Rais Dkt.Samia afunga njia ya kuchepusha maji na kuanza ujazaji wa maji Bwawa la JNHPP 

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia shughuli ya kufunga njia, kuchepusha maji na kuanza ujazaji maji kwenye Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria hatua ya kufunga njia ya kuchepusha maji na kuanza ujazaji wa maji kwenye Bwawa la Kuzalisha Umeme (Megawati 2115) la Julius Nyerere JNHPP kwenye Mto Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Desemba, 2022.(Picha na Ikulu).

Mradi huo ulianza mwaka 2018 baada ya Serikali ya Tanzania kupata Kandarasi ya ujenzi ubia wa kampuni ya Arab Contractors na El-Sewedy kutoka Misri.

Rais Dkt.Samia amesema, mradi huo ni mojawapo ya miradi mikubwa ya umeme barani Afrika ambapo bwawa hilo litaweza kuweka akiba kubwa ya maji na kuzalisha umeme hata mvua inapopungua.

Pia Rais Samia amesema mbali na kusaidia kudhibiti mafuriko ya mara kwa mara ya mto Rufiji bwawa hili litawezesha kilimo cha uhakika cha umwagiliaji.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameagiza Wakuu wa Mikoa kuwazuia wananchi wanaochepusha maji katika maeneo mbalimbali hasa katika Bonde la Mto Rufiji na kurejesha maji katika mikondo yake ya asili kwa kuzingatia kanuni za mgawanyo wa maji.

Vile vile Rais Samia amezitaka Wizara husika kutokutoa vibali vya matumizi ya maji na uwekezaji kwenye shughuli za uzalishaji unaohitaji maji mengi katika maeneo ya juu ya bonde (upstream) na badala yake utumike uwanda wa chini wa mradi.

Kukamilika kwa Mradi wa JNHPP ambao umefikia asilimia 78.68 kutaimarisha na kufungua fursa nyingi za utalii katika eneo la kusini mwa Tanzania hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na hivyo kutoa ajira kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news