Zambia yakomesha hukumu ya kifo na kashfa ya jinai kwa Rais

NA DIRAMAKINI

JAMHURI ya Zambia siku ya Ijumaa imetangaza kusitisha hukumu ya kifo na kosa la kashfa ambalo lilikuwa jinai nchini humo.

“Leo (Desemba 23, 2022) tumeidhinisha Muswada wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Marekebisho) namba 25 ya 2022, ukifuta hukumu ya kifo nchini Zambia na kosa la Kashfa ya Jinai kwa Rais. Niliahidi kurekebisha sheria zinazozuia demokrasia, haki za binadamu, utawala bora na uhuru wa kimsingi.Ahadi zinatekelezwa,” Rais Hakainde Hichilema alitweet.

Zambia ambayo ni nchi isiyo na bandari ni miongoni mwa mataifa ambayo yanagusa pande nyingi za Afrika ikiwemo Afrika ya Kati, Kusini na Mashariki, ingawa kwa kawaida inajulikana kuwa ipo Kusini mwa Afrika.

Majirani zake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa Kaskazini, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upande wa Kaskazini Mashariki, Malawi kwa upande wa Mashariki, Msumbiji upande wa Kusini Mashariki, Zimbabwe na Botswana upande wa Kusini, Namibia upande wa Kusini Magharibi na Angola upande wa Magharibi.

Mji mkuu wa Zambia ni Lusaka, ulioko Kusini Kati mwa Zambia. Idadi ya wakazi wa taifa hilo inakadiriwa kuwa takribani milioni 19.5.

Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini amesema, uondoaji huo wa adhabu ya kifo ni hatua nzuri na ya kimaendeleo inayoonesha dhamira ya nchi katika kulinda haki ya kuishi.

Kwa hatua hiyo, Zambia inakuwa nchi ya 25 Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika kukomesha hukumu ya kifo kwa makosa yote.

"Pia tunampongeza Rais Hichilema kwa kufuta kosa la jinai la kumkashifu rais, lililotumika hadi hivi karibuni kuzuia uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

"Uamuzi wa Zambia wa kupiga marufuku hukumu ya kifo unapaswa kuwa mfano kwa nchi nyingine katika eneo hilo ambazo bado zinatumia adhabu ya kifo, hivyo kuna umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kukomesha aina hii ya adhabu ya kikatili, ya kinyama na ya kudhalilisha na kulinda haki ya kuishi,"Chagutah aliongeza.

Wakati huo huo, Amnesty International pia imehimiza Zambia kukubaliana kwa haraka na Itifaki ya Pili ya Hiari ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, unaolenga kukomesha hukumu ya kifo.

Amnesty International katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu utekelezaji wa hukumu ya kifo, iliandika kwamba matukio ya unyongaji Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika uliongezeka zaidi ya mara mbili kutoka watu 16 mwaka 2020 hadi 33 mwaka 2021.

Kuhusu Hakainde

Hakainde Hichilema aliyezaliwa tarehe 4 Juni, 1962 ni mfanyabiashara, mkulima na mwanasiasa wa Zambia ambaye ni rais wa saba na wa sasa wa Zambia tangu Agosti 24, 2021.

Baada ya kushiriki katika chaguzi tano zilizopita mnamo 2006, 2008, 2011, 2015 na 2016, alishinda uchaguzi wa urais wa 2021 kwa zaidi ya asilimia 59 ya kura huku akiahidi kufanya mageuzi makubwa katika upande wa uhuru wa kujieleza, demokrasia, haki za binadamu na mengineyo.

Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND) alimshinda Edgar Lungu kutoka katika Chama cha Patriotic Front (PF) ambaye aliridhia matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 na hivyo kumaliza rasmi muda wake wa uongozi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news