Kocha wa Brazil ajiuzulu,nahodha Silva washindwa kujizuia

NA DIRAMAKINI

KOCHA mkuu wa Brazil, Tite amethibitisha kuwa ameacha kazi kufuatia kutolewa katika Robo Fainali ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 nchini Qatar dhidi ya Croatia siku ya Ijumaa.

Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa Dunia, ambao walichukuliwa na wengi kama wangeweza kubeba kombe hilo nchini Qatar wametoka katika hatua ya robo fainali kwa mara ya pili mfululizo ya Kombe la Dunia.

Ni baada ya kufungwa mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Croatia kufuatia sare ya 1-1 katika dakika 120 za soka la nguvu.

Baada ya pande zote mbili kutoka sare ya bila kufungana katika dakika 90, Neymar alifunga bao la kuongoza katikati ya muda wa nyongeza, lakini Selecao hawakuweza kushikilia uongozi wao mwembamba huku Bruno Petkovic akifunga bao la kusawazisha dakika ya 117 na kupeleka pambano hilo kwa mikwaju ya penalti.

Rodrygo na Marquinhos wote walikosa juhudi zao kutoka umbali wa yadi 12, huku Croatia wakifunga mikwaju yao yote minne ya penalti na kujikatia tiketi ya kutinga hatua ya nne bora na kupeleka taifa lililoorodheshwa namba moja duniani kurudi nyumbani wakiwa vichwa chini.

Kabla ya kusafiri kwenda Qatar, Tite alitangaza kwamba atajiuzulu nafasi yake kama kocha bila kujali jinsi Brazil walivyocheza kwenye Kombe la Dunia, na sasa amethibitisha uamuzi wake wa kuondoka baada ya miaka sita kwenye nafasi hiyo yenye joto kali.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi, muda mfupi baada ya kushindwa na Croatia, Tite alisema: "Mzunguko wangu umekwisha. Nilisema zaidi ya mwaka mmoja na nusu uliopita na ninatimiza ahadi yangu.

"Hatupaswi kufanya mchezo wa kuigiza kama nilivyosema mwaka mmoja na nusu uliopita. Kuna wataalamu wengine wakubwa ambao wanaweza kuchukua nafasi yangu. Kunaweza kuwa na vipengele vya kuchambua, lakini mzunguko umekwisha."

Alipoulizwa kuhusu tathimni yake, kwa mrithi ajaye Brazil, kocha huyo mwenye umri wa miaka 61 alijibu: "Muda unaweza kujibu vyema. Maumivu, hata kama ya kibinadamu, yanaendana, nina fahamu ninayoweza kuwa nayo, hisia zinaguswa.

"Sina uwezo wa kutathmini kazi yote iliyofanyika. Baada ya muda mtafanya tathmini hii. Sina uwezo huo sasa baada ya kuondolewa."

Tite alichukua nafasi ya Dunga kama kocha mkuu wa Brazil katika msimu wa joto wa 2016 na akashinda mechi 61 kati ya 81 katika mashindano yote.

Kocha huyo wa zamani wa Corinthians alishinda taji la Copa America 2019 wakati wa ualimu wake kabla ya kufungwa 1-0 katika fainali miaka miwili baadaye na wapinzani wa Amerika Kusini, Argentina.

Aidha, Brazil walitinga hatua ya kufuzu Kombe la Dunia na kujikatia tiketi ya kufuzu Qatar, wakishinda 14 na kutoka sare mechi tatu kati ya 17 za COMNEBOL, lakini kama walivyofanya mwaka 2018, Selecao wameshindwa kutinga nusu fainali kwenye hatua hiyo kubwa ya kimataifa, na kusubiri kwa miaka 20 kuwa mabingwa wa Dunia kwa mara ya sita.

Nahodha Thiago Silva, ambaye anatakiwa kuwafariji baadhi ya wachezaji wenzake kwa wakati wote, ameelezea masikitiko yake baada ya kushindwa na Croatia, lakini amewataka Brazil kusonga mbele kutokana na kuondoka kwao kwa kukatisha tamaa.

"Ni vigumu, lakini hata kama inasikitisha, maisha yanahitaji kusonga mbele, inua kichwa chako," mlinzi huyo wa Chelsea mwenye umri wa miaka 38 aliwaambia wanahabari. "Ninajivunia sana vijana hawa kwa kile tulichofanya, lakini kwa bahati mbaya ni sehemu ya soka.

"Nimepitia hali ya kukatishwa tamaa katika maisha yangu, sio tu katika timu ya taifa, lakini katika maisha yangu ya kibinafsi pia," Silva aliongeza. "Tunapopoteza kitu muhimu ulichonacho kama lengo, inauma...inauma sana, lakini ni kujaribu kuinua kichwa chako na kuendelea.

"Hakuna njia nyingine, mimi ni mtu ambaye kila nilipoanguka nilinuka, haitakuwa wakati huu nibaki hapa, bahati mbaya kama mchezaji sitaweza kuinua kombe hili, ninajua baadaye nina jukumu lingine." 
 
Hata hivyo, wakati ndoto ya Brazil katika Kombe la Dunia nchini Qatar ikizimika ghafla, Croatia itamenyana na Argentina katika nusu fainali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news