NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa msikiti wa Rahmman kuweka utaratibu maalum wa kuwawezesha walimu wa Madrasa, ili waweze kujikimu na kutekeleza vyema majukumu yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika kuitikia dua ikisomwa na Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume (hayupo pichani) baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Rahman Kijichi Wilaya ya Magharibu “A” Unguja.(Picha na Ikulu).
Alhaj Dkt. Mwinyi amewaeleza hayo waislamu baada ya kukamilisha ibada ya sala ya Ijumaa Novemba 11, 2022, iliyofanyika Masjid Rahman uliopo Kijichi Mkoa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema, kuna umuhimu kwa uongozi wa msikiti huo kuweka utaratibu maalum utakaowawezesha waislamu kutoa michango yao kwa ajili ya kuwawezesha walimu wanaofundisha katika madrasa ya msikiti huo ili waweze kujikimu kimaisha na kutekeleza vyema majukumu yao ya kufundisha.
“Sasa huyu mtu tunamkabidhi watoto wetu kusomesha kitabu cha Mwenyezi Mungu, ataishi vipi bila ya kumuwezesha?,”alihoji Alhaj Mwinyi.
Aidha, amesema hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na kuwawezesha maimamu pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuutunza msikiti huo kwa kuufanyia matengenezo ya mara kwa mara pale vifaa ikiwemo mifereji inapoharibika.
Alhaj Mwinyi amesema pamoja na msikiti huo kutumiwa kwa ajili ya sala, lakini pia inapaswa kutumika kwa shughuli nyinginezo za ibada.
Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amemshukuru Rais Alhaj Dkt. Mwinyi kwa kuungana na waislamu na kushiriki katika ibada tofauti katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, ikiwemo ufunguzi wa misikiti katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba, na hivyo akawaomba waislamu kuendelea kumuombea dua.
Mapema, Katibu katika sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Omar aliwataka waislamu kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuonesha ucha Mungu wao kwa kuepuka yale yote aliyoyakataza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa Kijichi baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Rahman Kijichi Wilaya ya Magharibu “A” Unguja.
Aidha, amewataka waislamu kuwa na mwamko katika kutafuta elimu ya dini yao, sambamba na kuwa na msimamo wa kushukuru neema za Mwenyezi Mungu, ikiwemo uwepo wa amani nchini.
Msikiti huo wa ‘Masjid Rahmman ulifunguliwa Ijumaa iliyopita, ambapo Rais Alhaj Dkt. Mwinyi aliwakilishwa.