QATAR NITARUDI TENA:Mambo yao ya ukora, wayalete ugenini? Qatar nitarudi tena

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni Mkuu wa Ulinzi wa Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linaloendelea nchini Qatar, Abdullah Al Nassari amesema, akama unataka kuelezea hisia zao kuhusu mapenzi ya jinsia moja, yafaa kufanya hivyo kwa jamii ambayo wanakubaliana na mambo hayo.

Picha na Skynews.

Abdullah Al Nassari alisisitiza kuwa, kamwe wao Qatar hawawezi kubadili utamaduni wao kwa tukio ambalo linachukua siku 28 tu.

Naye mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Qatar,Khalid Salman Al-Muhannad alimwambia mwandishi wa habari wa Ujerumani kuwa, ushoga ni haramu. Unajua nini maana ya haramu? Al-Muhannad alimuuliza mwandishi huyo huku akimfafanulia kuwa,

"Wakati wa Kombe la Dunia, mambo mengi yatakuja hapa nchini (Qatar). Hebu tuzungumze kuhusu mashoga, jambo muhimu zaidi ni kwamba kila mtu atakubali kuja hapa (Qatar), lakini itabidi kukubali sheria zetu". Ushoga ni haramu nchini Qatar chini ya Sheria ya Kiislamu ya Sharia. Ni kwa msimamo huo, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,imani pasipo matendo imekufa, hivyo uthubutu wa Qatar umempa ujasiri, yupo tayari kurudi tena huko, endelea;

1. Imani pasi matendo, imekufa nafsini,
Tuonayo ni matendo, yanatukosha moyoni,
Kuuondoa uvundo, kinyume cha Maanani,
Qatar nitarudi tena.

2. Upo wanuka uvundo, waangalia pembeni,
Wala huupigi nyundo, kuufukia shimoni,
Nyimbo nyingi za matendo, maneno ya mdomoni,
Qatar nitarudi tena.

3. Mnayotangaza kwiyo, ng’oo huko hamuoni,
Kubeza Imani hiyo, mkafanye jalalani,
Hapana yao si ndiyo, iwaelee kichwani,
Qatar nitarudi tena.

4. Hakuna kurahisisha, wafurahie usoni,
Ujumbe lishafikisha, mguu sawa nyumbani,
Walie hata kukesha, mewekwa korokoroni,
Qatar nitarudi tena.

5. Wasema walikosea, kuwaweka ulingoni,
Ila hawakukosea, mipango ya Maanani,
Ili kuwaoneshea, mwenyewe yuko enzini,
Qatar nitarudi tena.

6. Usodoma Ugomora, tuseme shangilieni?
Mambo yao ya ukora, wayalete ugenini?
Mwarabu ameshafura, na wao hawapatani,
Qatar nitarudi tena.

7. Vile wameshaamua, wanailinda Imani,
Kwa sababu wanajua, ni chuki kwa Maanani,
Kwa wale msiojua, zidisha lalamikeni,
Qatar nitarudi tena.

8. Kumbe kwa kizazi hiki, bado yapo ya mbinguni,
Yale Mungu aafiki, livyosema vitabuni,
Japo wengi wanafiki, wayaimba midomoni,
Qatar nitarudi tena.

9. Qatar wamesimama, mengine hawayaoni,
Watasema watakoma, mguu wabaki chini,
Kama noma iwe noma, wanailinda Imani,
Qatar nitarudi tena.

10. Waache huko wajute, walileta Qatar nini,
Sisi mafunzo tuchote, kung’ang’ania Imani,
Wakasirike watete, imeshasimama dini,
Qatar nitarudi tena.

11. Ingawa sijaalikwa, kwenda huko natamani,
Hata bila kualikwa, nikajifanye mgeni,
Na ya kwao nimetekwa, mwilini hadi moyoni,
Qatar nitarudi tena.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments