robo fainali pia, hili kombe la dunia,
Wasichana twaringia, tuwakilisha India,
Mechi ngumu jishindia, na bendera Tanzania,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

7.Tembo Warriors pia, lile Kombe la Dunia,
Nao tulishangilia, pale walipoingia,
Ni robo waliishia, wote twawafagilia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

8.Shindano Madola pia, imewika Tanzania,
Medali zimeingia, tusivyozifikiria,
Wachezaji Tanzania, nao tunawasifia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

9.Na Simba ya Tanzania, CAF ilitangulia,
Kwa Mabingwa nakwambia, Makundi ikaingia,
Yaibeba Tanzania, kote yatutangazia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

10.Na Yanga ya Tanzania, pazuri imefikia,
Makundi imeingia, Shirikisho nakwambia,
Imeshinda Tunisia, yapepea Tanzania,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

11.Taarifa meingia, Tembo Warriors pia,
Wachezaji Tanzania, timu wamejipatia,
Ulaya ninakwambia, ni soka la kulipia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

12.Ni wazi ninakwambia, inapaa Tanzania,
Jinsi huko wasifia, ndivyo tunafurahia,
Wachezaji kulipia, pesa nyingi tatujia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

13.Serikali Tanzania, yake Rais Samia,
Kongole twashindilia, tena twasisitizia,
Michezo mnachangia, pazuri tunafikia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

14.Na wawekezaji pia, ajira mnachangia,
Vijana wanaingia, kipato wajipatia,
Hongera za kwenu pia, mwaijenga Tanzania,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

15.Na Watanzania pia, timu mwazishangilia,
Vizuri watufanyia, nasi tunafurahia,
Kwa kweli mnachangia, haya tunafurahia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

16.Tuazimu Tanzania, juu ngazi kupandia,
Makombe tunasikia, yaweze kutufikia,
Makundi tukipitia, fainali kufikia,
Mmewakilisha vema, rudini kifua mbele.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news