TARI, Bodi ya Pamba, WFP wasaini mkataba wa kiutendaji kuinua zao la pamba

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Bodi ya Pamba (TCB) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamesaini mkataba wa mashirikiano ya kiutendaji (MoU) katika eneo la mradi wa kuzalisha na kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na mazao mengine ya chakula lishe.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Dkt. Geofrey Mkamilo (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kiutendaji utakaowaongoza kutekeleza programu ya kuinua tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na chakula lishe-ikiwemo mazao ya maharagwe, viazi, mahindi na mbogamboga kwa wilaya za Kwimba, Magu na Misungwi mkoani Mwanza-Novemba 21,2022.

Mradi huo wa mwaka mmoja unaojulikana kama ‘Beyond Cotton,’ unafadhiliwa na Serikali ya Brazil kwa gharama ya Dola za kimarekani 629,000, na kutekelezwa na taasisi hizo, unatarajiwa kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wa zao la pamba takribani 9,000 kutoka wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi mkoani hapa.

Akizungumza muda mfupi baada ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geofrey Mkamilo alipongeza serikali ya Brazili na Tanzania kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na mtazamo chanya katika kuhakikisha zao la pamba na mazao mengine ya chakula yanaendelezwa na kuongezewa tija kwa manufaa ya wakulima wake na ukuaji wa uchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI),Dkt. Geofrey Mkamilo (kulia) akipeana mkono na Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson baada ya kusaini mkataba huo.

Mkamilo alisema kwa namna serikali zote mbili zilivyojipanga, chini ya utekelezaji wa wadau mbalimbali, watahakikisha matokeo ya utekelezaji wa mradi huo yanakwenda kuleta ustawi na ongezeko la ubora na uzalishaji kwenye zao la pamba na kilimo mseto.

“Hafla hii ni fursa ya kipekee katika kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa mnyororo wa thamani kwa wakulima wa ukanda wa pamba, lakini pia kuwajengea uwezo zaidi maafisa ugani wa zao hilo,” alisema Dkt. Mkamilo.
Mwakilishi wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa bodi hiyo, James Shimbe (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kiutendaji utakaowaongoza kutekeleza programu ya kuinua tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na chakula lishe-ikiwemo mazao ya maharagwe, viazi, mahindi na mbogamboga kwa wilaya za Kwimba, Magu na Misungwi mkoani Mwanza-Novemba 21,2022.

Pia Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson, alisema ndani ya mfumo wa Ushirikiano wa Kusini-Kusini, Mradi wa ‘Beyond Cotton’ unalenga zaidi kubadilishana maarifa kati ya Tanzania na Brazili katika mustakabali chanya unaolenga kuongeza tija katika kilimo cha pamba na mazao mengine ya chakula, pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani, ikiwemo kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje.
Mwakilishi wa Bodi ya Pamba nchini (TCB) James Shimbe, (kushoto), Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Dkt. Geofrey Mkamilo kabla ya kusaini mkataba huo.

“Ni matumaini yetu kuwa mradi huu utabadilisha maisha ya wakulima wadogo, sisi WFP nchini Tanzania na Kituo cha Ubora cha WFP dhidi ya Njaa nchini Brazili-tunathamini ushirikiano thabiti wa TARI na TCB ulioanza tangu 2019, na tunatazamia kuendeleza vilivyo ushirikiano huu,” alisema Gibson na kuongeza;
“Naishukuru Serikali ya Brazil kupitia Shirika la Ushirikiano la Brazili, kwa kufadhili mpango huu, na kwa kuwachukulia wakulima wadogo wa Tanzania kama wadau watarajiwa katika sekta ya pamba. Pia ningependa kushukuru Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Campina Grande na Taasisi ya Pamba ya Brazili kwa kusaidia mradi huu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa TCB, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa bodi hiyo, James Shimbe, alisema ustawi, tija na ongezeko chanya la uzalishaji wa zao la pamba nchini linategemea zaidi utafiti. Hivyo katika kutekeleza azma ya mradi huo TCB, TARI na WFP wamejipanga kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na halmashauri zote zitakazofikiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Naye, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa TARI, Profesa Joseph Ndunguru alisema pamoja na mambo mengine, mradi huo unakwenda kufanya utafiti na majaribio ya mbegu, kutoa mafunzo ya kilimo cha pamba na mazao lishe mengine, ikiwemo viazi, mahindi na maharagwe lishe.

Kwa mujibu wa Ndunguru, mradi huo unakwenda kuongeza thamani kwenye uchakataji wa pamba kwa AMCOS 9 ndani ya wilaya 3 za Kwimba, Magu na Misungwi-na baadaye matokeo tarajiwa yatasambazwa nje ya wilaya hizo na kwingineko nchini kwa lengo la kueneza teknolojia ya mradi huo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI-Ukiruguru mkoani hapa, ambaye pia ni mratibu wa zao la Pamba nchini, Dkt. Paul Saidia, aliainisha baadhi ya mambo yatakayotazamwa zaidi katika utafiti kulingana na mkataba huo kuwa ni pamoja na kuongeza thamani kwa kuwa na mbegu bora za pamba, kuongeza usalama wa chakula na namna ya kupambana na magugu.
Washiriki wa hafla hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja.

“Na tunatarajia wakulima takribani 9,000 wa pamba watakaofikiwa wataelimishwa juu ya kilimo cha maharagwe lishe, viazi lishe na mbogamboga, pia mradi huo unatarajia kujenga matanki makubwa yatakayosaidia kuvuna maji ya mvua,” alisema Dkt Saidia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news