TUTAENDELEA KUENZI UHUSIANO WA KIDINI NA KIUTAMADUNI NA UGANDA-WAZIRI MKUU

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuenzi uhusiano wa kidini na kiutamaduni kati yake na Uganda.
Amesema hayo leo Desemba 17, 2022 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 75 tangu ulipojengwa msikiti wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Makarere kilichopo Kampala nchini Uganda. Msikiti huo ulifunguliwa na Mwanamfalme Abdullah wa Zanzibar mwaka 1948.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa msikiti huo umekuwa ni chachu ya kuimarisha mahusiano ya enzi kati ya wananchi wa Uganda, Zanzibar na iliyokuwa Tanganyika.
“Nyote mtakubaliana nami kwamba uwepo wetu hapa ni ishara tosha ya kutambua umuhimu na mchango wa tukio hili la kihistoria katika kukuza mahusiano ya watu wetu hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Aidha, Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Uganda na Chuo Kikuu cha Makerere katika kuusimamia Msikiti huo sambamba na kuruhusu Waislamu wa maeneo ya jirani kuutumia kwa ajili ya kuabudu.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa viongozi wa dini kuendelea kukemea mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao umeshika hatamu.

“Katika hili ningeomba turejee maneno ya maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur‘an tukufu Sura ya 33 Ayah 21 (Quran 33:21) kwamba “Hakika ninyi mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu”.

Ameongeza kuwa taasisi za elimu, jumuiya za dini, viongozi wa dini na viongozi wa umma wanao wajibu wa kuilea jamii kwa kutoa elimu sahihi ya mazingira sambamba na mafundisho sahihi na endelevu ya dini ili kuiwezesha kutambua na kufuata yote yaliyo mema kama tulivyo amrishwa na Mwenyezi Mungu na kuacha kabisa yote mabaya yanayomchukiza Mwenyezi Mungu.
“Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa Jumuiya kuongeza juhudi katika kutoa mafunzo ya dini ili kuijengea Jamii hofu ya Mwenyezi Mungu dhidi ya maovu na hivyo, kupunguza au kuondoa kabisa mmomonyoko wa maadili tunaoushuhudia sasa.”

Awali Akizungumza katika maadhimisho hayo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere alisema kuwa Prof. Umaru Kakumba alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ulilenga kujenga maadili mema miongoni mwa wanachuo .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news