Prof.Muhongo awauma sikio viongozi wa CCM waliochaguliwa Mara

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo ameshauri viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochaguliwa wakiwemo wenyeviti wa wilaya pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho atakayechaguliwa kuitisha kikao cha pamoja ili kujadili maendeleo na uchumi wa Mkoa wa Mara.

Prof.Muhongo ametoa ushauri huo leo Novemba 21, 2022 alipokuwa akitoa salamu kwa wajumbe wa uchaguzi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mara katika uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Mjumbe wa NEC na viongozi wengine watakaokitumikia chama hicho tawala kinachoongozwa na Mwenyekiti wake Taifa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Prof. Mubongo amesema, jambo la maendeleo na uchumi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Mkoa wa Mara na nchi kwa ujumla. Ambapo amesema wana Mara na watanzania shauku yao ni kuona uchumi ukikua na kuondokana na umaskini katika kuwa na maendeleo thabiti.

"Nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kusalimia kwenye mkutano huu wa uchaguzi wa viongozi wa CCM Mkoa wa Mara. Ushauri wangu ni kuomba viongozi watakaochaguliwa kuja na mikakati ya kiuchumi kwa kukaa pamoja na kushauriana kuona namna bora ya kukuza maendeleo na uchumi,"amesema Prof. Muhongo.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara anayemaliza muda wake,Samwel Kiboye amesema majina yote ya wagombea yaliyorudishwa ni watu safi ambao wanapaswa kuchaguliwa.

Amesema, wajumbe wanapaswa kuwa makini na kufanya uchaguzi makini ambao utawapata viongozi makini watakaokivusha chama katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Post a Comment

0 Comments