Haya hapa Matokeo ya Darasa la Saba 2022, NECTA yafungia na kufuta Mwanza kinara

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya darasa la saba ya 2022 huku likisema watahiniwa zaidi ya milioni 1.07 kati ya milioni 1.34 wenye matokeo sawa na asilimia 79.62 wamefaulu kwa kupata madaraja A na B na C.
Aidha, kati ya hao wasichana ni 558,825 ambao ni sawa na asilimia 78.91 na wavulana ni 514,577 sawa na asilimia 80.41.

Athumani Amasi ambaye ni Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA ametangaza matokeo hayo leo Desemba Mosi, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika Oktoba 5 na 6, 2022.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo amesema,katika matokeo ya mwaka 2021 watahiniwa walikuwa 907,802 sawa na asilimia 81.97.

Pia amesema, kitakwimu kuna kupungua kwa ufaulu kwa asilimia 2.35 ingawa idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa watahiniwa 165, 600 sawa na asilimia 18.24 ikilinganishwa na mwaka jana.

Wakati huo huo, watahiniwa 2,194 wamefutiwa kabisa matokeo yao na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kwa udanganyifu.

“Baraza la mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 2,194, sawa na asilimia 0.16 ya watahiniwa milioni 1.3, baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022, ” amesema Amas.

Aidha, idadi hiyo ya waliofutiwa matokeo ni kubwa zaidi ya watahiniwa 393 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2021.

Oktoba 25, mwaka huu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda aliagiza kufungwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary iliyopo mkoani Pwani kuwa kituo cha mtihani kwa muda usiojulikana baada ya kubainika kufanya ufanganyifu kwenye mtihani wa darasa la saba.

Huku hayo yakijiri, mwanafunzi wa shule hiyo, Iptisum Slim ambaye aliyebadilishiwa namba ya mtihani wa darasa la saba amefaulu kwa wastani wa juu.

Oktoba 14,2022 ilisambaa video inayomuonesha mtoto Slim akiomba msaada kwa Serikali akihofia kupoteza haki yake ya kusoma, baada ya kupewa namba 39 ya mwintimu mwingine badala ya namba yake halali 40 ambayo alipaswa kuketi.

Kupitia matokeo ya NECTA leo yameonesha, mtoto Slim amefaulu kwa wastani wa A, kwa kupata alama A katika masomo manne na B katika masomo mawili.

Miongoni mwa masomo aliyopata A ni Kiswahili, Kiingereza, Maarifa na Sayansi huku aliyopata B ikiwa ni Hisabati na Uraia ambapo hiyo ni ishara njema katika safari yake ya masomo.

Wakati huo huo, NECTA imezifungia shule 24 kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Shule hizo ambazo ni sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mitihani nchini, ni pamoja na shule ya msingi Kadama iliyopo Chato- Geita, Rweikiza iliyopo (Bukoba), Shule ya msingi Kilimanjaro iliyopo (Arusha), Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), pamoja na Al-hikma ya mkoani Dar es Salaam.

Shule nyingine ni Kazoba iliyopo mkoani Kagera, Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (Kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani), Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza), St Severine (Kagera) na Shule ya Msingi St Anne Marie ya Dar es Salaam.

“Vituo hivi vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” amesema Amas.

Kupitia orodha hiyo, Mkoa wa Mwanza ndiyo umeongoza kwa kuwa na vituo vingi vya mitihani vilivyofungiwa kwa kuwa na shule tisa.

Wa pili ni Kagera wenye shule tano, Mara (2), Arusha (2), Geita (1), Dar es Salaam (2), Pwani (1), Tanga (1) na mkoa wa Songwe ukiwa na shule moja.

Mbali na hayo, matokeo hayo yameonesha kuwa, asilimia 67.71 ya watahiniwa wote katika mtihani huo walipata daraja D katika somo la Kiingereza.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa 912,708 walipata ufaulu wa daraja hilo huku wengine 39,086 wakipata daraja E ambao ni sawa na asilimia 2.90.

“Katika somo la English language jumla ya watahiniwa 59,990 wamepata daraja A (utepe wa kijani daraja la kwanza), watahiniwa 56,569 wamepata daraja B (utepe wa kijani daraja la II) na watahiniwa 279,580 wamepata daraja C.

Hiyo ni tofauti na somo la Kiswahili ambapo ni asilimia 7.74 pekee ya watahiniwa ndiyo waliopata daraja D na asilimia 2.76 wakipata daraja E katika somo hilo.

Aidha, watahiniwa wengi katika somo hilo walikuwa katika daraja B, ambapo 552,404 walikuwa katika kiwango hicho cha ufaulu ikiwa ni sawa na asilimia 40.92, watahiniwa 403,825 sawa na asilimia 29.96 walipata daraja A katika somo hilo huku Kiswahili watahiniwa 250,194 sawa na asilimia 18.56 wakipata daraja C.

NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA

PSLE-2022 EXAMINATION RESULTS. Bonyeza jina la mkoa wako kuangalia matokeo ya shule uliyosoma au aliyosoma mwanao hapa chini;


ARUSHA

DAR ES SALAAM

DODOMA

IRINGA

KAGERA

KIGOMA

KILIMANJARO

LINDI

MARA

MBEYA

MOROGORO

MTWARA

MWANZA

PWANI

RUKWA

RUVUMA

SHINYANGA

SINGIDA

TABORA

TANGA

MANYARA

GEITA

KATAVI

NJOMBE

SIMIYU

SONGWE


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news