Rais Samia aagiza kijana aliyeokoa abiria katika ajali ya ndege apewe ajira

NA MWANDISHI WETU

RAIS Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana Majaliwa Jackson aliyeona ndege ikianguka na kuamua kwenda kutoa msaada wa uokoaji akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na aingizwe katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili apate mafunzo zaidi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpongeza na kumfariji kijana Jackson Majaliwa kwa ushujaa wake wa kuwahi katika eneo ilipotokea ajali ya ndege ya Shirika la Precision na kuwaokoa abiria waliokuwa wameshindwa kutoka ndani ya ndege hiyo. Maombolezo ya kuaga miili ya watu wa ajali hiyo yamefanyika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Mkoani Kagera 7/11/2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Hayo yamesemwa leo Novemba 7, 2022 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiongoza wananchi kuaga miili ya watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege ya shirika la ndege la Precision katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Ajali ya ndege hiyo aina ya ATR 42-500 yenye namba za usajili 5H-PWF iliyotokea jana asubuhi wakati ikijaribu kutua katika kiwanja cha ndege cha Bukoba ikiwa na watu 43 wakiwemo abiria 39, marubani wawili na wahudumu wawili.

Amesema kwamba taarifa za uokoaji zinaonesha kuwa watu waliookolewa ni 24 wakiwemo abiria 22 na wahudumu wa ndege wawili na waliopoteza maisha ni watu 19 wakiwemo abiria 17 na marubani wawili.

Pia, Waziri Mkuu amesema Rais Mheshimiwa Samia ameelekeza mazishi ya wahanga wote yatagharimiwa na Serikali, hivyo, amewaelekeza wakuu wa Mikoa katika maeneo husika wasimamie kikamilifu shughuli hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri ambazo Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wenyeviti zitaendelea kuimarishwa ili ziweze kuchukua hatua za haraka maafa yanapotokea.

Waziri Mkuu amesema kwa niaba ya Serikali ameendelea kuwapa pole wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki na anawatakia safari njema na maziko mema kwa wale wanaosafiri kwenda mbali na maeneo hayo ya Bukoba.

Awali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu Watanzania kuwa waendelee kutumia usafiri wa anga kwa kuwa mamlaka husika zipo na zinasimamia na kuchukua hatua stahiki ya kuhakikisha uwepo wa usalama wa anga kwa ajili ya safari za ndani ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news