MAEMBE USIHARIBU:Kesho yako waipunja

NA LWAGA MWAMBANDE

NENO la Mungu, mathalani kupitia Biblia Takatifu inawashauri vijana kumcha Mungu tangu ujana wao. Ukisoma, Biblia katika kitabu cha Muhubiri 12:1 inasema..,Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya,wala haijakaribia miaka utakaposema,mimi sina furaha katika hiyo.''
Kupitia andiko hilo, neno la Mungu linasisitiza kuwa,ni muhimu sana kwa kijana kumcha Bwana Mungu tangu mapema kabisa katika umri wake, kwa maana kijana asiyezoea kujizuia kimwili kabla ya ndoa, hataweza kujizuia katika ndoa.

Hii inatokana na ukweli kwamba, wasaliti wengi wa ndoa zao ni wale ambao hata kabla ya ndoa walishindwa kujizuia miili yao na kuwapelekea kufanya uasherati.

Rejea, kitabu cha 2 Timotheo 2:22..,Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi."

Ni wazi kwamba,baada ya kijana kumkumbuka Mungu kwa kumpokea Yesu na kuanza kuishi maisha ya wokovu, Biblia inashauri kijana kuanza kuliishi neno la Mungu, kulifanya taa ya miguu neno ili limuongoze katika matendo mema na kumtii Mungu siku zote.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kadri unavyojaribu jaribu na kuwaharibia wenzako maisha ya baadaye, ndivyo hivyo mwisho wako utakuwa wa hovyo hovyo, endelea;

1.Maembe usiharibu,
Kwa kujaribu jaribu,
Uwaache watu bubu,
Mwisho wako ni wa hovyo.

2.Kama ukishavuruga,
Hujui ushajiroga,
Hata maji kuyaoga?
Ndugu usifanye hivyo.

3.Jueni Mungu alivyo,
Hataki mfanye hivyo,
Kwa sababu hivyo sivyo,
Mtabakia wa hovyo,

4.Huko ni kujinajisi,
Na kujiletea mkosi,
Na maisha kuwa hasi,
Msitangetange hovyo.

5.Mabinti wana hisia,
Sidhani wafurahia,
Pabaya mtaishia,
Msitangetange hovyo.

6.Taratibu urafiki,
Chunguza yenye mantiki,
Endapo hauridhiki,
Ondoka vile ulivyo.

7.Urafiki ukitiki,
Mwenzako akiafiki,
Wazazi wakabariki,
Msifanye mambo hovyo.

8.Uchumba ukiingia,
Taratibu malizia,
Na kwenye ndoa ingia,
Msifanye mambo hovyo.

9.Kama unaonjaonja,
Amri unaivunja,
Kesho yako waipunja,
Takuja kuwa wa hovyo.

10.Na mabinti taratibu,
Sivunjevunje kibubu,
Mengi yaweza wasibu,
Muonekane wa hovyo.

11.Kusemeshwa ni halali,
Kukataa kukubali,
Huo kwenu uhalali,
Msinde hovyo hovyo.

12.Wala msidanganyike,
Wavulana wawateke,
Hadi nguo zivulike,
Mahusiano ya hovyo.

13.Wakisema sikiliza,
Mfanye kujiuliza,
Kama yao yakoleza,
Acha mihemko hovyo.

14.Kama mmeshika dini,
Hiyo ikae moyoni,
Hadi afike nyumbani,
Msifanye hovyo hovyo.

15.Kile kinasikitisha,
Mkivuruga maisha,
Mabinti ndiyo mwaisha,
Maamuzi yenu hovyo.

16.Mwacheza wawazalisha,
Kulea wanakausha,
Mnapigika maisha,
Sababu mambo ya hovyo.

17.Mabinti yenu thamani,
Ni sehemu za mwilini,
Zisianikwe juani,
Mwaonekana wa hovyo.

18.Jinsi mnajisetiri,
Mavazi yenu mazuri,
Mahusiano mazuri,
Hamtatumiwa hovyo.

19.Kama mnajianika,
Rahisi kudanganyika,
Ziara zinafanyika,
Mtabakia mlivyo.

20.Dunia meharibika,
Ukweli umekatika,
Lakini wapo wakaka,
Ambao siyo wa hovyo.

21.Hebu kumbuka Eliya,
Kwa jinsi alivyogwaya,
Akasema bila haya,
Moyoni mwake yalivyo.

22.Kwamba eti manabii,
Mungu wanaomtii,
Kabaki yeye nabii,
Wakati sivyo ilivyo.

23.Mungu alichomwambia,
Na kumthibitishia,
Bado katika dunia,
Wapo wasio wa hovyo.

24.Alfu saba manabii,
Mungu bado wamtii,
Iingie kwako hii,
Usifanye mambo hovyo.

25.Wapo wanaume wengi,
Na hata mabinti wengi,
Ambao si wengi wengi,
Kama wafanyao hovyo.

26.Utakiwacho kufanya,
Hiki hasa nakuonya,
Taratibu nzuri fanya,
Usiende hovyohovyo.

27.Hisia ukiumiza,
Mwanamke atawaza,
Hiyo mbele takukwaza,
Uishi maisha hovyo.

28.Vile ulimuahidi,
Mtakula wote idi,
Umefanya ukaidi,
Hutabaki hivyo hivyo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news