Tuunganishe nguvu kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii-Makebo

NA FRESHA KINASA

IMEELEZWA kuwa, vitendo vya ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka ambalo linagusa makundi na jinsi zote katika jamii, hivyo wadau, Serikali na wananchi wote wanapaswa kuunganisha nguvu ili kuweza kutokomeza kwa umoja wao.
Hayo yamesema Desemba 8, 2022 na Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, John Makebo wakati akifungua kikao cha wadau na viongozi wa serikali cha kujadili hali na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika halmashauri hiyo katika hitimisho la Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia, kikao ambacho kilifanyika Kibara katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Kampeni hiyo hufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Decemba 10 kila mwaka ikilenga kubadikishana taarifa na uzoefu, kujengeana uwezo wa pamoja katika kuunganisha nguvu na ushirikiano wa asasi za kijamii katika kuhamasisha, kueleweshana na kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.

Ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema,"kila uhai unathamani tokomeza mauaji ya wanawake na watoto."

Amesema, iwapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake wa kupinga vitendo hivyo ikiwemo kuwafichua wahusika katika vyombo vya sheria itasaidia kwa kiwango stahiki katika mapambano ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake Afisa Ustawi Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Fausta Parali amesema chimbuko la maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni mauaji ya kikatili yaliyofanywa na utawala wa kidikteta wa Jamhuri ya Dominica tarehe 25 Novemba 1960.

Fausta amesema, kampeni hiyo kabambe ni ya Kimataifa ya kupinga ukatili wa kijinsia hasa ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakifanyiwa.

Naye George Mathew kutoka Hospitali ya Kibara amesema, changamoto kubwa iliyopo katika kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia ni pamoja na jamii kuficha taarifa za wahanga.

Mathew amesema, wapo wananchi wanaofika katika hospitali hiyo kwa matibabu wakiwa wamefanyiwa vitendo vya ukatili na kuumizwa japo wahanga hao hutoa taarifa tofauti na tukio halisi.

Amewashauri wadau hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani ukatili usipodhibitiwa madhara yake ni makubwa ikiwemo ulemavu wa kidumu, athari za kisaikolojia na magonjwa ya kuambukiza.

Prisca Simburya ambaye ni msaidizi wa kisheria kutoka kata ya Nyamuswa wilayani Bunda amesema, elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia inapaswa kuwa endelevu na izidi kutolewa kwa makundi yote katika mikutano, matamasha, na mikutano ya kawaida katika jamii.

Akitoa taarifa Afisa Ustawi Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Fausta Parali amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia katika halmashauri hiyo vimekuwa vikiongezeka.
Parali amesema,kwa mwaka huu 2022 matukio ya ukatili yaliyotolewa taarifa katika halmashauri hiyo kuwa ukatili wa kimwili ni 208, ukatili wa kingono ni 640 ,ukatili wa wa kisaikolojia ni 1,364 na matukio ya kutelekezwa ni 74.

John Mkebo kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu amesema, mambukizi ya UKIMWI katika halmashauri hiyo ni asilimia 3.3 huku akina mama wenye maambukizi akisema kuwa ni wengi ukilinganisha na wanaume.

Makebo ameongeza kuwa, hali ya maambukizi imekuwa ikipanda na kushuka hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kwa watu wanaogundulika kuwa na maambulizi ni wale wanaofika katika hospitali na vituo vya afya kwa ajili ya kupima.

Kikao hicho cha wadau kimeandaliwa na halmashauri ya Wilaya ya Bunda kupitia idara ya ustawi wa jamii kwa kushirikiana na Shirika la VICTORIA FARMING AND FISHING ORGANIZATION (VIFAFIO) ambalo linatekeleza mradi wa 'Funguka kutokomeza ukatili wa Kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya Uvuvi katika kata nne za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Robnson Wangaso ni Mratibu wa Mradi wa 'Funguka kutokomeza ukatili wa Kijinsia uliozoeleka maeneo ya uvuvi' kutoka Shirika la VIFAFIO amesema kwamba, anaishukuru serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo katika kata nne za Wilaya ya Bunda na kata saba za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma unafadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society ukiwa na gharama ya shiligi milioni 37 ambapo ni wa miezi nane.

Washiriki hao wamesema, matukio ya ukatili wa kijinsia yanatendwa na watu wa karibu katika jamii hivyo elimu kwa wanajamii inapaswa kuendelee kutolewa na kuwafichua bila haya ndugu wa karibu wanaofanya vitendo hivyo bila kuwahurumia.

Kwa upande wake Afisa Elimu Watu Wazima Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Florence Njiku amesema wadau hawana budi kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia ikiwemo watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

Katika kikao hicho, wadau wamekubaliana kuendelea kutoa elimu ya malezi na makuzi katika jamii, elimu ya ulinzi na usalama wa mtoto na namna ya kulinda haki za watoto, wanawake na watu wote.

Wadau hao baada ya kikao walitembelea Kituo cha Matumaini ambacho ni Makao ya watoto Yatima kilichopo Bunere Kata ya Chitengule.
Wakiwa kituoni hapo wakiongozwa na maafisa ustawi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda waliwafundisha watoto juu ya haki zao na wajibu. Na kukabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya watoto hao kama sukari na vitu vingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news