Rais Dkt.Samia apeleka tabasamu Kituo cha Nyumba Salama Butiama na Hope Mugumu Nyumba Salama

NA FRESHA KINASA

KATIKA kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa misaada ya vyakula katika Kituo cha Nyumba Salama Butiama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama na Hope Mugumu Nyumba Salama katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Misaada hiyo ni pamoja na mafuta ya kupikia, unga wa ngano, sukari, kitoweo cha mbuzi, vinywaji (soda), mchele na sabuni ambavyo vimetolewa katika vituo hivyo. Ambavyo hutoa hifadhi kwa wasichana hao kufuatia kukimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketajii na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao.

Vituo hivyo, vinamilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly ambapo vimekuwa vikitoa hifadhi kwa wasichana hao wakiendelezwa katika masomo yao pamoja na mafunzo ya fani mbalimbali ili wafikie ndoto zao.

Katika Wilaya ya Serengeti, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Dkt.Vincent Mashinji amekabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee uliotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa Wilaya ya Butiama msaada huo umewasilishwa Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo pamoja na maafisa kutoka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii.
Akizungumza mara baada ya kupokea misaada hiyo ya vyakula, Mkurugenzi wa Shirika hilo Rhobi Samwelly amemshukuru Rais Dkt.Samia kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee kwa kuwakumbuka wasichana hao kwa misaada hiyo ya vyakula ambapo amesema ni jambo la faraja kubwa na upendo wa dhati kama ambavyo Mwenyezi Mungu ameelekeza katika vitabu vitakatatifu Quran na Biblia.

"Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Mkuu wetu wa Mkoa ambaye misaada hii kupitia yeye tumeipokea ambayo imewasilishwa na viongozi wakuu wa wilaya hizi. Watoto hawa waone kwamba hawako peke yao, bali watambue kwamba Serikali yetu iko pamoja nao na iko pia mstari wa mbele kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji ndoa za utotoni katika kuhakikisha kwamba vitendo hivi vinamalizika katika nchi yetu ya Tanzania,"amesema Rhobi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news