BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 60

NA WILLIAM BOMBOM

Mkutano mkubwa wa kichawi ulifanyika pale GAMBOSHI MPYA, wachawi wa kambi yote walihudhuria katika mkutano huo.

Agenda kuu katika mkutano huo ilikuwa ni kupanga namna ya kujaza misukule katika kambi nzima. Misukule ndiyo malighafi muhimu katika kambi za kichawi, misukule hao ndiyo hufanya shughuli zote za kambi.

Haijalishi misukule hao watakuwa na umri mkubwa kiasi gani, hufanya kazi kwa maelekezo toka kwa viongozi wao. Hapa niseme kidogo, umri wa maisha ya binadamu wa kawaida na umri wa misukule ni tofauti kabisa.

Misukule huishi miaka mingi zaidi ya maisha ya binadamu wa kawaida. Ni jambo la kawaida kwa msukule kuishi miaka mia tatu, wapo ambao huishi zaidi ya hapo.

Ni rahisi kwa msukule kulithishwa vizazi zaidi ya kumi yaani mzazi, mtoto, mjukuu, kitukuu, kilembwe, kilembwekezi, kinying'inya, kinying'inyiza na wengineo.

Wakati huo msukule huyo ni mzima kabisa huku wamiliki wake wanazeeka na kufa, wanamchukua wamiliki wapya nao wanazeeka na kufa huku yeye msukule akiendelea kuishi.

Kikao kilihudhuriwa na wachawi wa kambi yetu pekee, hakuna mtu mwingine aliyeruhusiwa kukanyaga kwenye kikao hicho.

Wajumbe wa kikao walitoa ushauri wao wa namna ya kuijaza kambi hiyo, ukubwa wa kambi hutegemea idadi ya wachawi, majengo ya kambi pamoja na idadi kubwa ya misukule.

Kwa upande wetu tulikuwa tumepungukiwa idadi ya misukule. Wajumbe walikuwa wakiendelea kuchangia mawazo yao ya namna njema ya kuijaza kambi hiyo.

Wapo walioshauri tuzalishe ugonjwa wa mlipuko ndani ya jamii, hapa walikuwa wamelenga kipindupindu ambacho kinapotokea huchukua idadi kubwa ya watu kwa muda mfupi.

Ugonjwa huu huwa tunatafuta sehemu ambapo jamii kubwa inapategemea kwa huduma, mfano vyanzo vya maji vinavyohudumia jamii kubwa.

Kule huwa tunamwaga madawa kisha kunanuia idadi ya watu wanaohitajika kuuawa. Kama kisima hicho tumenuia watu hamsini huwa tunahamia kisima kingine mpaka itimie idadi ya watu wanaohitajika.

Muda mwingine tunaweza kumwaga madawa kwa wapishi wa maeneo wanakokula idadi kubwa ya jamii, mfano mahotelini, magengeni pamoja na mashuleni kwa mama ntilie.

Baadhi ya wachawi waliikataa njia hii kwani huleta taharuki kwa jamii nzima, wachawi hao wakashauri tutumie njia nyingine.

Mchawi mmoja alishauri kuwa, ni vyema misukule tutakaowapata wasiwe wa eneo moja. Yeye alisema tutengeneze ajali kwenye vyombo vikubwa vya umma, alipendekeza kuwa vyombo hivyo viwe ni vile vinavyobeba idadi kubwa ya watu.

Alitolea mfano wa treni, meli, ndege au mabasi, hivyo ingekuwa rahisi kupata misukule wengi kwa mpigo. Idadi kubwa ya wachawi waliunga mkono ushauri huu japo waliomba tuendelee na njia zingine.

Mchawi mmoja alipopata nafasi ya kushauri yeye alisema, njia ya ajali siyo rafiki maana tungeweza kushindwa endapo kwenye vyombo hivyo wapo waganga wakubwa.

Yeye alishauri tutengeneze ajali, lakini ajali hiyo ijikite kwenye miti, majumba ambayo yanaweza kudondoka kupitia upepo ama mvua tutakayoileta wenyewe.

Aliendelea kusema endapo tutazalisha upepo wa ajabu ajabu eneo la soko, kisha ukaezua vibanda na majengo yaliyoko maeneo hiyo ni rahisi kuwachukua walengwa wetu.

Kupitia upepo huo watu watakatwa na mabati, wataangukiwa na majengo, paa, ukuta au mbao. Hii ingekuwa njia rahisi zaidi, maana idadi ya watu waliokuwa wakihitajika katika kambi hiyo ni elfu mbili mia mbili ishirini na mbili.

Endapo ajali hiyo ingetokea soko la majengo, kisha tukapitia majengo ya shule za msingi Majengo na shule ya msingi Magufuli idadi ingekamilika.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kuna muda hutokea kimbunga cha ajabu ajabu na kupelekea maafa makubwa. Vimbunga hivi huwa vya aina mbili, vipo ambavyo huwa ni majanga ya asili huku vingine huwa vinasababishwa na sisi.

Katika majanga ya namna hii hasa yale ya kutengenezwa na sisi huwa yanapukutisha roho za watu wengi. Jamii humsingizia Mungu huku ukweli ukibaki palepale, kuwa siyo Mungu bali ni sisi tumesababisha matukio hayo. Baadhi ya wachawi walikubaliana na wazo hilo lakini waliruhusu kikao kuchangia mawazo zaidi.

Mchawi mmoja alipewa nafasi ya kuzungumza, yeye alishauri kuwa tusipoteze muda wa kutengeneza ajali na vitu vingine.

Njia nzuri tungetegesha kwenye mikutano mikubwa ya siasa, maadamu mbunge wa jimbo husika atakuwa na kikao na wananchi tungetumia mwanya huo.

Tuzalishe kimbunga cha ajabu katika mkutano wake, hapa ndipo tutaweza kuchukua watu wengi maana mkutano wake huhudhuriwa na watu zaidi ya elfu kumi.

Hoja hii iliungwa mkono na baadhi ya wachawi, lakini wengine walipinga maana ingeleta taharuki ndani ya jamii husika.

Mchawi mwingine alisimama na kusema, mawazo yote yaliyochangiwa na wajumbe waliopita yalikuwa mazuri. Lakini yeye alitaka kushauri tofauti na mawazo hayo.

Katika ushauri wake alisema kuwa, yeye hakuona faida ya kutumia njia zote zilizotajwa na wajumbe waliopita. Njia ambayo tunapaswa kuitumia kuwapata misukule hao, ni vyema isilete taharuki ndani ya jamii.

Njia hiyo ingeleta pia heshima kwa kambi, hivyo yeye alishauri kuwavamia wachawi wa kambi ndogondogo. Kitendo hicho kingeleta heshima kwa kambi yetu, pia kingesababisha kuondoa kambi zingine za kichawi ukanda wa ziwa magharibi.

Wachawi hao tungewapora misukule wao kisha kusambaratisha kambi zote hatarishi kwa kambi yetu. Wazo hili lilikubalika kwa wachawi wengi, wakaona ni vyema wazo hilo ndilo lifanyiwe kazi.

Kwa pamoja tukaamua kuorodhesha kambi zote ndogo ndogo za kichawi, ili kupangilia tungeanza na kambi ipi na kumalizia kambi ipi. Baada ya hapo tulisambaa na kuelekea kwenye shughuli zetu.

Katika kuorodhesha kambi hizo tulifanikiwa kupata kambi saba, kambi hizo ni pamoja na ile ya Kaguruka, Mtegowanoti, Kamfuba, Mganza, Itebula, chagu na Mlyabibi ambayo ilikuwa ni kambi iliyoanzishwa na mama yangu. Kambi hii aliianzisha yeye na washirika wake baada ya kuiteketeza ile kambi yao ya Malagarasi darajani.

Kabla ya kushambulia kambi hizo nilipata muda wa kubadilishana mawazo na BUNDI WA GAMBOSHI kuhusiana na mpango huu.

Yeye alishauri kuwaitisha viongozi wa kambi hizo mmoja baada ya mwingine kisha niwaeleze kujiunga na kambi yetu ya GAMBOSHI MPYA.

Kwa kiongozi atakayegoma kuungana na kambi yetu, basi kusingekuwa na njia nyingine zaidi ya kumshambulia. Mawazo haya yalikuwa mazuri japo yangekuwa na ugumu, maana kumnyang'anya mtu madalaka pamoja na misukule yake kisha aje kujiunga na kambi yenu ni suala gumu.

Hatimaye siku ikawadia, badala ya kuwaita viongozi wa kambi hiyo niliamua kuwatembelea mwenyewe kwenye kambi zao.

Katika safari hiyo niliambatana na wasaidizi wangu wawili pamoja na BUNDI WA GAMBOSHI. Kwa mara ya kwanza wasaidizi wangu wa kichawi wakawa wamepata bahati ya kupanda usafiri wa BUNDI WA GAMBOSHI.

Huu ulikuwa ni usafiri maalumu kwa mkuu wa kambi pekee, ulitumika maalumu kwenye safari muhimu na zenye tija kwa kambi.

BUNDI WA GAMBOSHI ni usafiri ambao uliletwa na mkuu wa giza ili utumike katika matukio muhimu na safari kubwa kama za kwenda makao makuu ya mkuu wa giza kwenye mji wa heaven na safari kama hii niliyoiratibu.

Siku hiyo tulijiandaa mapema kwa safari yetu, tuliamua kuanzia kambi ndogo ya kichawi ya mji wa Chagu. Tayari tulikuwa tulishafanya uchunguzi mapema na kubaini siku hiyo mkuu wa kambi hiyo angekuwepo.

Tulipanda kwenye usafiri wetu wa BUNDI WA GAMBOSHI hao tukaelekea mji wa Chagu. Kutoka kambini kwetu kwenda mji wa huo ni kilometa 38, tulitumia dakika tatu kutua eneo la kambi hiyo.

Hapa niseme kidogo, katika usafiri wote wa kichawi huu ndiyo ulikuwa ni usafiri wa kasi kuliko usafiri wowote. Ni usafiri wa kasi ya kufumba na kufumbua, kasi hiyo inazidiwa kidogo sana na kasi ya mwanga ambayo ndiyo huongoza.

Tulishuka kwenye viunga vya kambi hiyo tukakutana na moto uliokuwa ukiwaka kuzunguka kambi hiyo. Kumbe umdhaniaye ndiye kumbe siye, kambi hii tuliichukulia ya kawaida sana...

Ndugu msomaji unadhani nini kitawapata THE BOMBOM na wasaidizi wake katika kambi hiyo? Endelea kuungana nami katika muendelezo wa simu lizi hii.

TULASOHOYE
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news