Ujenzi Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi wafikia asilimia 69, Rais Dkt.Mwinyi aridhika

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi katika hospitali mpya ya Mkoa wa Mjini Magharibi, inayoendelea kujengwa katika eneo la Lumumba.
Dk. Mwinyi amesema hayo Novemba 19, 2022 katika ziara fupi alipotembelea hospitali hiyo ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wake.

Akizungumza na viongozi, watendaji na wananchi walioshiriki katika ziara hiyo, Dkt. Mwinyi alisema amefurahishwa na kasi ya Mkandarasi anayeendeleza mradi huo, ambapo hadi sasa hatua za ujenzi zimefikia asilimia 69 ya kazi yote.

Amesema, kuna kila sababu ya kujivunia kwa uwepo wa hospitali hiyo ambayo ni ya aina yake hapa Zanzibar.
Amesema, Serikali ina matarajio makubwa kuwa Hospitali hiyo itakamilika ujenzi wake na kuanza kutumika ifikapo mwezi Aprili 2023 , na kuwa Hospitali mbadala katika kuendeleza tiba na kupisha ukarabati mkubwa unaotarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.

Aidha, amebainisha azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha kila mkoa hapa nchini unakuwa na hospitali ya aina hiyo.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi amewatoa hofu wajasiriamali wanaojihusisha na kazi za kutengeneza vyombo vya moto ambao wamelazimika kusimamisha shughuli zao na kuhama eneo hilo ili kupisha ujenzi wa hospitali hiyo.

Amewathibitishia wajasiriamali hao kuwa, tathmini kwa ajili ya malipo yao tayari imefanyika na wanatarajiwa kulipwa katika kipindi kifupi kijacho.

Aidha, amewahakikishia kuwekewa miundombinu muhimu katika sehemu yao mpya kazi.
Wakati huo huo, Mapema, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui alielezea maendeleo ya kazi za ujenzi wa hospitali hiyo na kusema kabla hospitali hiyo ilitarajiwa kukamilika ujenzi wake mnamo mwezi Januari 2023, lakini kutokana na changamoto ya kuibuka kwa Ugonjwa wa UVIKO-19, baadhi ya vifaa vilivyotarajiwa kutumika vilichelewa kufika nchini. Hata hivyo akabainisha kuwa tayari mahitaji mengi ya vifaa yameshakamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news