NI MSIBA WETU SOTE:Twawaombea faraja, mlioko duniani

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anawapa pole wafiwa wote na majeruhi wa ajali ya ndege iliyotokea Bukoba mkoani Kagera.

Pia, Mheshimiwa Rais Samia ametoa salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamaila kufuatia vifo vya watu 19 katika ajali hiyo iliyotokea Novemba 6, 2022 saa mbili na nusu asubuhi.

Ndege aina ya ATR 42-500 ya Kampuni ya Precision Air ilikuwa ikitoka jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba na ilipotaka kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba iliangukia Ziwa Victoria, mita 100 kutoka ulipo uwanja wa ndege.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,katikati ya majonzi bado tunaendelea kuuwaza ukuu wa Mungu, kwani licha ya vifo hivyo, idadi kubwa ya abiria waliokolewa, endelea;


1:Katikati ya majonzi, twamuwaza Maanani,
Twabubujika machozi, yalotupata jamani,
Makazi hata malazi, kweli hatuna amani,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

2:Kwetu sote mshtuko, yalotokea ziwani,
Walokuweko hawako, wameishia jamani,
Kwetu ni masikitiko, ajali toka angani,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

3:Kukitoa hatari, sote huenda kazini,
Vifaa vile vizuri, hata tuonavyo duni,
Lengo kuipisha shari, tuipate ahueni,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

4:Walopoteza wazazi, poleni sana jamani,
Na watoto kwa wazazi, poleni hapo nyumbani,
Wenzetu wafanyakazi, sote tuko majonzini,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

5:Wengine tumeguswa sana, ndugu zetu na jirani,
Kweli inauma sana, tuendavyo mautini,
Mungu unayetuona, tupe faraja moyoni,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

6:Ajali hizi ajali, zatumaliza jamani,
Moyo unauma kweli, jinsi twaenda shimoni,
Mipango yetu ya mbali, huishia ukingoni,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

7:Twawaombea faraja, mlioko duniani,
Ghafla na mara moja, ukiwa u mikononi,
Kwa Mungu twajenga hoja, awashike mioyoni,
Twawapa pole wafiwa, ni msiba wetu sote.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
7/11/202

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news