Serikali yafanikisha wajasiriamali 300 kushiriki Maonesho ya Juakali nchini Uganda

NA LUSAJO MWAKABUKU

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, imefanikisha ushiriki wa wajasiriamali zaidi ya 300 katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama Juakali yanayoendelea nchini Uganda.
Maonesho ambayo yalianza Desemba 8, 2022 na yanatarajiwa kuhitimishwa Desemba 18, 2022 katika viwanja vya Uhuru vilivyopo Kololo jijini Kampala, Uganda.

Maonesho ya mwaka huu ambayo yamevutia wajasiriamali zaidi 1500 kutoka nchi zote saba Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo kati wajasiriamali hao, asilimia 75 ni wanawake, yamesheheni bidhaa mbalimbali za asili kutoka nchi husika zikiongozwa na kauli mbiu ya maonesho haya “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki kwa Uchumi Stahimilivu na Endelevu”.

Maonesho haya yanalenga kutoa fursa kwa wajasiriamali kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika jumuiya, sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.
Kwa upande wa wajisiriamali wa Tanzania miongoni mwa bidhaa na huduma wanazozionesha ni pamoja na mavazi ya asili, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajasiriamali wa Tanzania wamepongeza juhudi na hatua mbalimbali muhimu zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo.

“Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zetu hadi hapa nchini Uganda, wengi wetu tusingeweza kumudu na tusingekuwa na uwakilishi wa kutosha katika maonesho haya. Lakini kutokana na nia ya Serikali ya kuhakikisha inatusaidia wajasiriamali kukua kibiashara kwa kupata masoko mapya ya bidhaa na huduma tunazozalisha na kutuongeza ujuzi na uzoefu imeona ni vyema itusaidie kwa kutuwezesha katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa usafiri bure wa kutuleta hapa nchini Uganda na kurudi nyumbani,”ameeleza Said Makia, mjasiriamali kutoka Dar es salaam.
Maonesho ya Juakali yalifanyika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba 1999 jijini Arusha ambapo yaliambatana na tukio la kihistoria la kusainiwa kwa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maonesho hayo, Wakuu wa Nchi za Jumuiya Afrika Mashariki walielekeza kuwa yafanyike kila mwaka kwa mzunguko ili kuimarisha mtangamano wa kijamii na kiuchumi wa watu katika jumuiya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news