Rais Dkt.Samia aelekeza milioni 960/- za Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru kujenga mabweni shuleni

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene amesema, fedha zilizokuwa zimetengwa na wizara na taasisi kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru mwaka huu zitapelekwe Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na kutumika kujenga mabweni katika shule nane za msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum hapa nchini.
Mheshimiwa Waziri Simbachawene ameyasema hayo leo Desemba 5, 2022 wakati akitoa taarifa hiyo na katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma.

“Shilingi milioni 960 zitatumika kujenga shule ya msingi Buhangija Shinyanga, Goweko Tabora, Darajani Singida, Mtanga Lindi, Songambele Lindi, Msanzi Rukwa, Idofi Njombe, na Longido Arusha,”amesema Waziri Simbachawene.

Pia amesema, ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ya kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini. "Hili ni jambo kubwa la kishujaa na la kupongezwa sana na wananchi wote wa Tanzania,"amesema.
Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu 2022 yatafanyika kwa Midahalo na Makongamano mbalimbali yatakayofanyika katika wilaya zote hapa nchini kujadili, kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulikotoka, tulipo na tunakoelekea kuhusu Maendeleo Endelevu ambayo Nchi yetu Tanzania imeyafikia. "Hivyo hakutakuwa na gwaride na shughuli nyingine za Kitaifa,"Waziri amesema, Maadhimisho ya MIAKA 61 YA UHURU yataadhimishwa kwa Kauli mbiu inayosema “AMANI NA UMOJA NI NGUZO YA MAENDELEO YETU”.

“Makongamano hayo yatatanguliwa na ratiba mbalimbali kwa viongozi wa Mikoa na Wilaya kufanya shughuli za kijamii kama vile kufanya usafi katika maeneo ya hospitali, shule, nyumba za Wazee na makundi yenye mahitaji maalum,”ameongeza.
Waziri ameelekeza ofisi zote za Serikali hapa nchini kupambwa kwa mapambo ya rangi za bendera ya Taifa pamoja na picha ya Mheshimiwa Rais.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news