Vigogo HESLB walioila chenga Kamati ya Waziri Mkenda mikononi mwa Bunge

NA DIRAMAKINI

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeutaka uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB) kufika katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii siku ya Novemba 4, 2022 ili kujieleza kwa nini hawataki kusikiliza maelekezo ya Serikali.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson. (Picha na MCL).

Maagizo hayo yametolewa Novemba Mosi, 2022 bungeni jijini Dodoma na Spika Dkt.Tulia Ackson ikiwa ni siku chache Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda na baadhi ya wabunge kulalamikia kuwa kamati aliyoiunda kuchunguza utoaji wa mikopo ya elimu ya juu imeshindwa kupata ushirikiano.

Oktoba 25, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Prof.Mkenda alisema kuwa, bodi hiyo inasuasua kutoa ushirikiano kwa kamati aliyoitangaza Julai 31, mwaka huu alipotembelea ofisi za bodi hiyo maeneo ya Tazara jijini Dar es salaam.

Waziri Mkenda alieleza kuwa, majukumu aliyoyatoa kwa kamati hiyo ilikuwa ni kuchunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa zilizoainishwa.

Prof. Mkenda alisema kuwa, atakula kichwa cha mtu kama Bodi ya Mikopo itaendelea kusuasua katika utekelezaji wa kazi hiyo.

“Mara wapite huku mara watokee huku,lengo la timu hii tungependa kile kidogo tulichonacho kitolewe kwa haki kusaidia wale wenye mahitaji makubwa zaidi. Lakini pia kuhakikisha kwamba hakuna fursa ya mimi waziri, mtoto wangu au ndugu zangu wenye uwezo kuhakikisha wao wanapata kwa sababu wao wana connection wakati mtu ambaye hana connection hapati,”alisisitiza Waziri Prof.Mkenda.

Waziri Mkenda alionesha masikitiko yake dhidi ya HESLB na kueleza kuwa kamati hiyo imechelewa kufanya kazi yake kwa sababu ya ‘lobbying’ (inashawishi) huku na kule ilihali wakifahamu kwamba kamati ya waziri haisimamishwi kufanya kazi.

“Wasi-lobby na bodi ya mikopo nitawachukulia hatua wakiendelea kufanya lobby-lobby kwa sababu wanataka kutuambia na wenyewe wanataka kuficha mambo. Ile kamati ifanye kazi, taarifa ni yetu tutaifanyia kazi kwa ndani kwa sababu sisi hatulengi kwenda kumuumbua sijui mtoto wa Salum amepata mkopo hapana.

“Sisi tunataka kujisahihisha ili kuhakikisha kwamba kile ambacho Serikali imetenga kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi kinaenda kwa mlengwa, sasa ninataka kutoa onyo ya kwamba kwenda kulobby sijui eti waziri asimamishe kamati isifanye kazi…hiyo lobbying inaonesha kuna madudu.

“Natuma salamu kwa bodi ya mikopo kwa sababu niliona wamejaribu wanasema ooh tumeitwa sijui tumetuma tusimamishe wakati kazi nimeitoa mimi na mimi ndio nimepewa kazi ya kusimamia mikopo.

“Bungeni watu wanalalamika sana, wanasema kuna yatima hawapewi mikopo, halafu watu wenye uwezo wanapewa mikopo, mimi naunda kamati halafu nisikie kuna mtu anasema waziri asiunde kamati, aah! Nitakula kichwa cha mtu,” alisisitiza Waziri Prof.Mkenda.

Katika hatua nyingine, Dkt.Tulia ametoa uamuzi huo baada ya Bunge kujadili hoja ya uwepo wa wanafunzi wenye vigezo kukosa mikopo ya elimu ya juu, hoja iliyotolewa na Mbunge wa Biharamulo (CCM), Ezra Chiwelesa

“Ninaamini kwamba Waziri hawakusikilizi kwenye mambo mengine, lakini kwenye hili watakusikiliza wao wataitwa katika Kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii…Siku ya Ijumaa saa 7.00 wajikute kwenye hiyo kamati.

"Tutatoa fursa tujue kama ni kiburi ama kitu kingine tofauti kwa ngazi hii. Kwa maana ya kuichunguza kama inatoa mikopo sawa sawa sio hoja wanazoitiwa ndani ya kamati, sasa hivi tunataka kuelewa kama Bunge kwa nini hiyo bodi haisikilizi hayo maelekezo,”amesema Dkt.Tulia.

Amesema kuhusu hoja kama HESLB inatoa mikopo sawa sawa itajadiliwa Februari, mwakani wakati Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itakapokuwa inatoa taarifa yake bungeni na hivyo kuona kama kuna haja ya Bunge kuunda tume ya kuchunguza bodi hiyo ama la.

Hata hivyo, Kamati hiyo ya kufuatilia utoaji wa mikopo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 aliyoitangaza Waziri Mkenda, inaongozwa na Profesa Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt. Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya kompyuta na takwimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news