Prof.Muhongo awasilisha maombi ya kupaisha uchumi wa Mara kwa Rais Dkt.Samia

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo ametoa maombi na mapendekezo kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yatakayosaidia kukuza uchumi wa mkoa huo.
Mheshimiwa Prof. Muhongo amewasikisha maombi na masuala ya kiuchumi ya Mkoa wa Mara katika mkutano Mkuu wa 10 wa CCM uliofanyika jijini Dodoma tarehe 7 na 8 Decemba, 2022.

"Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara tunakupatia pongezi nyingi sana kwa imani uliyoipata kwenye mkutano huu, hongera sana.

"Mkoa wa Mara tunaomba Mwenyekiti wa Chama na Rais wetu utusaidie kwenye maeneo ya kiuchuni, lakini kabla sijagusia vitatu ambavyo tunaviomba nianze na Chuo cha Mwalimu Nyerere kimekaa kwenye Ilani ya Chama, tunatoa shukrani nyingi sana kwa sababu umewezesha fedha kutoka Benki ya Dunia kuanza kujenga kile chuo.

"Pendekezo letu tunaomba chuo kile kianze kufanya kazi kwa sababu kawaida ya chuo kuanza kwa vyuo sio lazima chuo chote kijengwe. Mzee Warioba (Joseph Sinde Warioba) atakumbuka wao chuo Kikuu cha Dar es laam walianza kusomea Lumumba wakati wanajenga kule Mlimani, kwa hiyo Mheshimwa Rais tunaomba mwakani chuo cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo kianze kutoa mafunzo kwa sababu kuna sehemu za kuanza kutoa mafunzo," Prof. Muhongo amesema na kuongeza kuwa,

"Pili Chuo cha Mwalimu Nyerere ile Hospitali uliokwenda kuizindua ya Kwangwa Musoma tulitoa mapendekezo kiwe na Kitivo cha AfyA, tunashukuru Serikali, Mkoa wa Mara tuna vituo vya afya vingi, zahanati nyingi, Hospitali za wilaya...tutoe shukurani nyingi sana kwako,"amesema.

Pia, Prof. Mubongo ameomba Mkoa wa Mara uzalishe wafanyakazi kwenye sekta ya afya waanze pale Hospitali ya Mwalimu Nyerere Kwangwa Musoma.

Kuhusiana na mkoa wa Mara jinsi ambavyo umebarikiwa kuwa na ardhi bora ya kuzalisha mazao, Prof. Muhongo amesema."Mheshimiwa Rais, Mkoa wa Mara unaweza ukalisha Taifa hili, tunashukuru sana umeanza kutoa ahadi tunashukuru wewe ni muungwana ahadi imetekelezwa ila tunaomba kasi iongezeke,"amesema.

Aidha, Mheshimiwa Prof. Muhongo amesema Mkoa wa Mara utapiga hatua za kimaendeleo kufuatia uwepo wa bonde la Bugwema na Bonde la Mto Mara.

"Tunataka Mkoa wa Mara tuwe na mradi wa umwagiliaji, kuna bonde la Bugwema na Mto Mara tukipate hii miradi mikubwa ya umwagiliaji tutalisha Tanzania yote tuna mazao matano tumeshayaainisha tutalima pamba, alizeti, mahindi, mpunga na dengu kwa hiyo ombi kutoka Mkoa wa Mara ni kuhusu kilimo cha umwagiliaji.

"Tukishapata pamba nyingi, Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa CCM ndio maana tunakuomba utusaidie kiwanda chetu cha MUTEX, kile kiwanda ndio kilikuwa kinashika uchumi wa Mkoa wa Mara. Kwa kuwa tunapamba nyingi tunaomba kiwanda kidogo cha kisasa cha nguo, kiwanda cha kwanza hicho,"amesema Mheshimiwa Prof.Muhongo.

"Ziwa Victoria, wavuvi mashuhuri kwenye maziwa Tanzania nzima wako Mkoa wa Mara. Kwa hiyo sisi tunaomba Mkoa wa Mara tuvue samaki wengi ambao tunaweza tukalisha Tanzania nzima. Lakini huo uvuvi Mheshimiwa Mwenyekiti lazima uwe wa kisasa na uwe uvuvi wa vizimba,"amesema.

Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa hatua yake ya kutafuta fedha ambazo zitatolewa kwa wavuvi ili kuleta ufanisi.

"Nakupatia shukrani nyingi sana, umeweza kutafuta fedha na karibuni tataanza uvuvi wa vizimba sasa mahala pa kuwekeza kama Taifa ni kwenye Ziwa Victoria, Mkoa wa Mara una wavuvi wengi wazoefu," amesema Prof. Muhongo.

"Tukishapata samaki wengi vile viwanda vya Mkoa wa Mara ambavyo ni kama vimekufa, na samaki wachache wanaotoroshwa kwenda Kisumu nchini Kenya basi tutafufua na kuanzisha upya viwanda vingine vya samaki, kiwanda cha aina ya pili."

Prof.Muhongo ameomba pia Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kusaidia kuvifufua kiwanda cha maziwa cha Utegi kilichopo Rorya na kiwanda cha maziwa cha Musoma ambavyo vina mchango mkubwa wa uchumi katika Mkoa wa Mara.

"Na cha mwisho Mheshimiwa mwenyekiti tuna uzoefu, tulikuwa na kiwanda cha maziwa cha Utegi na kiwanda cha maziwa cha Musoma Mjini, Mheshimiwa viwanda vyote havifanyi kazi, teknolojia inakuwa ya zamani kidogo. Kwa uchumi wa Mkoa wa Mara tunaomba Serikali itusaidie. Tuwe na kiwanda cha maziwa tena, serikali itusaidie tuwe na kiwanda cha nguo tena.

"Mheshimiwa Rais, na mwisho, kwa kuwa umesema tutoe changamoto tunashukuru miradi inaenda vizuri sisi ombi letu kasi ya miradi tuna barabara tatu muhimu Tarime-Serengeti, Musoma-Makojo-Busekera na kutoka Butiama-Serengeti, Mheshimiwa tunaomba utuongeze bajeti na wakandarasi waongeze kasi. Namalizia kwa kutoa pongezi nyingi sana za dhati, kwani Mkoa wa Mara unafaidi sana fedha za miradi zinazotoka serikalini chini ya usimamizi wako,"amesema Prof. Muhongo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news