Rais Alhaj Dkt.Mwinyi:Serikali imedhamiria kufikisha maendeleo kila eneo na hatutaki kuona dhuluma katika jamii

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Zanzibar itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake na kuwafikishia maendeleo ya haraka kwa kadri ya hali ya kiuchumi itakavyoruhusu katika kufanikisha malengo iliyojiwekea huku akikemea dhuluma miongoni mwa jamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) pamoja na viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu wakiitikia dua iliyosomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi (wa pili kushoto) mara baada kujumuika katika sala ya Ijumaa katika Masjid Al Swafaa iliyopo Gongoni Wilaya ya Mjini, Mkoa Mjini Magharibi leo.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 30, 2022 wakati akizungumza na wananchi na waumini aliojumuika nao pamoja wakati wa sala ya Ijumaa huko Masjid Al Swafaa, Kikwajuni - Gongoni, Shehia ya Kisima majongoo, Wilaya ya mjini Unguja.

Pia Mheshimiwa Rais amesema, tatizo la mtaro linalowakabili wananchi wa eneo hilo ambalo limekuwa kero kubwa kwao, Serikali italitatua kwa haraka ili kuwapa wepesi wananchi wake wa kuendelea na masuala ya msingi ya ujenzi wa nchi na maendeleo kwa ujumla.
Sambamba na hilo, Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwasihi wazazi, walezi, wazee, masheikh pamoja na viongozi wa eneo hilo kujenga jamii yenye maadili na iliyoshiba imani na hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu, ili kupata jamii bora na yenye heshima na mapenzi kwa taifa lao.

Amesema, jamii inayojengwa kimaadili ndio ufumbuzi mkubwa zaidi ili kupata vijana wenye imani, weledi na nidhamu ya uzalendo kwa taifa lao.

Pia amewasihi vijana na waumini kwenye msikiti huo kusameheana kwa waliokoseana kwa namna yoyote ya maisha yao.Aidha, amewataka kutubu na kurejesha kwa walivyowachukuliwa wenzao ili kujenga jamii yenye maadili na imani ya vitendo.

"Vijana watambue kwamba kudhulumu ni jambo baya sana, yako mambo tutamkosea Mwenyezi Mungu moja kwa moja tutubieni, lakini yale tunayowakosea, binadamu wenzetu, tuwatake msamaha, kama kuna chao tumechukua turudishe, kisha tutubie,"amesema Rais Alhaj Dkt.Mwinyi.

Katika hatua nyingine Alhaj Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi hao kwamba serikali yao bado inapambana na kukabiliana na wanaofanya dhuluma na kuwadhulumu wenzao na kwamba serikali itawachukulia hatua na kuwawajibisha.

Hivyo, amewataka wananchi hao kupunguza matatizo katika jamii yanayotokana na masuala ya dhuluma.
"Huku kwingine tuachieni tutaendelea kupambana, kupambana kwa maana ya wale wanaofanya dhuluma, tukigundua tunawachukulia hatua, lakini dhuluma zimeshakuwa nyingi na nyngine za muda mrefu, yapo masuala ya nyumba, migogoro ya viwanja, Serikali inayatambua hayo,"amesema Rais Alhaj Dkt.Mwinyi.

Naye Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume amewasihi waumini wa dini ya Kiislamu na kuwashauri kutofungamana na haki za watu, badala yake kurejesha dhuluma wanazodhulumiana na kudumu kwenye istighfari ili kumcha Mwenyezi Mungu kiukweli.

Aidha, amewataka waumini hao kuwa na mipaka katika kuchukua haki za watu, sambamba na kuwataka wajitathmini kwa matendo waliyofanya mwaka 2022 kwa kuukaribisha vyema mwaka 2023 kwa kumcha Allah (S.W) kwa dhati ya nafsi zao.

Omar Abdi Abdalla, Khatib wa msikiti wa Masjid Al Swafaa wa Gongoni, alisema dini ya Kiislaam imeweka mwongozo mzuri kwa waumini wake kufanya toba ili kutubia makosa waliomkosea Mwenyezi Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Msikiti wa Masid Al Swafaa uliopo Gongoni, Kikwajuni, Ali Salum Mkweche alisema,wananchi wa eneo hilo wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane na kwamba maendeleo anayofanya Rais Dkt.Mwinyi ni makubwa na ya kupigiwa mfano kwani kipindi kifupi cha uongozi wake wameshuhudia maendeleo makubwa katika sekta zote za Elimu, Afya na Maji safi na salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news