RC Makongoro:Hata kama ni mwenyekiti wa Halmashauri kamata peleka magereza, tutampata mwingine

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Manyara,RC Makongoro Nyerere amewatuhumu Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Abdulrahaman Kololi kwa kuchochea migogoro ya ardhi kwenye shamba la mwekezaji Dudumera lililopo Kata ya Maisaka.
Makongoro akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) kilichofanyika mjini hapa, amesema viongozi hao wawili wanatuhumiwa kuwachochea wananchi ili wavamie shamba la hilo ambalo bado ni mali ya mwekezaji na kusababisha vurugu.

Amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara kuwakamata watu wanaovamia eneo hilo.

RC Makongoro amesema, hawezi kuvumilia viongozi wanaosababisha migogoro. "Hata kama ni mwenyekiti wa Halmashauri kamata peleka magereza,tutampata mwingine.

"RPC mkawakamate hao vijana, kwani mbunge anahusika na diwani anahusika kuchochea mgogoro ni bora akose hiyo nafasi ili uchaguzi ufanyike na tupate Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya mji," amesema Makongoro.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya siku mbili kutembelea mji wa Babati ambapo katika hotuba yake akizungumza na wananchi kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa Kwaraa, alitoa onyo kwa viongozi na kuwataka kutochochea migogoro ya ardhi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Abdulrahaman Kololi amesema, yeye hawezi kuzungumzia chochote juu ya tuhuma hizo huku Mheshimiwa Gekul akisema anashangazwa na tuhuma hizo kwani yeye amekuwa mpatanishi wa tatizo hilo na siyo kuchochea migogoro ya ardhi.

"Juzi kulitaka kuzuka vurugu pale juu ya mgogoro huo, nilifika na polisi tukawapooza wananchi, leo inakuwaje nasingiziwa kuanzisha mgogoro huo," amehoji Gekul.

Amesema wananchi hao hawajavamia eneo hilo kwani walikuwepo zaidi ya miaka 70 iliyopita hivyo hawapaswi kuondolewa hivi sasa labda wapewe sehemu nyingine ya kufidiwa kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news