Waarabu wanusa fursa za kiuchumi Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar

NA DIRAMAKINI

MUUNGANO wa Jumuiya za Waarabu wafanyabiashara (The Union of Arab Chambers) ambao ni wawakilishi rasmi wa sekta ya binafsi ya Waarabu, wamethibitisha kwamba kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2022 nchini Qatar ni jambo la kujivunia kwa watu wote wa eneo la uarabuni.

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya kuhitimisha mkutano wa 133 wa Bodi ya Wakurugenzi wa Muungano wa Nchi za Kiarabu (UAC) uliofanyika hivi karibuni huko Kuwait.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo, imefafanua kuwa, Mkutano wa Sekta Binafsi wa Kuwait pia ulisisitiza kwamba Kombe la Dunia litafungua upeo mpana kwa makampuni ya Kiarabu kutekeleza miradi zaidi na kupata ujuzi zaidi.

Mwenyekiti wa Chemba ya Qatat Sheikh Khalifa bin Jassim Al Thani aliongoza wajumbe wa baraza hilo walioshiriki katika mkutano huo ambao uligusia mada nyingi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwekezaji wa pamoja kati ya nchi za Kiarabu na vikwazo vinavyokabili biashara ya ndani ya nchi za Kiarabu, pamoja na kuimarika kwa biashara ya kimataifa na fursa zinazopatikana kwa uchumi wa Kiarabu.

Wakati wa mkutano huo, wakuu wa Qatar walipongezwa kwa mashindano hayo, na kuhakikishia kuwa ni ubingwa kwa Waarabu wote na kwamba faida zake za kiuchumi zitazidi matarajio yote.

Taarifa hiyo pia imezitaka serikali za nchi za Kiarabu kufikia nguzo nne za uhuru unaoimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa Waarabu, ambao ni uhuru wa mtu mmoja mmoja kusafiri, uhuru wa mtaji, uhuru wa usafirishaji wa bidhaa, pamoja na uhuru wa kuhamisha huduma kwa kuongeza kasi.

Sambamba na kupitishwa kwa Mkataba wa Uwekaji huria wa Biashara katika Huduma miongoni mwa nchi za Kiarabu.

Pia kuanzishwa kwa minyororo ya thamani na ugavi katika bidhaa zinazozalishwa na Waarabu kupitia bandari na vituo vya usafirishaji, na kutoa usaidizi kwa usafiri wa njia nyinginezo, pamoja na uanzishwaji wa kubadilishana bidhaa za Waarabu yalikuwa miongoni mwa mapendekezo.

Mkutano huo pia ulisisitiza juu ya kuhimiza sekta binafsi kutekeleza wajibu wake wa kijamii katika kuendeleza na kusaidia elimu, mafunzo, na ujasiriamali ili kujenga vizazi vyenye tija vinavyoendana na maendeleo, kwa kuzingatia vijana wajasiriamali.

Pia jumuiya hiyo ilitoa wito wa kuwezesha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, kuwezesha sekta za umma na binafsi kujumuishwa katika sekta zote za kiuchumi, na kuamsha jukumu la benki na kufadhili maendeleo ya Waarabu katika kusaidia uwekezaji.(Mashirika)

Post a Comment

0 Comments