Rais Dkt.Mwinyi aieleza Marekani mipango ya Serikali ya kulipaisha zao la mwani

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiomba Serikali ya Marekani kusaidia juhudi za Serikali katika uzalishaji na kuliongezea thamani zao la Mwani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi maalum ya Mlango wa Zanzibar mgeni wake Naibu Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Marekani , Dkt.Jewel Hairston Bronaugh, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi ametoa rai hiyo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo ya Marekani, Dkt. Jewel Bronaugh aliyefika Ikulu na ujumbe wake kwa mazungumzo.

Amesema, kupitia Sera ya Uchumi wa Buluu, Serikali inalenga kuimarisha kitaalamu uzalishaji wa zao la mwani ili kuliongezea thamani na kuwaletea tija wakulima, akibainisha akinamama ndio wakulima wakubwa wa kilimo hicho.

Alisema, Zanzibar ni nchi yenye ardhi ndogo ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikizalishaji zao la karafuu.

Dkt. Mwinyi amesema, Serikali inakusudia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa ajira kwa vijana kupitia sekta ya uvuvi akibainisha sekta hiyo ina mchango mkubwa wa kufanikisha hilo pale itakapokuwa na mfumo bora wa uvuvi na uchakataji.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika uimarishaji wa miundombinu ya kiuchumi kwa kuviimarisha Viwanja vya Ndege vya Unguja na Pemba pamoja na Bandari.

Aidha, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa kuwepo muundo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa hapa nchini kumefungua milango ya Uwekezaji kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo ya Utalii, hivyo akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa watalii wa Marekani kuja nchini, huku akisifia juhudi za serikali katika uimarishaji wa miundombinu pamoja kuwepo kwa vivutio vingi vya utalii.

Ameishukuru Serikali ya Marekani kwa mashirikiano yake ya muda mrefu na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na misaada mbali mbali ambapo nchi hiyo imekuwa ikiisaidia Zanzibar, ikiwemo ile inayopitia Shirika la misaada la ‘USAID’.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo ya Marekani, Dkt. Jewel Bronaugh ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano yake na Marekani na kuahidi kuendeleeza ushiirikiano huo kwa faida ya nchi mbili hizo.

Amesema, lengo la ziara yake hapa nchini ni kukuza ushirkiano wa kibiashara kati ya Zanzibar na Marekani, ambapo wafanyabiashara wa nchi hiyo watapata nafasi ya kuangalia fursa kupitia sekta za kilimo na utalii.

Aidha, amesema Serikali ya Marekani ipo tayari kusaidia juhudi za Serikali katika uimarishaji wa maeneo mbali mbali ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news