Mitandao ya kijamii itumike kuwanasua vijana katika dawa za kulevya-Profesa

NA GODFREY NNKO

PROFESA wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kuwait,Amthal Al-Huwaileh amesema, mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa ya kuwasaidia vijana kujinasua katika uraibu wa dawa za kulevya popote pale duniani.
(Picha na visionsteen).

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na Visions Treatment Centers ilibainisha kuwa, kijana kwa wastani hutumia karibu saa nane kwa siku kwenye simu au kompyuta kuperuzi mitandao ya kijamii.

Huu ni muda mwingi kuliko unaotumiwa kila siku darasani, na mara nyingi muda mwingi kuliko unaotumika kulala. Muda mwingi huu hutumiwa kuingiliana na wengine kupitia mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii inarejelea tovuti na programu zinazoruhusu taarifa kushirikishana kwa haraka, na hadhira pana.

Tovuti maarufu za mitandao ya kijamii zilizo na vijana ni pamoja na Instagram, Snapchat na Twitter. Pia kuna maelezo mengi ambayo yanashirikishwa kupitia machapisho ya video kwenye Youtube, blogu na kwingineko.

Hivyo, kuchapisha taarifa zinazotoa hamasa kwa mambo hasi hasa matumizi ya dawa za kulevya, unaweza kujikuta unawatengenezea vijana mazingira mabaya ambayo yanakatisha ndoto zao.
Amesema, majukwaa mengi ya mitandao ya kijamii yamekuwa na ushawishi wa namna ya kipekee katika kufikisha ujumbe kwa haraka tena kwa kundi kubwa la vijana ambao wamekuwa watumiaji wakubwa wa mitandao hiyo.

"Majukwaa ya mitandao ya kijamii yamekuwa upanga wenye makali ya kukata kuwili, yakitumika vema yana faida kubwa kuokoa vijana katika uraibu wa dawa za kulevya, lakini yakitumika ndivyo sivyo yanaweza kuwa sababu ya vijana wengi kuhamasika kujiingiza katika utumiaji wa dawa hizo.

"Kwa hiyo,majukwaa haya yakiwa yanafanya kazi ipasavyo kwa kutoa elimu ya kuwaondoa vijana katika ulimwengu wa uraibu wa dawa za kulevya, au kuwapa vijana maarifa ya namna ya kujiondoa katika viashiria au tabia za kujihusisha na matumizi ya dawa hizo, tutavishinda vita hivi;

Profesa wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kuwait,Amthal Al-Huwaileh ameyasema hayo katika mahojiano na
Shirika la Habari la Kuwait (KUNA).

Msomi huyo anaamini kuwa, mitandao ya kijamii inaweza kuwa nyenzo muhimu wakati wa kukuza kampeni zinazoongeza ufahamu juu ya hatari za utumiaji wa dawa za kulevya, na kuangazia chaguzi za matibabu kwa wale ambao wameangukia katika utumiaji wa dawa hizo.

Pia alisisitiza zaidi umuhimu wa kutumia majukwaa kuwasiliana na vijana, na kuwahimiza waraibu kutafuta msaada, na kuwahakikishia kuwa hakuna hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Badala yake, amesema, majukwaa hayo yajikite zaidi kuwatia moyo kuwa,wanaweza kusaidiwa kitaaluma na bila kukumbwa na uyanyapaa wa aina yoyote baada ya kujiondoa huko.

Profesa huyo anaamini kuwa,kuna umuhimu mkubwa kwa waendeshaji na wasimamizi wa majukwaa au mitandao hiyo kuchambua na kuangalia aina ya taarifa za kupakia ambazo zinahusu dawa za kulevya ili kuepuka kuwa sehemu ya kuwapa hamasa vijana kujiingiza huko, badala yake wawe sehemu ya kuwatoa katika janga hilo ambalo limeathiri idadi kubwa ya vijana duniani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma katika Chama cha Hilali Nyekundu cha Kuwait, Khaled Al-Zaid, alisema kuwa ingawa kuna mitandao ya kijamii yenye nyenzo muhimu za kielimu zinazoweza kung'arisha ujuzi wa vijana, tovuti nyingine zimekuwa chanzo cha vijana wengi kujitumbukiza katika dawa za kulevya.

Al-Zaid amesema kuwa, ili kuepuka athari mbaya ya jambo hilo, watu wanapaswa kufahamu vyema hatari na athari mbaya za kuitembelea mitandao ambayo imekuwa sehemu ya kushawishi kundi la vijana kujihusisha na dawa za kulevya.

Huku akisisitiza kuwa, wazazi wana nafasi kubwa ya kuhakikisha wanawajengea vijana wao mazingira mazuri ya malezi hususani kuwasisitiza kumtumikia Mungu, kwani kuwa na hofu ya Mungu ni moja wapo ya nguzo muhimu ya kuyashinda maovu ya dunia ikiwemo kujihusisha na mambo ya hovyo kama dawa za kulevya.

Matibabu

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kuna aina mbalimbali za matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya ingawa hakuna tiba moja ambayo inafaa kwa waraibu wote.

Aidha, matibabu ya uraibu wa dawa za kulevya hutofautiana sana kulingana na aina ya dawa husika, kiasi cha dawa kilichotumika, muda wa uraibu, matatizo ya kiafya na mahitaji ya kijamii na mtu binafsi.

DCEA inafafanua kuwa, huduma za tiba ya uraibu zinazotolewa nchini Tanzania ni tiba saidizi kwa waraibu kwa kutumia dawa (Medically Assisted Therapy-MAT),Huduma katika Nyumba za Upataji Nafuu (Sober Houses) na Tiba kwenye vituo vya kutolea Huduma za Afya ya Akili.

Hata hivyo, kuna baadhi ya waraibu wanaopatiwa huduma za unasihi pekee kwenye asasi za kiraia na kuachana na matumizi ya dawa hizo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news