Serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya Sheria ya Habari kwa watunga sheria-Waziri Nape

NA DIRAMAKINI

TAFITI mbalimbali zinaonesha kuwa, uandishi ni taaluma inayoweza kusaidia kupatikana kwa mitazamo na maoni ya aina mbalimbali kwenye nchi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, vyombo vya habari hutoa fursa kwa watu kuhabarishwa na wao kuweza kujenga na kueleza mitazamo yao.
Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma leo Novemba 9, 2022.

Pia tasnia imara ya habari huwezesha jitihada za kushawishi kupatikana kwa hoja mpya na mabadiliko muhimu, na kufuatilia utendaji wa Serikali ili kuifanya iwajibike kwa wananchi wake.

Kwa msingi huo, waandishi wa habari hutegemea taarifa kutoka kwenye vyombo na taasisi mbalimbali, na vyanzo vinavyoaminika wakiwemo wafichua uhalifu mbalimbali ili kuandaa habari na kuiarifu jamii.

Sheria zinazowezesha kuliko kuzuia juhudi hizo zinatajwa kuwa ni muhimu katika utendaji wa waandishi na kushamiri kwa tasnia nzima ya habari.

Hapa nchini kuna sheria, taratibu na miongozo mbalimbali iliyowekwa na mamlaka husika ambazo husimamia haki na wajibu wa vyombo vya habari katika kuchapisha, kurusha na kusambaza taaarifa mbalimbali.

Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016 (The Access to Information Act-2016),Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 (The Media Services Act-2016),Sheria ya Makosa ya Mtandao Tanzania 2015 (The Cybercrimes Act-2015) na nyinginezo.
Kati ya sheria hizo, wadau wa habari wamekuwa wakielekeza kilio na malalamiko yao serikalini kuwa, kuna haja ya kufanyiwa maboresho ili vyombo vingi vya habari viweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo wa kuwapasha habari wananchi.

Hivi karibuni,Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro alipokutana na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) jijini Arusha alisisitiza, changamoto za kisheria zinazoikabili taaluma hiyo kwa sasa,wakati mzuri wa kuzifanyia kazi ni huu.

“Rais tuliye naye sasa, Mheshimiwa Samia (Suluhu Hassan) ameonesha moyo na nia kubwa ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini.

“Kwa sasa mazingira ni mazuri na yanaruhusu. Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, maana mkisubiri miaka 10 ijayo, huwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,”amesema Dkt.Ndumbaro.

Rais Samia tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.
“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Waziri Nape

Huku Serikali ikiwa katika juhudi za kutekeleza maagizo ya Rais Samia, kuhusu maboresho ya sheria zinazoonekana kuwa kandamizi kwa vyombo vya habari nchini,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye amesema,Serikali ilishindwa kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari bungeni katika Bunge la Novemba, mwaka huu, kwa sababu baadhi ya taratibu hazikukamilika.
Mheshimiwa Nape ameyasema hayo leo Novemba 9, 2022 wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma.

Amesema,Serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo, lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutano kutoka kwa wadau wa habari.

Kwenye kikao hicho na CoRI, Waziri Nape amesema,Serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya Sheria ya Habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali kitakachofanyika Novemba 22, 2022, jijini Dar es Salaam.

‘‘Serikali tupo tayari kupeleka mabadiliko ya sheria ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho. Baada ya kikao hicho tutakubaliana tuliyokubaliana na ndio yataenda,"amesema Nape.

Amesema, haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.

‘‘Sisi kama serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema. Isingefaa kwenda na mabadishano bungeni. Mpaka sasa kuna maeneo ambayo bado hatujakubaliana na kikao hicho cha mwisho ndio kitatoa mwelekeo wa mapendekezo yote.

‘‘Sisi kama tupo happy (tunafuraha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’amebainisha Waziri Nape huku akitoa akishauri.

Mheshimiwa Waziri Nape amebainisha kuwa,pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.

‘‘Hata kama kuna mapitio tunayofanya, lakini lazima tuangalie uhalisia wa nchini,’’amesema Waziri Mheshimiwa Nape.

Akizungumzia takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape amesema, wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.

‘‘Katika Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Rais aliagiza wizara kutaka kukutana na wanahabari. Tunafanyia kazi hilo,’’ amesema Nape.

Kwa upande wake Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), ameshauri wanahabari kubaki pamoja kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Tutumie vizuri kipindi hiki ambacho serikali imekuwa tayari kusikiliza. Tubaki pamoja mpaka mwisho,’’amesema Msigwa.
Naye Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF ameomba wadau wa habari kushiriki vema katika kikao cha mwisho cha Serikali na wadau wa habari kwa kuwa ni muhimu.

‘‘Kama kuna mtu anawazo, alilete kupitia umoja wa haki ya kupata habari ili kwenye kikao hicho tuwe na lugha moja,’’amesema Balile.

Kwa upande wake, Dkt.Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) amesema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.

‘‘Tunapaswa kutoa mawazo yetu, lakini ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliana ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka. Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ amesema.

James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN) amesema katika kikao cha pili, hakuna jambo litalobaki bila kushughulikiwa.

‘‘Baada ya kikao cha pili kama ambavyo imeelezwa na serikali, tunaamini mabadiliko yatakayopelekwa bungeni yatakidhi matakwa ya wanahabari kwa ajili ya kunufaishi wananchi, serikali na tasnia kwa ujumla,’’amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news