TUNAWAOMBEA WOTE:Twasema bila kusita, Mungu kweli ni Muweza

NA LWAGA MWAMBANDE

MVUVI aliyefahamika kwa jina la Majaliwa ambaye anatajwa kuwa shujaa wakati wa uokozi wa watu waliokuwa katika ndege ya Precision Air iliyoanguka Ziwa Victoria, Novemba 6, mwaka huu na kuua watu 19 akiwemo rubani wa ndege amepewa shilingi milioni moja.
Fedha hizo za mkono wa pongezi zimetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Majaliwa anadaiwa kutumia kasia yake kuvunja mlango wa dharura wa ndege hiyo na kuwezesha kuokoa watu 24 waliokuwa katika ndege hiyo.

Licha ya kutokuwa na elimu ya uokozi na wala kuwahi kupanda ndege, Majaliwa anatajwa kuwa mtu wa kwanza kufika katika ndege hiyo dakika chache tu baada ya kuanguka katika Ziwa Victoria kwa kushindwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema licha ya juhudi na ushujaa uliooneshwa na Majaliwa kwa kushirikiana na wenzake, yafaa tumshukuru Mungu wetu, kwani hajatuteketeza, endelea;


1:Twashukuru Mungu wetu, haujatuteketeza,
Kwa hii ajali yetu, wenzetu tumepoteza,
Pia miongoni mwetu, uhai umeutunza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

2:Kweli ajali za ndege, huwa zinatuduwaza,
Manusura kwenye ndege, ni kudra za Muweza,
Asante kwa hii ndege, uhai ameutunza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

3:Watu ishiri na sita, kuwa hai wameweza,
Twasema bila kusita, Mungu kweli ni Muweza,
Ni mapito tunapita, vigumu hata kuwaza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

4:Pia twawageukia, kuokoa waloweza,
Majini wakaingia, bila yao kuyawaza,
Ili kuwasaidia, wale wasiojiweza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

5:Kutumia nguvu zao, kuokoa wameweza,
Hata zile zana zao, hatari wamepunguza,
Hao mashujaa hao, kwa kweli twawapongeza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

6:Upendo Watanzania, kwa hili mmesambaza,
Mmefanya yenye nia, bila muda kupoteza,
Hili tunafurahia, vile linajieleza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

7:Serikali yetu pia, hatua izoziwaza,
Mahali kupafikia, uokozi kuongoza,
Hiyo imesaidia, maisha kutopoteza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

8:Vitendo walivyofanya, upendo ninauwaza,
Maisha wameyaponya, kuwatoa wakaweza,
Hata miili kufanya, kuitoa wakaweza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

9:Yanapotokea haya, yatupe sisi kuwaza,
Ya kwamba maisha haya, yapo ya kutuduwaza,
Hivyo tusiwe na haya, kuyatenda ya Muweza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

10:Hapa pia twarudia, pole zetu kusambaza,
Wale waliosikia, habari kuwaumiza,
Na ndugu walotufia, hali zetu kulegeza,
Tunawaombea wote, ili wapone haraka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
7/11/2022

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news