Rodrick Masawe adakwa akitumia kivuli cha JWTZ kufanya uhalifu Tanga

NA DIRAMAKINI

RODRICK Masawe mkazi wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga amekamatwa na makachero wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na bastola (pistol) bandia iliyotengenezwa kienyeji ambayo amekuwa akiitumia kufanyia vitendo vya uhalifu huku akijifanya kuwa ni mtumishi wa serikali wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mtu mwingine anayeshikiliwa kwa tuhuma za kumiliki bastola iliyotengenezwa kienyeji ni Huruma John ambaye alikamatwa Mtaa wa Kisosora kata ya Nguvumali jijini Tanga.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia silaha hizo kwenye matukio mbalimbali ya kihalifu.

Amesema, Rodrick Masawe alikamatwa katika Kijiji cha Mamboleo wilayani Muheza akiwa na pistol bandia na kujifanya mtumishi wa JWTZ ambapo mtuhimiwa huyo yupo mbaroni kwa hatua za kisheria.

Kamanda Mwaibambe ameelezea mtuhumiwa mwingine Huruma John aliyekamatwa na silaha ya pistol bandia alikutwa eneo la Kisosora Kata ya Nguvumali Tarafa ya Chumbageni jijini Tanga akiwa na silaha hiyo kwenye begi lake la mgongoni ambapo mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Wakati huo huo, Kamanda Mwaibambe ameeleza kukamatwa kwa Mtua Wambura mwenye umri wa miaka 50 mkazi wa Mwakijembe kwa tuhuma za kukutwa na pembe tatu za mnyama aina ya pongo akiwa amezihifadhi kwenye begi dogo nyumbani kwake kinyume cha sheria ambapo uchunguzi unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Pia Kamanda ameeleza kuwa, Mkoa wa Tanga umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kampeni ya usalimishaji wa silaha kwa hiari ambapo jumla ya silaha 488 zimesalimishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news