MWAKA THEMANINI NA TANO

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWAKA 1985 walifika nyumbani kwetu Waingereza wawili, kwa kuwa kimombo changu kilikuwa cha Mr & Mrs Daudi mambo yalikuwa magumu sana katika ugeni huo.
Mimi nilikuwa miongoni mwa watoto wadogo wanne wa kiume, wageni hao wakaniuliza una miaka mingapi, mimi nikawajibu nina miaka 100. Waingereza hao walicheka sana, mama Mwingereza akasema kweli wewe ni mzee, wewe ni babu, nikasema ndiyo.

Mama yangu akawaambia hawa wazungu kuwa huyu ni mwanangu ana miaka kumi tu. Mimi nikajibu nilidhani wananiuliza kama ninaweza kuhesabu mpaka ngapi kwa kimombo ? Wakacheka sana mara zikanunuliwa Orange Skwashi na biskuti tukagawana alafu zikapigwa picha nyingi sana mojawapo ni hiyo hapo juu.

Hawa wazungu mtu na mkewe walikuwa karibu sana na mama kupitia kwa kaka yake yaani mjomba wangu, Novemba 29, 2022 mama huyu akanikumbuka bali mumewe alifariki, tukazungumza kwa kirefu sana mambo mengi.

Alianza kwa kusema mwanagu mzima? Leo nimekumbuka sana, akaniuliza tena mwanangu mzima ? Nikamjibu ninacheka, mimi mzima. “Leo nilikuwa natazama picha za zamani kumbukumbu na yale majibu yako ya miaka 100 imenijia, sasa mwanangu una miaka mingapi?” Nikautaja umri wangu, akacheka sana,

“Nimetazama picha nyingi wengi wamefariki, hata hiyo miaka yako 100 uliotaja wakati ule hawajafikisha na mie ndiyo kwanza nina miaka 69".

Nikampa heko kwa umri huo.Akaniulizia wakati Mwalimu Dorith anazikwa wewe ulkuwa wapi? Maana sikukuona msibani, nikamjibu kwanza nilikuwa nafanya kazi huko Kasulu Kigoma nakumbuka nikapata pesa kiasi, nikachukua shilingi 18,000 nikamnunulia Batiki, nikamtumia kupitia kijana mmoja aliyekuwa anafanya biashara ya Dar es Salaam-Kasulu na kuupeleka Shule ya Msingi Kisarawe-Kariakoo, Ilala Dar es Salaam.

Ndani ya huo mzigo niliweka bahasha yenye barua na ndani yake niliweka shilingi 20,000. Kwa bahati mbaya niliyemtuma alimkosa mwalimu huyo.

Nikamwambia Mungu bahati walimu wanapendana sana, mfanyabiashara huyu akaambiwa mwalimu huyo ni mgonjwa na hajarudi likizo.

Mwanakwetu walimu wanapendana sasa sana akaambiwa mzigo huo apatiwe Mwalimu Catherine (Huyu ni mwalimu wangu wa Somo la Kiswahili Darasa la Tatu Shule ya Msingi Mkuranga Pwani.)

Mwalimu Catherine akamtumia mzigo wake Mwalimu Dorith huko Manyoni kwa basi na bila ya kuifungua ile bahasha na tena akitumia pesa yake mwenyewe kutuma mzigo huo.

Mwanakwetu narudia tena kusema walimu wanapendana sana. Kama ndugu yangu unasoma matini haya unataka kuoa au kuolewa katika machaguo yako yupo mwalimu nakwambia mchangamkie mwalimu.

Mimi nilipoutuma ule mzigo tu nikajiunga na Chuo cha Ualimu Kasulu kusoma Stashahada ya Ualimu, wala majibu kama ule mzigo uliokuwa na thamani shilingi 40,000 kama umefika au la sikuwa nayo, kwa hoja mbili niliyemtuma alikuwa mseminari wa zamani na Kiongozi Kanisa Katoliki Parokia ya Makere Jimbo Katoliki la Kigoma.

Nikiwa chuoni hapo siku moja nikaitwa, nikiambiwa nina mgeni getini, ndugu huyu aliyeniita nikamuliza huyo mgeni anatoka wapi? Nikajibiwa yupo mgeni wewe nenda kamsikilize.

Nikatoka zangu na mabuti kwani nilikuwa zamu katika banda la ng’ombe la chuo, nikaulizwa haya ndugu wewe ndiyo fulani bini fulani nikajibu naam!. Akaniuliza unamfahamu Bernad Mlemeta nikamjibu ndiyo-huyo ni mjomba wangu kabisa tena ni mjomba rafiki.

Unamfahamu Mwalimu Dorith Mlemeta nikajibu ndiyo huyu ni mama yangu mzazi. Unazo taarifa zake zozote? Nikajibu natambua yupo kazini Dar es Salaam.

“Sisi tunatokea Kanisa la Wasabato Kasulu Mjini tuna Radio Call, tumepigiwa na Wasabato wenzetu wa Manyoni Mjini tukujulishe kuwa Manyoni kuna msiba, nadhani mama yako alikuwa mgonjwa? Nenda msibani haraka, Je nauli unayo.” Nikajibu nauli ninayo.

Lo salalee nikatoka zangu nikaenda benki ya kitabu nikatoa pesa na kuanza safari ya Kigoma, alafu Kigoma -Manyoni kwa treni, nilifika Manyoni saa 12.00 watu wanatoka kuzika.

Watu wengi waliokuwa na haraka ya kuondoka msibani sikuwaona, akiwamo mama huyu Mwingereza ninayemsimulia maana alielekea Arusha alafu akaenda zake Ughaibuni.

Nilikaa Manyoni kuona kaburi na kusali kwa siku kadhaa na kurudi Chuoni Kasulu. Niliporudi chuoni nilikutana na fedha ya rambirambi kutoka kwa serikali ya wanachuo nikakabidhiwa kama shilingi 19,650. Nilipewa na mtu anayefahamika kama Manyota Severino akiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanachuo wakati huo.
Nilichobaini nilipoondoka kwenda kuzika wanachuo wezangu walianza michango, nilikaa chuoni kama wiki hivi kuna mwanachuo mmoja wa msichana anaitwa Pendo Haule akaniambia ana shida ya kuzungumza na mimi baada ya masomo.

Muda ulipofika akafika sehemu moja palipokuwa na duka la chuo akanisalimu na kuniambia,“Mimi nimekuja kukupa pole ya msiba na wakati michango inachanghwa sikuwa na pesa na ndiyo maana leo nimekuja mwenyewe, pole yangu hii hapa shilingi 5000.”. Nikapokea na kuagana naye.

Kumbuka haya maelezo namueleza mama yangu huyu, nikamwambia leo umenikumbusha na mimi mambo mengi ya mwaka 1985 na mwaka 2000 , mama huyu akaniambia kuwa hata yeye leo amekuwa na huzuni kubwa akiyakumbuka maisha ya zamani, ndugu na jamaa aliyokuwa nao wengi wamefariki.“Jamani tukiwapigia simu mpokee, msione tunawasumbua.” Alisema,

Mwanangu kuzaliwa na pale unapoishi ni sawa na kuandika kitabu tu, siku unakufa ndiyo kitabu chako kinafungwa paaa ! Unapofariki duniani anayetaka kukisoma kitabu chako anakisoma vizuri sana.

Kiwiliwili ndiyo kinazikwa kaburini kitabu kinabaki. Sasa mwanangu ile miaka 100 ya 1985 hicho kitabu kinakuwa na mambo mengi. Nikamjibu hapo unatakiwa kuwa na volume I-X,akasema hiyo mwanangu ni Encylopedia.

“Kifo kinatutenganisha na watu tunaowapenda na hata wale tunaowachukia na mara nyingi kifo kinatazamwa katika mitazamo mibaya tuu lakini nakwambia msiba ni baraka kama ilivyo kuzaliwa. Aliyefariki kama alikuwa mwema anapata uzima wa milele. Kwa sasa dunia imeendelea kitekinolojia unaumwa unapata matibabu na kila unapotibiwa unaongeza siku za kuishi lakini mwisho upo.”

Akasema sasa ebu mkumbuke yule mseminari uliyemtuma mzigo, wakumbuke wale walimu wa Shule ya Msingi Kisarawe akiwamo Mwalimu Catherine, wakumbuke wale Wasabato wa Manyoni na Kasulu Mjini, wakumbuke wale Wanachuo wa Chuo cha Ualimu Kasulu mkumbuke yule mwanafunzi Pendo Haule, Mwanagu hawa wote walisambaza upendo.

“Tena wajomba walikuwa Waanglikana na mimi Mkatoliki,Wasabato walitufanyia hisani ya simu yao ya upepo na kufunga safari hadi nilipokuwapo.”Nilimwambia mama yangu huyu.

Mama yangu huyu akaniuliza kama ninamfahamu mchoraji wa picha wa Kiitaliano Pedro Subecaseaus? Nikamjibu hapana, akasema huyu ndugu alizaliwa mwaka 1880 na kufariki 1956 huyu alikuwa mchoraji mahiri sana, aliwahi kuchora picha ya huzuni juu ya kifo cha Mtakatifu Frasisko wa Assisi.

Je, Mtakatifu huyu unamfahamu ? Nikamwambia kiasi kidogo namfahamu.“Huyu Pedro Subecaseaus alichora picha ya taswira wakati wa msiba wa Mtakatifu Fransisko wa Assisi- mwili wake uliwekwa katika kijibanda kidogo kando ya Kanisa alilolijenga akiwa hai, mchoro huo unawaonesha wenzake kadhaa wakisikitika mno kutokana na msiba huo, kwani si kwamba tu alikuwa mwanajumuiya mwezao bali alikuwa mtu mwenye mchango wenye manufaa kwa wenzake na jamii yake.”

Mwanakwetu simu yangu ikawa inatoa mlio wa chaji kwisha nikamjulisha mama yangu huyu, akasema haya mwanangu na mimi nikasema kwaheri mama.

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news