Usafi ni kinga dhidi ya Ebola-Wizara

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imesema, ushirikano wa pamoja na wadau mbalimbali nchini unahitajika ili kuendelea kuwajengea wanajamii uwelewa wa kutosha ili waweze kuzingatia miongozo na kanuni mbalimbali za usafi nchini.
Wakati huo huo,kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini, hivyo katika mipaka na vituo vya afya wameweka wataalamu na utaratibu muhimu.

Mafanikio ya kuzingatia kanuni na taratibu hizo katika maisha ya kila siku yanatajwa yatawezesha jamii kuyashinda magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Ebola na mengineyo.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam na Dkt.Joseph Hokororo ambaye ni Mratibu wa Kujikinga na Kudhibiti Maambukizi Wizara ya Afya.

Ni wakati akiwasilisha mada katika siku ya kwanza ya mafunzo ya kuwajengea waandishi wa habari uelewa kuhusu namna bora ya kutoa elimu ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola iwapo utaingia hapa nchini.
Ebola ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kasi ambao unasababisha kifo kama hatua za haraka hazitachukuliwa, umepewa jina hilo la mto uitwao Ebola uliopo Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako ulijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1976.

"Kwa hiyo, ushirikiano wa pamoja ni muhimu sana, pia tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunaendelea kuelimisha jamii zetu ili ziweze kuwa na ustaarabu wa kuzingatia miongozo na kanuni za usafi.

"Magonjwa yote duniani, kadri nchi ilivyo na uchumi mzuri ndivyo inafanikiwa kuyadhibiti mapema, kwa sababu mifumo ya afya, wataalamu wa afya wapo wa kutosha kwa ajili ya kushughulikia magonjwa hayo.
"Kwa sababu ni rahisi pale ambapo mgonjwa anaripotiwa au kisa chochote cha ugonjwa, inakuwa rahisi wao kuchukua hatua za haraka, lakini nchi ambazo uchumi wake na mifumo ya afya ipo vibaya, si rahisi kudhibiti magonjwa.

"Nina uhakika kwa Tanzania kwa namna aambavyo tulivyojipanga na namna mfumo wa afya ulivyo, ni rahisi kukabiliana na magonjwa, ingawa hatuwezi kujilinganisha na nchi kama Marekani,"amefafanua.

Pia amesema, vijidudu vya Ebola vikiingia mwilini jambo la kwanza ambalo huwa vinaenda kufanya ni kushambulia kinga mwili.

"Baada ya hapo vinakuacha ukiwa hauna kinga yoyote mwilini, hivyo ndiyo maana tunashauri kila mmoja achukue tahadhari na pale ambapo anaona dalili za ugonjwa huo achukue hatua za haraka kuripoti kituo cha afya,"amesema Dkt.Hokororo.
Amesema, iwapo mtu anabainika kuwa anaugua ugonjwa wa Ebola bila kujali ni ndugu wa karibu inashauriwa kutomgusa au kuaribiana naye badala yake apelekwe kituo cha matibabu kwa hatua zaidi ili kuepuka kupata maambukizi zaidi.

"Tusiguse mtu au eneo au kushirikiana vyombo mbalimbali kwa maana ya kushika vyombo ambavyo havijafanyiwa usafi kwa kutumia kemikali ambazo hazina madhara kwa vifaa husika ili kuepuka kuenea kwa maambukizi zaidi, iwe simu au chochote, mathalani matumizi ya vitakasa mikono ni rafiki zaidi katika kudhibiti maambukizi,"amefafanua Dkt.Hokororo.

Dkt.Hokororo amefafanua kuwa, wagonjwa wa Ebola wamegawanyika katika makundi matatu. "Kundi la kwanza ni wale ambao wanahisiwa kuwa ni wagonjwa, hawa wanatakiwa kutengwa, na kupelekwa Ebola Treatment Units (ETU), na waliothibitishwa.
"Wengine ni wale ambao walikutana na wahisiwa au wagonjwa na wanapaswa kufuatiliwa ndani ya siku 21, wanafuatiliwa hatua kwa hatua kama mtu amepata dalili kuhusu ugonjwa wa ebola. Hivyo, na hao wanapaswa kutengwa, na kuna njia mbalimbali ikiwemo kufungiwa katika hosteli,"amesema Dkt.Hokororo.

Aidha, amesema mwanaume ambaye ameambukizwa Ebola na akapona ndani ya siku 21, ana uwezekano wa kuambukiza Ebola ndani ya mwaka mmoja kupitia manii zake, vivyo hivyo kwa mama anayenyoyesha anaweza kumuambukiza mtoto wake.
"Kumbuka kuwa, mtu akishaugua Ebola, na ukawa katika kambi ambapo baadaye wamekuchunguza na kukugundua kuwa umepona,vijidudu vinaweza kukaa kwa miezi sita, hivyo inashauriwa baada ya kuruhusiwa kuchukua taadhari kwa miezi sita ikiwemo kutumia kinga baada ya hapo unaweza kuendelea,"amefafanua.

Naye Said Chibwana ambaye ni Mtaalamu wa Kujikinga na Kudhibiti Maambukizi kutoka Jamii Bora Health Services Network amesema kuwa, kuosha mikono kwa kufuata taratibu na miongozo ya afya inawezesha kuepusha mtu kuepukana na magonjwa ya milipuko kama vile Ebola au Corona.
Chibwana amesema, kuna njia nne za uoshaji wa mikono ikiwemo kwa kutumia maji na sabuni, matumizi ya maji kimininika yenye dawa katika maeneo mbalimbali hususani kwenye milipuko, matumizi ya vitakasa mikono.

"Kama mikono haina uchafu unaoonekana.Iwapo unaona mikono yako ina uchafu unaoonekana unapaswa kutumia sabuni na maji. Njia nyingine ni ile inayotumika katika maeneo ya vituo vya afya,"amefafanua Chibwana.

Mtaalamu huyo amefafanua kuwa, ili kuifanya mikono yako iwe salama yafaa wakati wa kuosha kusugua na baada ya hapo kutumia kitambaa kikavu au tishu kwa ajili ya kukausha.
"Hatua ya kwanza ni kufungua koki ya maji,kulowanisha mikono, unaweka sabuni, unatengeneza povu (kunakuwepo msuguano kati ya viganja viwili) na kuendelea. Asilimia kubwa ya magonjwa ya kuambukiza chanzo kikuu kimekuwa ni uoshaji wa mikono usiofaa, hivyo jamii inashauriwa kuzingatia usafi wa mikono ili kuwa salama.

"Mikono iwe safi, watu waoshe mikono mara kwa mara, vile vile vifaa vya kunawia ambavyo vinatumika zaidi ya mara moja yafaa kufanyiwa usafi kwa maana ya kuvitakasa ili kuweza kuendelea kutoa huduma.
"Pia matumizi ya kinga mwili, kwa ajili ya kujiepusha na magonjwa ya kuambukiza na vinapaswa kutumika kwa usahihi kama vile mipira ya mikono (gloves),"amefafanua Chibwana.

Unaambukizwaje?

Ebola huweza kuambukizwa kupitia binadamu na wanyama. Pia unaambikizwa kwa kugusana kwa damu au kwa njia ya jasho.

Ripoti za hivi karibuni zinabainisha kuwa, wafanyakazi wa afya wamekuwa wakipata maambukizi wakati wakiwatibu wagonjwa.

Hii inatokea wakati wanapogusana na mgonjwa bila ya kuvaa mipira ya mikono (gloves),barakoa au miwani ya kufunika macho.
Aidha,baadhi ya maeneo ya Afrika, maambukizi yamekuwa yakiripotiwa kupitia watu kugusa au kula nyama za sokwe, nyani, popo, digidigi na mizoga iliyokufa kutokana na virusi hivyo.

Katika hatua nyingine, waombolezaji ambao wamegusana na mtu aliyekufa kutokana na virusi vya Ebola pia huweza kupata maambukizi, huku maambukizi kupitia shahawa kwa kujamiiana huanza kuonesha dalili hadi kufikia wiki saba tangu kupona.

Kuna dalili?

Inaelezwa kuwa, mara nyingi hakuna dalili mahsusi, hali inayofanya kuwa vigumu kuubaini ugonjwa huo. Mgonjwa mara nyingi hugundulika kutokana na kupata joto la ghafla, kudhoofu mwili, kuumwa viungo vya mwili, kuumwa kichwa sana na koo kukauka.

Hayo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, kuwashwa, figo kushindwa kufanya kazi pamoja na ini, katika baadhi ya kesi, kutokwa damu ndani na nje ya mwili.
Dalili huweza kuonekana kati ya siku mbili hadi 21 tangu kupata maambukizi. Baadhi ya wagonjwa hupata miwasho, macho kuwa mekundu, kwikwi, maumivu ya kifua, kupata shida kupumua na kumeza chakula.

Aidha, hakuna tiba maalumu au chanjo ambayo inapatikana kwa sasa kwa ajili ya Ebola, lakini majaribio yanaendelea.
Njia mbadala ya kutibu Ebola ni kupitia matibabu. Hii inajumuisha kumpatia mgonjwa maji ya kutosha, kudhibiti hewa na shinikizo la damu na kuwatibu kwa magonjwa mengine wanayoyapata.
Licha ya ugumu wa kutambua ugonjwa wa Ebola katika hatua za awali, wale ambao wataonesha dalili ni lazima watengwe na wataalamu wa afya wafahamishwe.

Pia huduma huweza kuendelea kutolewa kwa kuvaa nguo maalumu hadi pale sampuli za vipimo kutoka kwa mgonjwa zitakapotolewa kuthibitisha ugonjwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news