TWASHEREHEKEA UHURU, KAZI INAENDELEA-6:Naye Dkt.Samia Suluhu Hassan, Niseme kwa kutulia

NA LWAGA MWAMBANDE

MHESHIMIWA Dkt.Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dkt.Samia aliapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Ndugu Samia ni mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, yapo mengi ya kumweleza mama huyu hodari katika uongozi wakati tukisherehekea miaka 61 ya Uhuru leo Desemba 9, endelea;


1:Kwa mara ya kwanza, Mama, sasa yuko kileleni,
Ni Rais kasimama, tayari yuko kazini,
Mwaka mmoja mzima, wa pili uko njiani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

2.Msiba lipoingia, wa Magufuli kifoni,
Kaja Rais Samia, kushikilia mpini,
Yale alituambia, afanya yamesheheni,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

3:Kwanza litahadharisha, walioko mitaani,
Ambao walinganisha, mwanamke kileleni,
Wazi liwafahamisha, ameshakaa kitini,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

4:Yale mazitomazito, aliyashika shingoni,
Tusibaki tumbo joto, ilivyokuwa zamani,
Mara akatoa wito, tujitoe kifungoni,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

5:Kujitenga ya UVIKO, yote akapiga chini,
Kwenda dunia iliko, pamoja kuwa vitani,
Kokote chanjo ziliko, kaita zije nyumbani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

6:Chanjo kwetu kuingia, sema changamkieni,
Ni yeye alianzia, akadungwa mabegani,
Wengi tulomwangalia, tukaruhusu mwilini,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

7:Kufanya hivyo hakika, nasi tuko duniani,
Faida zimeshafika, mijini na vijijini,
Sasa tunaaminika, na safari duniani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

8:Wapinzani hawakosi, kusema ya mdomoni,
Kwamba amefanya hasi, chanjo kuleta nchini,
Yeye liongeza kasi, chanjo ni nyingi nchini,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

9:Miradi kimkakati, kaishika mikononi,
Tena inapanda chati, tekelezaji makini,
Amesema yuko fiti, ifikie kileleni,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

10:Rais Samia wetu, amekwenda duniani,
Sasa huko nchi yetu, tamba mambo ya kigeni,
Ni nyingi faida kwetu, kujiunga duniani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

11:Maka kawa stelingi, picha bora ya nchini,
Kaupiga sana mwingi, kwa utalii nchini,
Royal Tour ya msingi, filamu i duniani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

12:Watalii Tanzania, wale walishuka chini,
Sasa wengi waingia, Samia yuko kazini,
Jinsi aliigizia, kwetu fedha za kigeni,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

13:Niseme kwa kutulia, hili latoka moyoni,
Ana Suluhu Samia, kwake yamkaa dini,
Yale ametufanyia, sifa kote duniani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

14:Ni hawa Watanzania, tuitao wapinzani,
Mazuri kawafanyia, iwaingie Imani,
Jana singefikiria, wangeishi kwa Amani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

15:Ameunyosha mkono, kuuachia mpini,
Alisema kwa maneno, matendo yako kazini,
Siasa rafiki mno, kama Kikwete zamani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

16:Alivyokwenda Ulaya, kule watu ugenini,
Akaona si vibaya, kuchati na mpinzani,
Tunasema bila haya, huyu mtu wa Amani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

17:Nchi ameifungua, mitaja yaja nchini,
Wigo ameutanua, uhuru wa mdomoni,
Michezo ameinua, tunatamba duniani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

18:Kazi inaendelea, hiyo yake slogani,
Wengi tunapendelea, tuzidi kuwa kazini,
Nchi itaendelea, tuwe juu duniani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

19:Bado atutumikia, Ikulu kwake nyumbani,
Twamwaminia Samia, tatufikisha Kanani,
Kule tutafurahia, kwa upendo na Amani,
Twashereheka Uhuru, kazi inaendelea.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news